• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Showing posts with label Uswazi. Show all posts
Showing posts with label Uswazi. Show all posts

Thursday, February 22, 2018

Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N? Soma hapa kujua ubora tofauti wa simenti




Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu. 

Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi. Kwa baadhi ya nchi wana simenti ya uimara wa juu zaidi ya kipimo cha 52.5.

Kwa ujumla simenti hutumika kwa kutengenezea matofali, kuteneneza plaster na chipping, kusakafia, kuziba cracks, kuunganishia matofali kutengeneza ukuta, kutengenezea zege nk. 

Si ajabu ukaenda dukani na kunua saruji ya OPC ikiwa na mifuko yenye maandishi ya ubora kama 32.5N, 32.5R, 42.5N, 42.5R au hata 52.5N. Hizi herufi ‘N’ au ‘R’ hazina maana yeyote zaidi ya kuelezea kipindi cha mapema zaidi (umri) kwa simenti kuanza kufikia ubora wake ukipimwa katika siku 2 au 7.

Ni bahati nzuri Tanzania sasa ina viwanda vingi vya kuzalisha portland cement ambavyo hutambulika kwa majina kama Twiga Cement, Simba Cement, Tembo Cement, Moshi Cement, Dangote Cement n.k. WIngi huu wa wazalishaji huleta nafuu kwa walaji kupitia ushindani wa soko kibiashara.  

Tabia moja ya zege (mchanganyiko wa kokoto, mchanga na simenti katika uwioano uliopimwa na kuchanganywa na maji) huendelee kuwa bora kadiri siku zinavyoongezeka. Katika upimaji product ya zege, ubora hupimwa baada ya siku saba kuona kama kuna uwezekanao wa kufikia ubora unaotarajiwa huko baadae. Kipimo cha siku saba kikionesha kutoatoa majibu ya mwelekeo mzuri basi zege husika inabomolewa. Halafu kuna kipimo baada ya umri wa siku 14 na baadae siku 28 kuhitimisha kwamba viwango vya ubora vitafikiwa kadiri umri wa zege unavyoongezeka.  

Karibu tena Tujifunze!

Friday, December 22, 2017

Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu? Soma Hapa.

Mfano wa jengo la ghorofa moja katika hatua za ubunifu. Ukiwa na mahitaji ya kufanya ubunifu wa jengo lako, wasiliana nasi tutakusaidia. 
Mara nyingi tunajenga nyumba zetu za kuishi au kwa shughuli za kiofisi/biashara kwa kutumia malighafi ya tofali. Vipande vya mawe, tofali nk huungwa moja moja juu ya jingine kwa mpishano maalumu kwa kutumia mota ya simenti na mchanga na hatimaye kupata kitu kinachoitwa ukuta wa nyumba. Aghalabu malighafi na aina ya tofali ikawa tofauti kutegemeana na sababu mbalimbali.

Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jingo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi au tuseme kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

Ukuta tunaouzungumzia hapa ni ule unaoitwa kitaalamu kama ‘masonry wall’ au ukuta wa tope ambao ni matokeo ya utaalamu wa ufundi uashi. Fundi huyu hutumia mota iliyotokana na mchanganyiko wa simenti (au chokaa, udongo nk), mchanga na maji kwa uwiano maalumu kutengeneza kiunganishi (bonding materials). Mchanganyiko huu ukiwa na utepetepe kiasi huunganisha kipande kimoja kimoja cha ama tofali, jiwe, marble, granite, vigae n.k. Tofali linaweza kuwa ama la kuchoma (brick) au yatokanayo na simenti na mchanga pekee au pamoja na kokoto (blocks). 

Yapo majengo yaliyojengwa kwa kuta za zege, mbao au malighafi nyingine. Hatutaweza kutazamia hayo. Tutajikita zaidi kuangazia masonry walls kama nilivyotambulisha awali.

Kwa sehemu kubwa ya ujenzi wetu, katika kujenga ukuta wa tope tunatumia simenti kama kemilikali unganishi muhimu zaidi. Simenti nayo ina ubora tofauti kutegemeana na matumizi. Zipo simenti za aina nyingi kwa matumizi tofauti, tutakuja kuzifahamu wakati mwingine.
Jambo la msingi sana kufahamu, ukuta wa nyumba yako utakuwa imara na wa kudumu zaidi kutegemeana na mambo makubwa matatu
1.   Aina ya ukuta unaojenga, mtindo na muundo wake (ukuta wa mawe, tofali,
2.   Ubora wa malighafi uliyotumia kulingana na hali nyingine za mazingira
3.   Ufundi sahihi katika kujenga ukuta
Kulingana na aina ya malighafi inayotumika kujenga ukuta wa tope, inaweza kuwa ni mawe, tofali n.k tunaweza kupata ubora na uimara tofauti ambao utawezesha kuwako kwa aina mbili kuu za ukuta kutokana na nafasi yake kwenye jengo.
1.   Ukuta unaobeba uzito wa jengo (Load Bearing Masonry Walls)
2.   Ukuta usiobeba uzito wa jengo (Non Load Bearing Masonry Walls)
Aina ya kwanza ya Ukuta unaobeba uzito wa jengo, hujengwa kwa kutumia matofali ya kuchoma, mawe, au matofali ya zege/mchanga. Kazi ya ukuta wa aina hii mbali na kugawanya vyumba na kutoa usiri, hufanya kazi kubwa ya kuchukua na kusafirisha uzito wa paa ama jengo jingine la juu kama ni nyumba ya ghoroa na kuupeleka kwenye msingi wa jengo na hatimaye ardhini.
Mfundi ujenzi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa msingi wa nyumba, msingi wa tofali
Kuna unafuu wa gharama kama ukijenga ghorofa kwa kutumia ukuta wa aina hii badala ya nguzo na bimu za zege, hasa kwa jingo la ghorofa moja. Jambo muhimu ni ubora wa malighafi na unene wa ukuta, bila kusahau uwiano wa urefu na unene (slanderness ratio), na huku uimara wa msingi wa jengo katika dhibiti kucheza kwa ardhi kukiwa na umuhimu mkubwa. Kwa hiyo kuta hizi hufanya kazi ya kusafirisha uzito kama mbadala nguzo za zege na nondo. Unafuu unaweza usionekane pia kama eneo unalojenga litalazimu kuwa na msingi wa jamvi nene la zege (raft foundation)
Msingi wa nyumba ukiwa tayari kwa kujenga kuta za kugawanya vyumba. Msingi wa namna hii unauwezo wa kuhimili nguvu zinazoweza kusababisha nyufa. 
Hata hivyo, kuna hatari ya kutokea nyufa kwenye kuta za namna hii kutokana na kukosekana kwa fremu ya nondo na zege ambayo husaidia kukabiliana na nguvu mgandamizo (compression force) na nguvu za utengano (tension forces). Nyufa hizi huwa hatari zaidi kama zitashuka mpaka kuvuka msingi wa jengo.

Mashaka ya jengo kutohimili kutokea kwa nyufa ni hasa wakati wa kukabiliana na matukio kama tetemeko la ardhi, mvua kubwa na upepo mkali, na bila kusahau misukumo ardhini na kuyumba kwa utulivu wa msingi wa jengo (earth pressure & differential foundation settlement). Kufikiria hatari hizi, unalazimika kujihami kwa kushirikisha wataalamu ili kuondokana na mashaka  
Uzito (loads) tunaouzungumzia hapa ni mjumuisho wa uzito wa kuta zenyewe, watu na vilivyomo ndani ya jengo, paa la jengo na nguvu ya upepo (imposed & dead loads). Vipimo vya matofali kwa viwango vyetu ni mm 450x230x150 na mm 450x230x100 ambayo kwa lugha za mafundi huzungumzia inchi 9 (tofali la kulaza), 6, 5 na 4 (tofali la kusimama). Kama utatumia tofali kwa ajili ya ukuta unaobeba uzito, ni wazi kuwa utahitajika kujenga ukuta mnene (tofali za zege za kulaza) ambao utakuwa haupungui mm 225 (inchi 9). Kuta nyingine nyembamba unaweza kuzitumia kwa ajili ya kugawanya vyumba.
Hata hivyo, unene wa ukuta utaongezeka kutegemeana na matumizi ya jengo (occupancy) sambamba na idadi ya ghorofa juu ya “floor” ya chini inayogusana na ardhi.
Kwa ujenzi wa ghorofa, ni sahihi zaidi kujenga kuta za chini kwa mtindo wa mchanganyiko wa tofali pamoja na nguzo chache za zege na nondo zilizoungwa na bimu kuzunguka jengo zima, zikiunganishwa na slabu. Wahandisi wabunifu majengo (Structural/Civil Engineers) wanaweza kukusaidia kupata vipimo sahihi.
Ujenzi wa linta ambayo pia inatumika kuunganisha nyumba nzima kama ring beam. Ni aina ya ujenzi wa kawaida mitaani kwetu na matokeo huwa bora kama mafundi wataalamu watatumika. 
Aina ya pili, Ukuta usiobeba uzito wa jengo ni kuta ambazo kazi yake kubwa ni kugawa vyumba (partition walls) kwa ajili ya usiri na kulinda waliomo ndani dhidi ya hatari za nje. Katika jengo lenye kuta za namna hii kunakuwa na kuta nyingine ama nguzo ambazo ni maalumu kwa ajili ya kusafirisha uzito, mathalani maghorofa mengi tunayoyaona yakijengwa mijini. Kuta hizi hazilazimiki kuwa nene sana na ndio maana unaweza kujenga ukuta wa inchi 4 tu kwa ajili ya kugawanya maeneo ya choo na bafu. 
Mfano wa nyumba ya kuishi iliyokamilika . PICHA ZOTE NI HATI MILIKI YA BLOGU HII

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU? - PART III: SOMA HAPA UNACHOTAKIWA KUFANYA UKITAKA KUJENGA NYUMBA KISASA



ILIPOISHIA SEHEMU YA TATU


Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya maaandalizi muhimu yatakayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. 

Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.

Mfano wa ramani ya nyumba


Jambo la kuanza nalo ni kufikiria mahali sahihi utakapo jenga nyumba yako


Mahali unapotamani kujenga makazi yako yanahusika kuamua aina ya nyumba yako hapo baadae. Inaweza kuwa unawazia kujenga nje ya mji au mjini. Eneo unalotamani kujenga nyumba ya kuishi linaweza kuwa ni eneo lililopimwa ama bado halijapiwa. Ardhi yake ni ya mabonde na milima ama tambarare. Utaangalia matumizi mengine ya eneo hilo na miundombinu yake. Pengine ni eneo jirani na viwanda n.k. Hata udongo na hali ya hewa ya eneo husika inanafasi yake, pengine ni ufukweni mwa bahari.

Kumbuka, uamuzi wa eneo la kujenga unaweza kuashiria uharaka wa kukamilisha kujenga nyumba yako kwasababu kwa mfano kama unatazamia kujenga katika eneo la katikati ya mji huwa ni gharama kubwa na hata upatikanaji wake ni wa taabu kidogo. Ikiwa ni eneo la mjini kuna ugumu wake pia kwa mfano kupata kibali cha kujenga.Miji mingine kwa mfano Jiji letu la Arusha halitoi vibali kwa ujenzi wa nyumba ndogo zisizo za ghorofa kwa maeneo ya katikati ya Jiji.


Kwa eneo ambalo limekwishajengwa na kupangwa kuwa eneo la makazi huwa ni rahisi zaidi hata kupata kibali cha ujenzi wa makazi na miundombinu yake huwa maalumu kwa makazi ya watu.


Jambo la pili kujiandaa nalo ni pesa za kugharamia ujenzi husika hata kwa kuanzia tu na wataalamu utakaowatumia bila kusahahu gharama za mamlaka ya mji au mtaa husika na tozo za vibali mbalimbali vya huduma na ruhusa. Ni vizuri kupanga kiasi cha fedha ulichonacho au kujikusanyia kitakufikisha wapi katika ujenzi wako. Itakuwa gharama zaidi kama utaamua kupata eneo na kujenga hapo hao, ingawa kwa baadhi wanaweza.

Hata hivyo, kutokuwa na pesa ya kuanza ujenzi hadi kumaliza hakuwezi kuwa kizuizi cha kutojenga nyumba iliyobora. Kamwe usikate tamaa ama kuamua kujenga tu alimradi umejenga kitu ambacho hakina ubora na hakikidhi mahitaji kitaalamu. Kuna taasisi nyingi za mikopo (loans and mortgages) zinaweza kukusaidia. 

Lakini pia kwa kujikusanyia pesa kidogokidogo na kuzitunza kwa malengo ya ujenzi unaweza kufanya ujenzi wako ulio katika ubora mzuri. Kuna wataalamu washauri wa maswala ya gharama za ujenzi kabla, baada na wakati wa ujenzi wanaweza kusaidia. Kitaalamu wanaitwa  Quantity Surveyors ama Cost Engineers kwa baadhi ya nchi kama Uingereza.

Hatua ya ya tatu, baada ya kuwa umejiandaa kifedha na maandalizi mengine kufanya ujenzi, fikiria sasa kumpata mtaalamu mbunifu wa majengo atakayekusaidia kuandaa mchoro wa nyumba yako. Hatua hii ni muhimu zaidi na ndipo watu wengi wanapokosea na kujikuta wakitumia gharama kubwa baadae kujenga nyumba ambayo haiwapi raha waliyoitamani kwa kuwazia ama kwa kuona mahali fulani ama kwenye mitandao ya internet. Shirikiana na mchoraji akuelekeze namna ambavyo mawazo yako ameyaweka kwenye mchoro kama unavyohitaji na kuhakiki ukubwa wa nyumba na mgawanyo wa vyumba.

roof structure - seriajr
Jengo kwa matumizi ya kuishi likiwa katika hatua za uezekaji
Kuna baadhi ya watu wanaweza kuona muonekano wa nyumba kwa nje wakavutiwa nao na kumuonesha fundi mjenzi na kumtaka awajengee wakiamini kwa muonekano wa nje watapata kuridhika hata na ndani. Bahati mbaya wanakuwa hawafahamu kuwa mgawanyo wa vyumba ndani, saizi yake na mpangilio wa mahusiano ya vyumba na maeneo tofauti ndio huleta mvuto, ubora na raha ya nyumba husika.

Kwa hiyo, kama nilivyoeleza kuwa ukishakuwa umejiandaa unamtafuta mtaalamu mbunifu wa majengo, kitaalamu anaitwa Architect (tutajifunza baadae nafasi yake katika ujenzi pamoja na wasaidizi wake). Unampatia mahitaji yako halisi na namna unavyotamani nyumba yako iwe, nae kwa utaalamu wake atakushauri namna nzuri ya kuyapanga mahitaji yako hayo na kuyaweka kwenye mchoro ambao fundi anaweza kuutumia kujenga nyumba yako.

Mtaalamu huyo atayaunganisha mahitaji yako na kuyapanga kitaalamu ili kuweza kupata jengo ambalo litakuwa na sifa za mahitaji ya nyumba bora. Mifano ya mahihaji muhimu ni madirisha yanayoruhusu hewa kwa kupangilia uhusiano mzuri na milango kupata kitu kinachoitwa kitaalamu kama cross ventilation. Pia mpangilio wa vyumba, sehemu ya chakula, jiko na vyoo bila kusahau baraza na korido.


Utoaji na uingizaji wa maji masafi na machafu una umuhimu wake pia na halikadhalika namna sebule itakavyokaa na kutumiwa na wageni na watu watakaokuwa wanaishi kwenye hiyo nyumba bila kusahau maliwato kwa mgeni. Pia maswala ya usalama wa jengo dhidi ya hatari ya moto na hata mpangilio wa madirisha kuoanish na uelekeo wa upepo.

Ni vizuri pia tukifahamishana kuwa kwa mujibu wa sheria zetu za ujenzi hapa nchini kuhusu nyumba za kuishi (residential houses), endapo mtu anajenga jengo la ghorofa analazimika kumtafuta injinia amsaidie kumuandalia mchoro utakaohusu uimara wa jeingo kwa maana kwamba utakuwa ni mchoro unaoonesha namna nondo zitakavyojipanga, idadi na saizi yake, bila kusahahu ubora wa zege na mambo mengine yahusuyo uimara wa jingo lako.

Sasa kama utakuwa unawazia jengo la namna hiyo ni lazima kisheria kutafuta Structural Engineer akusaidie kuandaa michoro mingine.


Hatua ya nne, baada ya kuwa na mchoro wako utahitaji kujua makisio ya gharama halisi za mradi ama kwa kujenga mpaka kumaliza ama kwa awamu tofauti. Mtaalamu mkadiriaji majenzi niliyemueleza hapo awali kuwa anatambulika kitaaluma kama Quantity Surveyor/Cost Engineer atahitajika kufanya hesabu za makadirio ya gharama ili uweze kujua namna halisi ya kujipanga kutegemeana na mchoro ulivyo na jinsi utakavyokuwa umechagua material gani za kutumia kwa kushauriana na kitaalamu. QS huyu atakusaidia kubajeti vizuri na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima au bidhaa bora na rahisi lakini lengo likibaki kupata nyumba bora. Wakati mwingine hata fundi mzoefu anaweza kukusaidia.

Hatua ya tano. Mpaka hapo utakuwa umeshakamilisha hatua za awali muhimu kabla ya kuanza mradi wako wa ujenzi. Sasa unaweza kuwatafuta wataalamu wajenzi kwa maana ya kampuni au mafundi binafsi wenye uelewa mzuri wa kutafsiri michoro ya ujenzi ili muweze kukubaliana na kuanza kazi ya ujenzi tukichukulia kuwa eneo tayari lipo, limehakikiwa na kuonekana liko tayari kwa ujenzi na udongo wake ukiwa umeshaoanishwa na aina ya msingi wa nyumba utakavyokuwa.

nembo ya AQRB
Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 ya AQRB, Bodi ya Wakadiria Majenzi na Wabunifu wa Majengo inahimiza matumizi ya kampuni za wakandarasi zilizosajiliwa kufanya ujenzi kwa kufuata mchanganuo ufuatao

· Ujenzi wa majengo yoyote ya ghorofa ya ukubwa na thamani yeyote
·  Majenzi yote ya makazi yanayozidi thamani ya sh milioni 50 na ujenzi wake unahitaji uhandisi (structural inputs)
· Ujenzi wa majengo yote ya umma kama shule, hospitali, masoko, makanisa, misikiti, kumbi za starehe n.k


·  Ujenzi wa majengo ya viwanda, maghala n.k

Kwa hiyo utaona ni namna gani sheria inajaribu kumsaidia mjenzi kupata kilicho bora kwa kutumia wataalamu. Ni ukweli kwamba idadi kubwa ya watanzania hawana uwezo wa kujenga kwa kutumia wataalamu na hata kiwango cha nyumba yenye thamani ya milioni 50 wakati wa kuanza ujenzi hawana. Baadhi wanazikwepa kampuni wakijaribu kuokoa gharama za ziada ili zitumike kwenye ujenzi wenyewe.
Sehemu ya kazi za kweka urembo wa nyumba kwa ndani. Kazi ya SeriaMjenzi
Hata hivyo, kutokuwa na uwezo wa kukodi ama kuajiri kampuni kufanya ujenzi wako sio kipingamizi cha kutowashirikisha wataalamu kama nilivyoeleza hapo awali. 

Unaweza kuepuka kutumia kampuni kujenga lakini kama uliwashirikisha wataalamu kuandaa wazo la ujenzi wako kitaalamu unaweza kumtumia fundi yeyote mjuzi akakusaidia kujenga kwa gharama ambazo mara nyingi ni pungufu kidogo ya gharama za makampuni. Mtaani tunao mafundi wengi na wataalamu baadhi wakiwa wamehudhuria mafunzo rasmi chuoni na wengine wakijifunzia tu mtaani na kujikusanyia uzoefu. Wote ni wataalamu. 


Itaendelea Sehemu ya nne, ambapo tutaweza kuwajua wataalamu mbalimbali wanaohusikana ujenzi.

Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com


TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI ? - PART II: DHANA YA MAKAZI BORA


Leo ikiwa ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hii tutaangalia kwa ukaribu zaidi dhana nzima ya nyumba bora ya binadamu ambapo madhumuni na miundo yake hutegemeana sana na hali halisi ya kidunia kwa utofauti wa sehemu moja na nyingine. Hii ni dhana tata kidogo.

Dhumuni kubwa la kuwa na nyumba ya kuishi ni kumpatia mwanadamu usiri wa mambo yake binafsi, na kumlinda dhidi ya madhara yatokananyo na hali ya hewa ya kidunia na viumbe wengine hatari kwa binadamu. Malengo mengine ni raha, ufariji na mahali pa kuendeleza uzao na kutunza afya ya mwanadamu. Nyumba ya kuishi inajitofautisha sana na mejengo mengine kama ya biashara, ofisi, masoko, hospitali, viwanda n.k. Tofauti hiyo hutegemeana sana na lengo la matumizi ya jengo husika kama nilivyoeleza hapo juu.



Ili jamii iweze kuwa na makazi bora inalazimu timu ya wataalamu mbalimbali washirikiane kwa ukaribu sana ili kufanikisha hilo. Makazi bora lazima yahusishe nyumba bora na miundombinu inayoizunguka. 

Watu wengi wanaamini kujenga nyumba ya kuishi ni jambo gumu sana katika maisha yetu na hivyo kuishia kujenga alimradi tu ni kijumba cha kujisitiri. Ni kweli ujenzi ni gharama, lakini ukiwa na mipango mizuri na malengo thabiti unaweza kufanikisha kuwa na nyumba yako iliyo bora kwa urahisi kabisa. Kila kinachopangwa kikapangika vizuri huleta matokeo mazuri. 

Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya mambo muhimu yanayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.


Itaendelea Sehemu ya 3.. 
Tembelea ukurasa huu tuelimike pamoja



Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WA NYUMBA ZETU!? - PART I

“Nyumba bora, salama na nafuu ni hitaji muhimu kwa kila familia. Bila kuwa na mahali pazuri pa kuishi, watu hawataweza kuwa sehemu ya jamii inayozalisha, watoto hawataweza kujifunza na familia hazitastawi” anaeleza   Bw Tracy Kaufman, Mtafiti wa makazi nafuu kutoka Marekani (http://www.habitat.org/how/poverty.html)


Historia ya binaamu inaelezea mabadiliko makubwa ya ukuaji katika awamu tofauti tofauti za maisha yake.  Kutoka kutembea kwa kuinama mpaka kutembea wima. Kutoka kwenye ugunduzi wa moto, zana za mawe, magome ya miti kujisitiri maungo mpaka ugunduzi wa viatu, nguo, umeme, kompyuta na njia nyingi za usafiri bila kusahau bidhaa mbalimbali za kurahisisha kazi na kujenga makazi bora yenye kila aina ya madoido. 

Binadamu wa awali kabisa wanaelezwa kuwa na utaalamu wao ambao kutokana na hali halisi ya wakati huo ni wa kiwango duni sana kama utalinganishwa kwa nyakati za sasa. Binadamu wa kale alianza kuishi kwenye mapango na mahema ya miti, akitumia nyasi na ngozi za wanyama. Nyumba hizi hazikuwa na milango wala madirisha. Baadae akajua namna ya kutengeneza nyumba za miti na udongo, na baade wakatengeneza tofali za udongo za  kuchoma kwa joto la jua.

Makazi ya kale kwa maana ya nyumba za kuishi binadamu yalihusisha matumizi ya vitu asili moja kwa moja katika ujenzi wake tofauti na sasa ambapo bidhaa ya asili inasanisiwa kupata bidhaa nyingine katika hali ya kuongeza ubora na umaridadi. Nyumba iliyokuwa maalumu kwa mifugo haikuwa tofauti sana na anayoishi binadamu na wakati mwingine ilikuwa inatengenezwa kuwezesha mifugo kama ng’ombe, kondoo na mbuzi kuishi mahali pamoja na binadamu. Wataalamu wa historia wanatueleza kuwa nyumba nyingi za kale zilijengwa kutegemeana na tamaduni na mila za jamii husika.

Kwa kadiri miaka inavyokwenda binadamu amezidi kuwa mgunduzi wa bidhaa na mbinu mbalimbali zitakazomuwezesha kukabiliana na mazingira yanayomzunguka. Ugunduzi huo unahusisha ujenzi wa nyumba bora na bidhaa zake zinazoikidhi mahitaji muhimu kumuwezesha binadamu kuishi mahali safi salama huku kukiwa na nyongeza ya urembo na umaridadi wa aina tofauti tofauti. 

Nikukaribishe katika mfululizo wa makala hii itakayohusu kuwajua wataalamu mbalimbali katika taaluma ya ujenzi, hususani ujenzi wa nyumba za kuishi binadamu sambamba na umuhimu wa mjenzi kuwashirikisha watalamu hao katika kila hatua ya ujenzi wake kwa minajili ya kupata nyumba iliyobora, nzuri, salama na yenyekukidhi mahitaji. 


Nakumbuka wakati fulani nikiwa mwanafunzi Chuo Kikuu (UCLAS) mwalimu wangu wa somo la Ujenzi alipata kuniambia tukiwa mapumziko ya chakula kuwa kila mtu ni mbumbumbu kwa jambo fulani bila kujali vyeti alivyonavyo; akimaanisha kuwa kama wewe ni mtaalamu katika taaluma fulani uliyosomea ama kujifunza lazima utakuwa mbumbumbu kwenye taaluma nyingine ambazo hujajifunza.


Akadai kuwa kadiri mtu anavyozidi kusoma jambo moja kwa undani zaidi ndivyo anavyozidi kuacha mambo mengine mengi na kubobea kwenye hilo moja pekee. Daktari aliyebobea kwenye upasuaji mkubwa kwa mfano, hawezi kuwa mjuzi kwa kiwango kile kile sawa na mtu mwingine anayeshugulika na maswala ya umeme kama taaluma yake. 

Binadamu wa sasa anajipenda mno na anatamani kufaidi maisha yake kwa kadiri awezavyo. Moja ya matamanio hayo ni makazi bora yatakayompendeza kutegemeana na uwezo wake kifedha na kiutaalamu kugharamia hilo. 

Lakini wapo watu wengi ambao wanatamani kuwa na makazi yanayokonga roho zao bila kujali kama wana uwezo mkubwa kifedha kugharamia umaridadi wanaoutaka ama la na wapo wengine ambao wao hujenga tu kwasababu inawalazimu wajisitiri ndani ya jengo wasidhurike na mashambulizi ya wanyama wakali na ama hali ya hewa ya kidunia. 

Hawa wanaojenga tu alimradi ni jengo la wao kuishi husababishwa kuamua hivyo ama kwa kutokujua wapi na ni nani wamuone kwa ushauri na pia uwezo mdogo kiuchumi. Baadhi pia hujenga kwa mazoea na hata mafundi wanaowatumia sehemu kubwa wanatumia uzoefu pekee.


Nyumba iliyojengwa kwa gharama kubwa sio lazima iwe nyumba bora. Kwa tafsiri rahisi nyumba bora ni ile inayokidhi mahitaji muhimu ya binadamu kuishi ndani na kujisitiri kwa usalama bila kupata madhara. Hii ni pamoja na mazingira yaliyoizunguka nyumba hiyo. 

Tutaona baadae mahitaji hayo muhimu ni yapi. Kwasasa itoshe kufahamu kuwa gharama zilizotumika kujenga makazi yetu ya uswahilini zinatosha kabisa kujenga makazi bora zaidi kwa kuhusisha wataalamu na kuacha kujenga kwa mazoea, sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo kiuchumi na kuogopa kuwashirikisha wataalamu kwa kuhofia gharama.



Itaendelea Sehemu ya pili kuelezea Dhana ya Makazi Bora
Tembelea blogu hii tuelimike pamoja




Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080seria.tw@gmail.com

Thursday, December 21, 2017

Unafahamu nini kuhusu Window-Sill? Soma hapa

Window-sill ni kimkanda cha zege kwa unene wa mpaka kufikia mm 75 kinachoweka chini ya dirisha kwa ajili ya kuongeza urembo (muonekano mzuri wa dirisha na kusaidia kuelekeza maji  ili yasiingiendani au kubaki kwenye dirisha kwa kutiririka yenyewe kufuata ulalo unaokuwepo kama picha zetu zinavyoonesha.

Unaweza kuzijengea hapo hapo dirishani kwa kusuka box lake, kweka nondo au wiremesh; au kununua ambazo zimeshatengenezwa tayari na kuzipachika eneo husika au unaweza pia zitengeneza pembenni wewe mwenyewe na kuzipachika dirishani na kisha kufanyia finishinh inayofaa.

Ili kufanya kazi ya kuondosha maji (to drain water) kwa usahihi bila kuchafua ukuta, huwa kuna kimfereji (throat) kinawekwa kwa chini ili maji yakiwa yanatiririka yasiweze kugeuka na kuukuta ukuta.

Maji tunayoyazungumzia hapa ni yale yanayoweza kufikia dirisha kutokana na aidha mvua ya upepo au wakati wa kusafidha madirisha.   





NOGESHA UREMBO WA NYUMBA KWA KUWEKA 'PLANTER' ZA MAUA


Baadhi ya watu hujenga nyumba zao kwa kutilia mkazo urembo wa ndani pekee. Hata wakati wa kununua kiwanja husahau kufikiria na mahitaji ya nyumba kwa nje na kujikuta wananunua maeneo ambayo hayatoshelezi kujenga nyumba na kuacha eneo la wazi kwa maana ya bustani za kupumzikia, maeneo ya kuanikia nguo, kuegesha magari na hata kutengeneza urembo mwingine wa kuzunguka jengo.

Picha hii zinaonesha baadhi ya urembo wa mawe kuzunguka nyumba ukipambwa kwa maua. Hizi tunaita "planter boxes" au hata "flower boxes".  Ni nzuri zaidi kwa nyumba ambayo imejengwa kwa kuwa na msingi mrefu kutokea kwenye udongo. Unaweza kuotesha maua peke yake au kuchanganya na nyasi/ukoka kutegemeana na ubunifu wako. Zaidi kwenye muonekano wa mbele ya nyumba unapoingilia.

Picha zingine zinaonesha uendelezaji wa bustani za maua na ukoka kupamba eneo la makazi. Unaweza kuiga vitu vizuri kama hivi na ukaboresha nyumbani kwako.






Tangastone Surfacing with regular pattern!




Regular pattern Tangastone surfacing to floor, externally! For your driving areas, parking etc.
TUNAO MAFUNDI WAZURI SANA KUKUSAIDIA KAZI YAKO. WASILIANA NASI UPATE KILICHO BORA +255713705462









Friday, January 20, 2017

MWONGOZO WA KUCHAGUA RAMANI BORA YA NYUMBA

Ramani ya nyumba-Mali ya P.Joseph

Bila shaka kila mmoja wetu anatamani kumiliki nyumba yake,na bila shaka wale ambao wamekwisha jenga wana ndoto za kujenga tena ama kuwashauri ndugu na marafiki kujenga.

Ujenzi katika sehemu kubwa ya Tanzania haufuati taratibu na sheria za ujenzi wa makazi.Zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha hili lakini kwa leo mjadala utajikita katika namna ya kuchagua ramani bora ya nyumba

Ramani ya nyumba ni dira ambayo ni kazi ya usanifu yenye kuleta picha ya uhalisia utakaofikiwa na kutarajiwa na mteja.Kazi hii hufanywa na msanifu majengo amnbaye kwa lugha ya kiingereza huitwa Architect.

Msanifu husikiliza kwa makini matarajio ya mteja na kuiweka picha ya matarajio katika mchoro (picha).Watu wengi hudhani kazi ya Architect ni kuchora tu ramani,na ndio maana wengi hudhani ni jambo rahisi.Ukweli ni kwamba kazi yake ni kusanifu mawazo ya mteja na kuyaweka kuwa halisi.Kwa maana hiyo,hii ni fani ambayo huitaji umakini na elimu ya kutosha ili kuhakikisha anasanifu jengo ambalo litafanya wanaoishi waishi wakiupata msawazo katika joto,hewa,mwanga na wawe na furaha na kupapenda wanapoishi.

Baada bya maelezo hayo sasa tujiulize je,ramani bora inazingatia mambo gani?Ijulikane kwamba nimejaribu kupitia vigezo vitakavyomfanya kila mtu aelewe

Kwa wale ambao wana mpango wa kujenga nyumba bora za kisasa,mambo
yafuatayo ni muhimu kuyazingatia unapochagua ramani bora kwa ajili ya
nyumba yako: 
Mchoro ukionesha uhusiano uliopo kati ya sehemu moja na nyingine katika eneo (site plan).Picha ni mali ya Nyumba BoraTz


1.Izingatie maono ya mteja (client)-client imaginationikiwa na maana,mteja anapaswa kupata kile anachokipenda na alichofikiri kichwani kwake eitha kwa kuona ama kwa kutarajia 

2.Iwe na uhusiano mzuri kati ya eneo na eneo (mfano sebule na dining,dining na
jiko, sebule na vyumba.

3. Izingatie matumizi bora ya ardhi kwani ardhini gharama ( iwe na mgawanyo bora kati ya eneo linalojengwa, eneo amanafasi ya kutembea (circulating space), eneo la kijana (green
zone)-ama eneo linalopandwa miti, maua na vingine vyenye kuleta uhai.Ni lazima iepuke uwepo wa sehemu zisizo na kazi (dead space)

4.Izingatie hewa na mwanga wa kutosha katika kila eneo linalotumika,nanyumba bora huzingatia hewa na mwanga wa asili na sio artificial air.(viyoyozi)

5.Izingatie uwepo wa sitiri (privacy) –ihakikishe kila mtumiajianakuwa na uhuru wa kutosha na kuepuka muingiliano

6. Izingatie kuliendeleza eneo, lisiwe mfu kwa maana ya kuliharibu ama kuondoa vitu
vya msingi ambavyo vinafanya ardhi iwe oevu/endelevu 

7. Iwe inazingatia kufikika na matumizi kwa watu wa umri wote na maumbile yote mfano wazee,walemavu. 

8. Uzingatie uzuri- iwe inavutia (appealing to eyes) na wakati Fulani mvuto wake uwe wa kipekee ama mfano mahali inapojengwapo, iwe kioo cha eneo,utamaduni na mazingira ya eneo.

9.Izingatie matumizi bora ya maji na nishati,ikihusianisha vema sehemu zinazohitaji matumizi ya maji (wet areas) na zisizohitaji maji |(dry areas), sehemu zenye kuhitaji nishati na kutoa nishati-hot areas na hivyo kurahisisha matumizi bora ya maji na nishati.Na katika zama hizi ambayo dunia inashuhudia uhaba wa maji na nishati katika nchi za Afrika,ni vizuri wasanifu majengo waanze kufikiria majengo ambayo ni rafiki katika matumizi na rafiki wa mazingira

10.Kwa nyumba ambazo ni za wakazi wengi,ni vema ikazingatia kukuza uhusiano na undugu mfano kuwe na kibaraza (verandah ya pamoja), sehemu za mapumziko za pamoja pia,ili kuhakikisha ujamaa na ushirikiano unadumishwa

 Kumbuka nyumba
utakayoijenga ni sehemu ya kudumu ( permanent structures) hivyo ni vizuri ukifahamu mapema mambo haya kabla ya kujenga kuepuka mkanganyiko wa kisaikolojia,maamuzi na uchumi. 
N:B- Nyakati hizi watu wanapenda nyumba ambazo zinaondoa kabisa uhusiano wa kijamii mfano
ukaribu na majirani,ushirikiano-nadhani ni wakati sasa wasanifu majengo Tanzania wafikirie ni jinsi gani kinachoitwa privacy kinavyoathiri ujamaa,enzi za nyerere fikra ilikuwa watu wanaotumia apartment wapike pamoja,wafue sehemu moja,lakini kwa sasa watanzania
wanafiki tofauti na labda kwa sababu hatuna falsafa inayoliunganisha taifa

CHANZO/HATIMILIKI YA STORI: UJENZIBORATZ

Kwa maswali na maoni Wasiliana nasi UJENZIBONGO ama wasiliana na UJENZIBORATZ kupitia anwani pepe nyumbaboratz@gmail.com