Header Ads

Header Ads

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KATIKA UJENZI WETU? - PART V: FAHAMU HASARA ZINAZOKUKABILI

KARIBU KATIKA SEMEHU YA MWISHO YA MAKALA YETU INAYOHOJI “TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?”. 

Sehemu iliyopita tuliweza kuwafahamu baadhi ya wataalamu muhimu katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, halikadhalika miradi mingine kama ujenzi wa barabara, madaraja na mabwawa ya maji.


Katika kuhitimisha makala yetu hii, leo tutahitimisha kwa kauangalia baadhi ya faida tunazozikosa kwa kutowashirikisha wataalamu katika kufanya miradi yetu ya ujenzi, hasa kwa nyumba zetu za makazi.

Kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, nchi yetu pia imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa nyumba na makazi bora ya watu kuishi. Watu wengi wamejikuta wakijenga kiholela kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na mamlaka za miji kutowajibika ipasavyo kusaidia jamii kuwa na makazi bora na yanayokidhi mahitaji ya sasa na baadae.


Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi. Wataalamu wanaposhirikishwa Serikali yetu inakuwa na uhakika kuwa mipango, sheria, kanuni za ujenzi, na viwango vya ujenzi vinazingatiwa ili kuiwesesha kupanga mipango ya kuhudumia jamii yote kwa mahitaji kama miundombinu ya umeme, kukabili majanga ya moto, maji safi na maji taka.

Kama tulivyofahamu awali, Ujenzi ni teknolojia ya kujenga nyumba, viwanda, barabara, daraja au hata miji. Ni kazi inayohusisha wataalamu wengi na ngazi mbalimbali ya kupanga na kutekeleza. Majengo madogo yanajengwa na watu binfasi kufuatana na maarifa yao bila kuhitaji mpangilio mkubwa kwa kutumia mafundi wenye ujuzi kiasi kutoka vyuo vya ufundi au waliojifunza kupitia maarifa ya watu waliowatangulia. Mamlaka ya Mji husika hulazimika kushirikishwa ili kuruhusu mpangilio unaoruhusiwa kisheria.
Miradi mikubwa ya ujenzi huhitaji mpangilio maalumu na ni lazima kwa mwenye jengo kutafuta kwanza ushauri wa wataalamu, ambao watasimamia kazi yake kuanzia mwanzo wa ubunifu mpaka kukamilika kwa ujenzi.

Mhadisi na msanifu majengo watachora michoro ya jengo. Wataalamu wakadiriaji gharama watakadiria mahitaji ya vifaa na gharama za jengo, usimamizi na malipo mengine ya vibali. Watatafutwa wakandarasi ambao watakaa na kupanga mahitaji ya muda, pesa, wafanyakazi na mashine zitakazotumika.
Kisha ujenzi utasimamiwa na mhandisi na msanifu wa jengo pamoja na wataalamu wengine ambao wamesajiliwa na kupewa vibali vya kufanya kazi hiyo na mamlaka husika. Mamlaka ya mji husika nayo itahusika na watu wake wa ardhi na mipango miji. 

Yote yakizingatiwa na kutekelezwa kwa usahihi na uaminifu hitimisho ni kupata jengo zuri na lenye thamani kulingana na gharama zilizotumika, ambayo ni faida kwa mmiliki wa jengo. 

Kwahiyo, ukiachana na utambulisho huo mpana kuhusu majengo makubwa tufikirie sasa kwa udogo wa majenzi yetu ya makazi ya kuishi kwa kuzingatia sharia na taratibu za miji mbalimbali. Ingawa kwa sehemu kubwa nchi yetu ina shida ya maeneo kutopimwa na kutambulika matumizi halali ya ardhi, lakini bado kuna changamoto ya watu wengi kupuuza taratibu zilizopo kwa sababu za kawaida sana.

Kujenga nyumba kunahitaji umakini mkubwa sana na wakati mwingine mwenye kujenga anahitajika kuwepo eneo la ujenzi mara kwa mara na ikibidi kushiriki katika hatua zote za kuanza wazo la ujenzi mpaka kukamilika kwa nyumba yake. Ukaribu huu unakusaidia kupata nyumba na makazi ya ndoto yako.

Kwa kuangalia msingi kwamba atakayeitumia ni wewe na familia yako, ni wazi kuwa unahitaji kuhakikisha unapata makazi yaliyo bora na yatakayodumu kwa muda mrefu. Pengine, yawezekana ukawa huna kabisa ufahamu wowote kuhusu namna ya kufanya ujenzi wako na kuwa vile unavyotamani. Pengo hilo linazibwa na wataalamu wa ujenzi kama ukiamua kuwashirikisha. Hawa watakusaidia kufanya ndoto yako kuwa kweli na kukuongoza kupata bidhaa za gharama nafuu na bora. 


Mtaani kuna mafundi wengi wazuri na wazoefu lakini wana dosari ya kujenga kwa mazoea pekee na kukariri kazi nyingine zilizopita na ndio maana ni rahisi kukuta mitindo ya nyumba iliyojengwa na fundi mmoja ikifanana kwa mambo mengi. Hali itakuwa tofauti kama mafundi hawa watashirikisha ujuzi wao na utaalamu mwingine ili kuweza kufanikisha kile anachohitaji mwenye kutaka nyumba.

Katika kunogesha mada yetu hii, nadhani ni vyema pia tukafahamishana na kujikumbusha baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kujenga nyumba yako kwa upya kabisa, na hasa ikiwa ndio mara yako ya kwanza kufanya ujenzi:


1.    Kuwa na dondoo kadhaa kuhusu gharama za ujenzi
Kabla ya kuanza ujenzi, fanya tathmini binafsi ili uweze kujua kama unaweza kumudu gaharama ya nyumba unayotaka kwa ukubwa gani kwa muda kiasi gani. Mambo mengine ni malighafi utakazotumia na zitapatikana wapi nan i wapi utajenga. Mambo yote haya ukiyatathmini kwa usahihi y1akupa muelekeo wa gharama na jinsi utakavyofanikisha ujenzi wako.

2.    Fahamu aina ya mafundi na wataalamu utakaowahitaji kukujengea
Ni muhimu pia kuwajua mafundi wazuri na unafuu wao wa gharama sambamba na wataalamu washauri na wachora ramani watakaokusaidia hasa kwa miradi mikubwa. Endapo utataka kuuza kazi zote kwa mtu mmoja ni muhimu pia kuwafahmu uwezo wake, gharama, ubora wa kazi afanyazo na uaminifu wake kwenye kazi na usimamizi wa fedha.

3.    Fahamu kuhusu taratibu za kisheria zinazosimamia maswala ya ujenzi katika eneo la Mji unaoishi
Kila mamlaka ya Mji inataratibu zake za upangaji mandhari ya mji wake kwa makazi na matumizi ya umma, viwanda n.k. Ni muhimu kufahamu mamalaka ya eneo husika imepanga matumizi gani kwenye eneo unalotaka kujenga. Idara ya ardhi itathibitisha umiliki wa eneo na uhalali wa matumizi tarajiwa na idara ya ujenzi watakagua michoro kama inakindhi viwango vya ubora na miundombinu ya maji taka na kutoa Kibali cha Ujenzi. Kwa tatizo la kuwa na maeneo mengi yasiyopimwa, Mabaraza ya Ardhi ya Kata husaidia kutoa uthibitisho wa matumizi ya eneo husika kama halijapimwa. Fuata masharti ya ujenzi kuepuka usumbufu usio na sababu.

4.    Fikiria mahitaji halisi na muundo wa nyumba unayoitaka
Kama ni nyumba ya familia au biashara, ni wewe ndiye unayejua mahitaji halisi kwa maana ya idadi ya vyumba, matumizi yake na pengine muonekano unaoutamani. Mbunifu majengo anaweza kukuongoza kupata mchoro mzuri kwa viwango vya nafasi kitaalamu ili kusitokee nyumba ikajenga halafu ikaonekana chumba Fulani ni kikubwa sana au kimepungua. Kwa hiyo katika hatua hii unafanya kama vile ndio uko ndani ya nyumba na unaigiza akilini kama ndio unaona maisha halisi ndani ya nyumba, unaona swichi za umeme na taa zilipo na kukuhudumia vizuri.

5.    Fikiria mandhari ya nje ya nyumba
Watu wengi hasa wanaokopi ramani tu na kujenga wanakosa umaridadi wa mandhari ya nje. Ni vyema sana ukajenga kufuatana na muundo wa kiwanja chako. Kwa hiyo, utaona umuhimu wa kupata mtaalamu akakutengenezea ramani itakayoendana na eneo lako. Kuna mambo ya kuzingatia kama sehemu ya kuegesha gari, kuanikia nguo na shughuli za uwani, mahali pa kupumzikia na watoto kucheza, na namna ya kuingia nyumbani kwako bila kusahau sehemu sahihi ya kuweka mifumo ya maji taka kwa urahisi wa gari la maji taka kufika hasa kama hakuna mfumo wa majai taka wa umma kuweza kuunganisha.
Mandhari ya nje inahusisha ukijani wa miti na maua. Ni muhimu pia kuwazia mambo kama hayo pia.

6.    Fikiria maisha marefu ya jengo lako
Yawezekana unapanga kujenga nyumba yako eneo fulani ukitaraji litakuwa makazi yako ya kudumu. Lakini, uhalisia ni kuwa maisha nayo hubadilika kadiri majukumu ya kiuchumi yanavyobadilika. Ni nyema ukafikiria kuwa na jengo lisilohitaji ukarabati mkubwa kisi cha kuongeza gharama za maboresho huko baadae endapo itatokeo ukalazimika kufanya biashara. Aina ya malighafi utakayotumia pia ina nafasi kubwa kwenye gharama za ukarabati muda baada ya muda.

7.    Fanya uchaguzi mzuri wa finishing materials na decorations

Ni kawaida kukuta nyumba imebuniwa vizuri lakini finishing touch yake na rangi vinafanya iwe ya muonekano usiopendeza. Tumia muda mwingi kupeleleza huku ukishauriana na wataalamu na kusoma majarida mbalimbali ili uweze kupata chaguo sahihi la rangi na malighafi nyingine za kumba nyumba yako kwa ndani na nje. Kuna rangi maalumu kwa ndani pekee na nyingine kwa nje pekee. Halikadhalika madhari ya majirani zako na ukijani uliokuzunguka navyo vinaathiri aina ya urembo wa nyumba. Muhimu kushirikisha wataalamu wa kazi husika kukusaidia mawazo na ushauri.




Kwa hiyo, usiposhirikisha wataalamu katika ujenzi wako unakosa faida zifuatazo:

1.       Kupata aina ya nyumba inayojitosheleza kuendana na matamanio yako. Katika ubunifu kuna mambo usiyoyajua ambayo wataalamu watakusaidia kuyafahamu, matahali uhusiano wa uelekeo wa upepo na milango/madirisha (cross ventilation) n.k. Ukimshirikisha mbunifu akayaweka mawazo yako katika mchoro, atakusaidia kupata picha halisi ya jinsi nyumba yako itakavyokuwa nah ii itakuongezea hamasa ya kukamilisha ndoto yako.



2.       Kujenga kwa ramani/michoro ya nyumba. Michoro hii itakusaidia kwa masuala mengine kama bima, kupata mkopo, kuuza n.k. Itakusaidia pia kama utahitaji kufanya maboresho ya nyumba yako na kuwa rahisi kwa fundi mwingine kujua eneo Fulani kuna nini katika nyumba.

3. Kushirikisha wataalamu kutakusaidia kujua makadirio ya gharama za ujenzi wako. Makadirio haya hayatawezekana kukupa uhalisia kama hutakuwa na michoro yenye vipimo na mapendekezo ya finishing, milango, madirisha, na aina ya uezekaji wa paa. Michoro hii utaipata kwa mbunifu wa majengo endapo utamshirikisha. Ukishakuwa na michoro ya jengo lako, unaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujua ujenge namna gani kwa awamu hasa kama huna nguvu ya kujenga nyumba nzima kwa wakati mmoja. Bila michoro utajikuta unajenga na kuongeza vyumba kwa mpangilio usioshabihiana.

4.       Kushirikisha wataalamu kutakuepusha kujikuta unaingia kwenye hasara ama ya kubomolewa nyumba au kulipishwa faini zisizo za lazima kwa ama kupuuza au kutojua na kufuata utaratibu fulani.  Wakati mwingine ukipata mtaalamu mwaminifu atakusaidia kutotapeliwa na maofisa wasio waaminifu.

5.       Nafasi ya kushauriana na mtaalamu mchoraji namna ya kuongeza au kupunguza ukubwa wa jengo lako wakati ujenzi ukiendelea kwa msingi kwamba wakati wowote mawazo yanaweza kubadilika na kutamani eneo Fulani likae tofauti na lilivyobuniwa awali.

6.       Kama unataka kujenga kwenye eneo ambalo halijapimwa, mtaalamu atakusaidia kupata michoro ya jengo ambayo hata wakati wa ukaguzi wa baadae bado jengo lako litapimwa na kuonekana liko kwenye viwango na kuwa na thamani nzuri.

7.       Kushirikisha wataalamu waaminifu kutakusaidia kuepukana na wachakachuaji wakitumia kigezo cha wewe kutokuwa na ufahamu na mambo ya ujenzi. Kuna baadhi ya wajenzi si waaminifu na wanaweza kukupa hesabu kubwa za vifaa kinyume na uhalisia kwa lengo la kupata faida zaidi.
8.       Kupata kilicho bora na kwa thamani halisi ya fedha zako.

9.       Wataalamu watakusaidia kupata mbadala wa malighafi ya kutumia katika ujenzi wako huku ubora na uzuri wa kazi ukiwa vile vile kama unavyotamani. Hii ni pamoja na ushauri kuhusu malighafi zinazoweza kukuongezea gharama za ukarabati wa nyumba yako mara kwa mara.

10      Wataalamu watakusaidia kujua ukubwa wa chumba kwa matumizi tofauti kuendana na ukuaji wa teknolojia. Mathalani size ya madirisha, milango, vitasa na hata ukubwa wa maeneo kama choo na bafu ili kutosheleza vifaa utakavyonunua kwa ajili ya matumizi yako. Hata namna ya kupanga sebule kisasa kwa uwiano mzuri na sebule, jiko na veranda ni mambo ambayo utayapata kwa ushauriano mzuri na mtaalamu wa ujenzi.

11      Kuepuka hasara ya kujenga nyumba kubwa isiyosadifu mahitaji halisi kwa mhusika kutofahamu namna ya kujenga kulingana na mahitaji ya wakati gani.

Nyumba iliyojengwa kwa kubuniwa vizuri huleta raha kuishi ndani yake maana inakuwa na mpangilio unaotoa uhuru kwa kila memba wa familia kufurahia eneo lake na kuweka usiri wa mambo ya familia na wageni. Unaweza kujiuliza, kuna sababu yeyote ya msingi kwa mtu anayejenga nyumba ya milioni 65 lakini anakwepa kupata michoro kwa gharama ya shilingi laki tano tu au hata pungufu?

Kumbuka, katika ujenzi wa nyumba, kosa likishafanyika awali na nyumba kukamilika ni gharama sana kurekebisha. 


Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Blogger (http//:arusha255.blogspot.com na http//:ujenzidirect.blogspot.com)
Project QS, Proposed PPF Plaza Corridor Area Arusha
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com

No comments: