Header Ads

Header Ads

Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu? Soma Hapa.

Mfano wa jengo la ghorofa moja katika hatua za ubunifu. Ukiwa na mahitaji ya kufanya ubunifu wa jengo lako, wasiliana nasi tutakusaidia. 
Mara nyingi tunajenga nyumba zetu za kuishi au kwa shughuli za kiofisi/biashara kwa kutumia malighafi ya tofali. Vipande vya mawe, tofali nk huungwa moja moja juu ya jingine kwa mpishano maalumu kwa kutumia mota ya simenti na mchanga na hatimaye kupata kitu kinachoitwa ukuta wa nyumba. Aghalabu malighafi na aina ya tofali ikawa tofauti kutegemeana na sababu mbalimbali.

Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jingo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi au tuseme kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

Ukuta tunaouzungumzia hapa ni ule unaoitwa kitaalamu kama ‘masonry wall’ au ukuta wa tope ambao ni matokeo ya utaalamu wa ufundi uashi. Fundi huyu hutumia mota iliyotokana na mchanganyiko wa simenti (au chokaa, udongo nk), mchanga na maji kwa uwiano maalumu kutengeneza kiunganishi (bonding materials). Mchanganyiko huu ukiwa na utepetepe kiasi huunganisha kipande kimoja kimoja cha ama tofali, jiwe, marble, granite, vigae n.k. Tofali linaweza kuwa ama la kuchoma (brick) au yatokanayo na simenti na mchanga pekee au pamoja na kokoto (blocks). 

Yapo majengo yaliyojengwa kwa kuta za zege, mbao au malighafi nyingine. Hatutaweza kutazamia hayo. Tutajikita zaidi kuangazia masonry walls kama nilivyotambulisha awali.

Kwa sehemu kubwa ya ujenzi wetu, katika kujenga ukuta wa tope tunatumia simenti kama kemilikali unganishi muhimu zaidi. Simenti nayo ina ubora tofauti kutegemeana na matumizi. Zipo simenti za aina nyingi kwa matumizi tofauti, tutakuja kuzifahamu wakati mwingine.
Jambo la msingi sana kufahamu, ukuta wa nyumba yako utakuwa imara na wa kudumu zaidi kutegemeana na mambo makubwa matatu
1.   Aina ya ukuta unaojenga, mtindo na muundo wake (ukuta wa mawe, tofali,
2.   Ubora wa malighafi uliyotumia kulingana na hali nyingine za mazingira
3.   Ufundi sahihi katika kujenga ukuta
Kulingana na aina ya malighafi inayotumika kujenga ukuta wa tope, inaweza kuwa ni mawe, tofali n.k tunaweza kupata ubora na uimara tofauti ambao utawezesha kuwako kwa aina mbili kuu za ukuta kutokana na nafasi yake kwenye jengo.
1.   Ukuta unaobeba uzito wa jengo (Load Bearing Masonry Walls)
2.   Ukuta usiobeba uzito wa jengo (Non Load Bearing Masonry Walls)
Aina ya kwanza ya Ukuta unaobeba uzito wa jengo, hujengwa kwa kutumia matofali ya kuchoma, mawe, au matofali ya zege/mchanga. Kazi ya ukuta wa aina hii mbali na kugawanya vyumba na kutoa usiri, hufanya kazi kubwa ya kuchukua na kusafirisha uzito wa paa ama jengo jingine la juu kama ni nyumba ya ghoroa na kuupeleka kwenye msingi wa jengo na hatimaye ardhini.
Mfundi ujenzi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa msingi wa nyumba, msingi wa tofali
Kuna unafuu wa gharama kama ukijenga ghorofa kwa kutumia ukuta wa aina hii badala ya nguzo na bimu za zege, hasa kwa jingo la ghorofa moja. Jambo muhimu ni ubora wa malighafi na unene wa ukuta, bila kusahau uwiano wa urefu na unene (slanderness ratio), na huku uimara wa msingi wa jengo katika dhibiti kucheza kwa ardhi kukiwa na umuhimu mkubwa. Kwa hiyo kuta hizi hufanya kazi ya kusafirisha uzito kama mbadala nguzo za zege na nondo. Unafuu unaweza usionekane pia kama eneo unalojenga litalazimu kuwa na msingi wa jamvi nene la zege (raft foundation)
Msingi wa nyumba ukiwa tayari kwa kujenga kuta za kugawanya vyumba. Msingi wa namna hii unauwezo wa kuhimili nguvu zinazoweza kusababisha nyufa. 
Hata hivyo, kuna hatari ya kutokea nyufa kwenye kuta za namna hii kutokana na kukosekana kwa fremu ya nondo na zege ambayo husaidia kukabiliana na nguvu mgandamizo (compression force) na nguvu za utengano (tension forces). Nyufa hizi huwa hatari zaidi kama zitashuka mpaka kuvuka msingi wa jengo.

Mashaka ya jengo kutohimili kutokea kwa nyufa ni hasa wakati wa kukabiliana na matukio kama tetemeko la ardhi, mvua kubwa na upepo mkali, na bila kusahau misukumo ardhini na kuyumba kwa utulivu wa msingi wa jengo (earth pressure & differential foundation settlement). Kufikiria hatari hizi, unalazimika kujihami kwa kushirikisha wataalamu ili kuondokana na mashaka  
Uzito (loads) tunaouzungumzia hapa ni mjumuisho wa uzito wa kuta zenyewe, watu na vilivyomo ndani ya jengo, paa la jengo na nguvu ya upepo (imposed & dead loads). Vipimo vya matofali kwa viwango vyetu ni mm 450x230x150 na mm 450x230x100 ambayo kwa lugha za mafundi huzungumzia inchi 9 (tofali la kulaza), 6, 5 na 4 (tofali la kusimama). Kama utatumia tofali kwa ajili ya ukuta unaobeba uzito, ni wazi kuwa utahitajika kujenga ukuta mnene (tofali za zege za kulaza) ambao utakuwa haupungui mm 225 (inchi 9). Kuta nyingine nyembamba unaweza kuzitumia kwa ajili ya kugawanya vyumba.
Hata hivyo, unene wa ukuta utaongezeka kutegemeana na matumizi ya jengo (occupancy) sambamba na idadi ya ghorofa juu ya “floor” ya chini inayogusana na ardhi.
Kwa ujenzi wa ghorofa, ni sahihi zaidi kujenga kuta za chini kwa mtindo wa mchanganyiko wa tofali pamoja na nguzo chache za zege na nondo zilizoungwa na bimu kuzunguka jengo zima, zikiunganishwa na slabu. Wahandisi wabunifu majengo (Structural/Civil Engineers) wanaweza kukusaidia kupata vipimo sahihi.
Ujenzi wa linta ambayo pia inatumika kuunganisha nyumba nzima kama ring beam. Ni aina ya ujenzi wa kawaida mitaani kwetu na matokeo huwa bora kama mafundi wataalamu watatumika. 
Aina ya pili, Ukuta usiobeba uzito wa jengo ni kuta ambazo kazi yake kubwa ni kugawa vyumba (partition walls) kwa ajili ya usiri na kulinda waliomo ndani dhidi ya hatari za nje. Katika jengo lenye kuta za namna hii kunakuwa na kuta nyingine ama nguzo ambazo ni maalumu kwa ajili ya kusafirisha uzito, mathalani maghorofa mengi tunayoyaona yakijengwa mijini. Kuta hizi hazilazimiki kuwa nene sana na ndio maana unaweza kujenga ukuta wa inchi 4 tu kwa ajili ya kugawanya maeneo ya choo na bafu. 
Mfano wa nyumba ya kuishi iliyokamilika . PICHA ZOTE NI HATI MILIKI YA BLOGU HII

No comments: