Header Ads

Header Ads

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WA NYUMBA ZETU!? - PART I

“Nyumba bora, salama na nafuu ni hitaji muhimu kwa kila familia. Bila kuwa na mahali pazuri pa kuishi, watu hawataweza kuwa sehemu ya jamii inayozalisha, watoto hawataweza kujifunza na familia hazitastawi” anaeleza   Bw Tracy Kaufman, Mtafiti wa makazi nafuu kutoka Marekani (http://www.habitat.org/how/poverty.html)


Historia ya binaamu inaelezea mabadiliko makubwa ya ukuaji katika awamu tofauti tofauti za maisha yake.  Kutoka kutembea kwa kuinama mpaka kutembea wima. Kutoka kwenye ugunduzi wa moto, zana za mawe, magome ya miti kujisitiri maungo mpaka ugunduzi wa viatu, nguo, umeme, kompyuta na njia nyingi za usafiri bila kusahau bidhaa mbalimbali za kurahisisha kazi na kujenga makazi bora yenye kila aina ya madoido. 

Binadamu wa awali kabisa wanaelezwa kuwa na utaalamu wao ambao kutokana na hali halisi ya wakati huo ni wa kiwango duni sana kama utalinganishwa kwa nyakati za sasa. Binadamu wa kale alianza kuishi kwenye mapango na mahema ya miti, akitumia nyasi na ngozi za wanyama. Nyumba hizi hazikuwa na milango wala madirisha. Baadae akajua namna ya kutengeneza nyumba za miti na udongo, na baade wakatengeneza tofali za udongo za  kuchoma kwa joto la jua.

Makazi ya kale kwa maana ya nyumba za kuishi binadamu yalihusisha matumizi ya vitu asili moja kwa moja katika ujenzi wake tofauti na sasa ambapo bidhaa ya asili inasanisiwa kupata bidhaa nyingine katika hali ya kuongeza ubora na umaridadi. Nyumba iliyokuwa maalumu kwa mifugo haikuwa tofauti sana na anayoishi binadamu na wakati mwingine ilikuwa inatengenezwa kuwezesha mifugo kama ng’ombe, kondoo na mbuzi kuishi mahali pamoja na binadamu. Wataalamu wa historia wanatueleza kuwa nyumba nyingi za kale zilijengwa kutegemeana na tamaduni na mila za jamii husika.

Kwa kadiri miaka inavyokwenda binadamu amezidi kuwa mgunduzi wa bidhaa na mbinu mbalimbali zitakazomuwezesha kukabiliana na mazingira yanayomzunguka. Ugunduzi huo unahusisha ujenzi wa nyumba bora na bidhaa zake zinazoikidhi mahitaji muhimu kumuwezesha binadamu kuishi mahali safi salama huku kukiwa na nyongeza ya urembo na umaridadi wa aina tofauti tofauti. 

Nikukaribishe katika mfululizo wa makala hii itakayohusu kuwajua wataalamu mbalimbali katika taaluma ya ujenzi, hususani ujenzi wa nyumba za kuishi binadamu sambamba na umuhimu wa mjenzi kuwashirikisha watalamu hao katika kila hatua ya ujenzi wake kwa minajili ya kupata nyumba iliyobora, nzuri, salama na yenyekukidhi mahitaji. 


Nakumbuka wakati fulani nikiwa mwanafunzi Chuo Kikuu (UCLAS) mwalimu wangu wa somo la Ujenzi alipata kuniambia tukiwa mapumziko ya chakula kuwa kila mtu ni mbumbumbu kwa jambo fulani bila kujali vyeti alivyonavyo; akimaanisha kuwa kama wewe ni mtaalamu katika taaluma fulani uliyosomea ama kujifunza lazima utakuwa mbumbumbu kwenye taaluma nyingine ambazo hujajifunza.


Akadai kuwa kadiri mtu anavyozidi kusoma jambo moja kwa undani zaidi ndivyo anavyozidi kuacha mambo mengine mengi na kubobea kwenye hilo moja pekee. Daktari aliyebobea kwenye upasuaji mkubwa kwa mfano, hawezi kuwa mjuzi kwa kiwango kile kile sawa na mtu mwingine anayeshugulika na maswala ya umeme kama taaluma yake. 

Binadamu wa sasa anajipenda mno na anatamani kufaidi maisha yake kwa kadiri awezavyo. Moja ya matamanio hayo ni makazi bora yatakayompendeza kutegemeana na uwezo wake kifedha na kiutaalamu kugharamia hilo. 

Lakini wapo watu wengi ambao wanatamani kuwa na makazi yanayokonga roho zao bila kujali kama wana uwezo mkubwa kifedha kugharamia umaridadi wanaoutaka ama la na wapo wengine ambao wao hujenga tu kwasababu inawalazimu wajisitiri ndani ya jengo wasidhurike na mashambulizi ya wanyama wakali na ama hali ya hewa ya kidunia. 

Hawa wanaojenga tu alimradi ni jengo la wao kuishi husababishwa kuamua hivyo ama kwa kutokujua wapi na ni nani wamuone kwa ushauri na pia uwezo mdogo kiuchumi. Baadhi pia hujenga kwa mazoea na hata mafundi wanaowatumia sehemu kubwa wanatumia uzoefu pekee.


Nyumba iliyojengwa kwa gharama kubwa sio lazima iwe nyumba bora. Kwa tafsiri rahisi nyumba bora ni ile inayokidhi mahitaji muhimu ya binadamu kuishi ndani na kujisitiri kwa usalama bila kupata madhara. Hii ni pamoja na mazingira yaliyoizunguka nyumba hiyo. 

Tutaona baadae mahitaji hayo muhimu ni yapi. Kwasasa itoshe kufahamu kuwa gharama zilizotumika kujenga makazi yetu ya uswahilini zinatosha kabisa kujenga makazi bora zaidi kwa kuhusisha wataalamu na kuacha kujenga kwa mazoea, sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo kiuchumi na kuogopa kuwashirikisha wataalamu kwa kuhofia gharama.



Itaendelea Sehemu ya pili kuelezea Dhana ya Makazi Bora
Tembelea blogu hii tuelimike pamoja




Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080seria.tw@gmail.com

No comments: