• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Showing posts with label Fundi. Show all posts
Showing posts with label Fundi. Show all posts

Thursday, February 22, 2018

Unahifadhi vipi saruji yako?


Simenti au saruji inahitajika kuhifadhiwa mahali palipo pakavu, pasiporuhusu unyevunyevu kupita kadiri iwezekanavyo. Na inashauriwa kama zimewekwa ndani ya nyumba basi mifuko yake ipangwe juu ya kichanja cha mbao na isigusane na ukuta kukwepa ubaridi wa sakafu na ukuta. Kukia na madirisha ya wastani itapendeza zaidi!

Si vyema sana kupanga mstari mmoja zaidi ya mifuko 10 mmoja juu ya mwingine. Zipange katika mtindo kwamba iliyotangulia kuhifadhiwa ndio itakayotumika kwanza kwa sababu ni rahisi sana saruji kuanza kuganda ikipata unyevunyevu. Kumbuka moja ya kipimo cha kujua ubora wa simenti ni ulaini vidoleni na kukosekana mabonge bonge yaliyoganda. 


Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N? Soma hapa kujua ubora tofauti wa simenti




Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu. 

Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi. Kwa baadhi ya nchi wana simenti ya uimara wa juu zaidi ya kipimo cha 52.5.

Kwa ujumla simenti hutumika kwa kutengenezea matofali, kuteneneza plaster na chipping, kusakafia, kuziba cracks, kuunganishia matofali kutengeneza ukuta, kutengenezea zege nk. 

Si ajabu ukaenda dukani na kunua saruji ya OPC ikiwa na mifuko yenye maandishi ya ubora kama 32.5N, 32.5R, 42.5N, 42.5R au hata 52.5N. Hizi herufi ‘N’ au ‘R’ hazina maana yeyote zaidi ya kuelezea kipindi cha mapema zaidi (umri) kwa simenti kuanza kufikia ubora wake ukipimwa katika siku 2 au 7.

Ni bahati nzuri Tanzania sasa ina viwanda vingi vya kuzalisha portland cement ambavyo hutambulika kwa majina kama Twiga Cement, Simba Cement, Tembo Cement, Moshi Cement, Dangote Cement n.k. WIngi huu wa wazalishaji huleta nafuu kwa walaji kupitia ushindani wa soko kibiashara.  

Tabia moja ya zege (mchanganyiko wa kokoto, mchanga na simenti katika uwioano uliopimwa na kuchanganywa na maji) huendelee kuwa bora kadiri siku zinavyoongezeka. Katika upimaji product ya zege, ubora hupimwa baada ya siku saba kuona kama kuna uwezekanao wa kufikia ubora unaotarajiwa huko baadae. Kipimo cha siku saba kikionesha kutoatoa majibu ya mwelekeo mzuri basi zege husika inabomolewa. Halafu kuna kipimo baada ya umri wa siku 14 na baadae siku 28 kuhitimisha kwamba viwango vya ubora vitafikiwa kadiri umri wa zege unavyoongezeka.  

Karibu tena Tujifunze!

Friday, December 22, 2017

Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu? Soma Hapa.

Mfano wa jengo la ghorofa moja katika hatua za ubunifu. Ukiwa na mahitaji ya kufanya ubunifu wa jengo lako, wasiliana nasi tutakusaidia. 
Mara nyingi tunajenga nyumba zetu za kuishi au kwa shughuli za kiofisi/biashara kwa kutumia malighafi ya tofali. Vipande vya mawe, tofali nk huungwa moja moja juu ya jingine kwa mpishano maalumu kwa kutumia mota ya simenti na mchanga na hatimaye kupata kitu kinachoitwa ukuta wa nyumba. Aghalabu malighafi na aina ya tofali ikawa tofauti kutegemeana na sababu mbalimbali.

Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jingo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi au tuseme kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

Ukuta tunaouzungumzia hapa ni ule unaoitwa kitaalamu kama ‘masonry wall’ au ukuta wa tope ambao ni matokeo ya utaalamu wa ufundi uashi. Fundi huyu hutumia mota iliyotokana na mchanganyiko wa simenti (au chokaa, udongo nk), mchanga na maji kwa uwiano maalumu kutengeneza kiunganishi (bonding materials). Mchanganyiko huu ukiwa na utepetepe kiasi huunganisha kipande kimoja kimoja cha ama tofali, jiwe, marble, granite, vigae n.k. Tofali linaweza kuwa ama la kuchoma (brick) au yatokanayo na simenti na mchanga pekee au pamoja na kokoto (blocks). 

Yapo majengo yaliyojengwa kwa kuta za zege, mbao au malighafi nyingine. Hatutaweza kutazamia hayo. Tutajikita zaidi kuangazia masonry walls kama nilivyotambulisha awali.

Kwa sehemu kubwa ya ujenzi wetu, katika kujenga ukuta wa tope tunatumia simenti kama kemilikali unganishi muhimu zaidi. Simenti nayo ina ubora tofauti kutegemeana na matumizi. Zipo simenti za aina nyingi kwa matumizi tofauti, tutakuja kuzifahamu wakati mwingine.
Jambo la msingi sana kufahamu, ukuta wa nyumba yako utakuwa imara na wa kudumu zaidi kutegemeana na mambo makubwa matatu
1.   Aina ya ukuta unaojenga, mtindo na muundo wake (ukuta wa mawe, tofali,
2.   Ubora wa malighafi uliyotumia kulingana na hali nyingine za mazingira
3.   Ufundi sahihi katika kujenga ukuta
Kulingana na aina ya malighafi inayotumika kujenga ukuta wa tope, inaweza kuwa ni mawe, tofali n.k tunaweza kupata ubora na uimara tofauti ambao utawezesha kuwako kwa aina mbili kuu za ukuta kutokana na nafasi yake kwenye jengo.
1.   Ukuta unaobeba uzito wa jengo (Load Bearing Masonry Walls)
2.   Ukuta usiobeba uzito wa jengo (Non Load Bearing Masonry Walls)
Aina ya kwanza ya Ukuta unaobeba uzito wa jengo, hujengwa kwa kutumia matofali ya kuchoma, mawe, au matofali ya zege/mchanga. Kazi ya ukuta wa aina hii mbali na kugawanya vyumba na kutoa usiri, hufanya kazi kubwa ya kuchukua na kusafirisha uzito wa paa ama jengo jingine la juu kama ni nyumba ya ghoroa na kuupeleka kwenye msingi wa jengo na hatimaye ardhini.
Mfundi ujenzi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa msingi wa nyumba, msingi wa tofali
Kuna unafuu wa gharama kama ukijenga ghorofa kwa kutumia ukuta wa aina hii badala ya nguzo na bimu za zege, hasa kwa jingo la ghorofa moja. Jambo muhimu ni ubora wa malighafi na unene wa ukuta, bila kusahau uwiano wa urefu na unene (slanderness ratio), na huku uimara wa msingi wa jengo katika dhibiti kucheza kwa ardhi kukiwa na umuhimu mkubwa. Kwa hiyo kuta hizi hufanya kazi ya kusafirisha uzito kama mbadala nguzo za zege na nondo. Unafuu unaweza usionekane pia kama eneo unalojenga litalazimu kuwa na msingi wa jamvi nene la zege (raft foundation)
Msingi wa nyumba ukiwa tayari kwa kujenga kuta za kugawanya vyumba. Msingi wa namna hii unauwezo wa kuhimili nguvu zinazoweza kusababisha nyufa. 
Hata hivyo, kuna hatari ya kutokea nyufa kwenye kuta za namna hii kutokana na kukosekana kwa fremu ya nondo na zege ambayo husaidia kukabiliana na nguvu mgandamizo (compression force) na nguvu za utengano (tension forces). Nyufa hizi huwa hatari zaidi kama zitashuka mpaka kuvuka msingi wa jengo.

Mashaka ya jengo kutohimili kutokea kwa nyufa ni hasa wakati wa kukabiliana na matukio kama tetemeko la ardhi, mvua kubwa na upepo mkali, na bila kusahau misukumo ardhini na kuyumba kwa utulivu wa msingi wa jengo (earth pressure & differential foundation settlement). Kufikiria hatari hizi, unalazimika kujihami kwa kushirikisha wataalamu ili kuondokana na mashaka  
Uzito (loads) tunaouzungumzia hapa ni mjumuisho wa uzito wa kuta zenyewe, watu na vilivyomo ndani ya jengo, paa la jengo na nguvu ya upepo (imposed & dead loads). Vipimo vya matofali kwa viwango vyetu ni mm 450x230x150 na mm 450x230x100 ambayo kwa lugha za mafundi huzungumzia inchi 9 (tofali la kulaza), 6, 5 na 4 (tofali la kusimama). Kama utatumia tofali kwa ajili ya ukuta unaobeba uzito, ni wazi kuwa utahitajika kujenga ukuta mnene (tofali za zege za kulaza) ambao utakuwa haupungui mm 225 (inchi 9). Kuta nyingine nyembamba unaweza kuzitumia kwa ajili ya kugawanya vyumba.
Hata hivyo, unene wa ukuta utaongezeka kutegemeana na matumizi ya jengo (occupancy) sambamba na idadi ya ghorofa juu ya “floor” ya chini inayogusana na ardhi.
Kwa ujenzi wa ghorofa, ni sahihi zaidi kujenga kuta za chini kwa mtindo wa mchanganyiko wa tofali pamoja na nguzo chache za zege na nondo zilizoungwa na bimu kuzunguka jengo zima, zikiunganishwa na slabu. Wahandisi wabunifu majengo (Structural/Civil Engineers) wanaweza kukusaidia kupata vipimo sahihi.
Ujenzi wa linta ambayo pia inatumika kuunganisha nyumba nzima kama ring beam. Ni aina ya ujenzi wa kawaida mitaani kwetu na matokeo huwa bora kama mafundi wataalamu watatumika. 
Aina ya pili, Ukuta usiobeba uzito wa jengo ni kuta ambazo kazi yake kubwa ni kugawa vyumba (partition walls) kwa ajili ya usiri na kulinda waliomo ndani dhidi ya hatari za nje. Katika jengo lenye kuta za namna hii kunakuwa na kuta nyingine ama nguzo ambazo ni maalumu kwa ajili ya kusafirisha uzito, mathalani maghorofa mengi tunayoyaona yakijengwa mijini. Kuta hizi hazilazimiki kuwa nene sana na ndio maana unaweza kujenga ukuta wa inchi 4 tu kwa ajili ya kugawanya maeneo ya choo na bafu. 
Mfano wa nyumba ya kuishi iliyokamilika . PICHA ZOTE NI HATI MILIKI YA BLOGU HII

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KATIKA UJENZI WETU? - PART V: FAHAMU HASARA ZINAZOKUKABILI

KARIBU KATIKA SEMEHU YA MWISHO YA MAKALA YETU INAYOHOJI “TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?”. 

Sehemu iliyopita tuliweza kuwafahamu baadhi ya wataalamu muhimu katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, halikadhalika miradi mingine kama ujenzi wa barabara, madaraja na mabwawa ya maji.


Katika kuhitimisha makala yetu hii, leo tutahitimisha kwa kauangalia baadhi ya faida tunazozikosa kwa kutowashirikisha wataalamu katika kufanya miradi yetu ya ujenzi, hasa kwa nyumba zetu za makazi.

Kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, nchi yetu pia imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa nyumba na makazi bora ya watu kuishi. Watu wengi wamejikuta wakijenga kiholela kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na mamlaka za miji kutowajibika ipasavyo kusaidia jamii kuwa na makazi bora na yanayokidhi mahitaji ya sasa na baadae.


Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi. Wataalamu wanaposhirikishwa Serikali yetu inakuwa na uhakika kuwa mipango, sheria, kanuni za ujenzi, na viwango vya ujenzi vinazingatiwa ili kuiwesesha kupanga mipango ya kuhudumia jamii yote kwa mahitaji kama miundombinu ya umeme, kukabili majanga ya moto, maji safi na maji taka.

Kama tulivyofahamu awali, Ujenzi ni teknolojia ya kujenga nyumba, viwanda, barabara, daraja au hata miji. Ni kazi inayohusisha wataalamu wengi na ngazi mbalimbali ya kupanga na kutekeleza. Majengo madogo yanajengwa na watu binfasi kufuatana na maarifa yao bila kuhitaji mpangilio mkubwa kwa kutumia mafundi wenye ujuzi kiasi kutoka vyuo vya ufundi au waliojifunza kupitia maarifa ya watu waliowatangulia. Mamlaka ya Mji husika hulazimika kushirikishwa ili kuruhusu mpangilio unaoruhusiwa kisheria.
Miradi mikubwa ya ujenzi huhitaji mpangilio maalumu na ni lazima kwa mwenye jengo kutafuta kwanza ushauri wa wataalamu, ambao watasimamia kazi yake kuanzia mwanzo wa ubunifu mpaka kukamilika kwa ujenzi.

Mhadisi na msanifu majengo watachora michoro ya jengo. Wataalamu wakadiriaji gharama watakadiria mahitaji ya vifaa na gharama za jengo, usimamizi na malipo mengine ya vibali. Watatafutwa wakandarasi ambao watakaa na kupanga mahitaji ya muda, pesa, wafanyakazi na mashine zitakazotumika.
Kisha ujenzi utasimamiwa na mhandisi na msanifu wa jengo pamoja na wataalamu wengine ambao wamesajiliwa na kupewa vibali vya kufanya kazi hiyo na mamlaka husika. Mamlaka ya mji husika nayo itahusika na watu wake wa ardhi na mipango miji. 

Yote yakizingatiwa na kutekelezwa kwa usahihi na uaminifu hitimisho ni kupata jengo zuri na lenye thamani kulingana na gharama zilizotumika, ambayo ni faida kwa mmiliki wa jengo. 

Kwahiyo, ukiachana na utambulisho huo mpana kuhusu majengo makubwa tufikirie sasa kwa udogo wa majenzi yetu ya makazi ya kuishi kwa kuzingatia sharia na taratibu za miji mbalimbali. Ingawa kwa sehemu kubwa nchi yetu ina shida ya maeneo kutopimwa na kutambulika matumizi halali ya ardhi, lakini bado kuna changamoto ya watu wengi kupuuza taratibu zilizopo kwa sababu za kawaida sana.

Kujenga nyumba kunahitaji umakini mkubwa sana na wakati mwingine mwenye kujenga anahitajika kuwepo eneo la ujenzi mara kwa mara na ikibidi kushiriki katika hatua zote za kuanza wazo la ujenzi mpaka kukamilika kwa nyumba yake. Ukaribu huu unakusaidia kupata nyumba na makazi ya ndoto yako.

Kwa kuangalia msingi kwamba atakayeitumia ni wewe na familia yako, ni wazi kuwa unahitaji kuhakikisha unapata makazi yaliyo bora na yatakayodumu kwa muda mrefu. Pengine, yawezekana ukawa huna kabisa ufahamu wowote kuhusu namna ya kufanya ujenzi wako na kuwa vile unavyotamani. Pengo hilo linazibwa na wataalamu wa ujenzi kama ukiamua kuwashirikisha. Hawa watakusaidia kufanya ndoto yako kuwa kweli na kukuongoza kupata bidhaa za gharama nafuu na bora. 


Mtaani kuna mafundi wengi wazuri na wazoefu lakini wana dosari ya kujenga kwa mazoea pekee na kukariri kazi nyingine zilizopita na ndio maana ni rahisi kukuta mitindo ya nyumba iliyojengwa na fundi mmoja ikifanana kwa mambo mengi. Hali itakuwa tofauti kama mafundi hawa watashirikisha ujuzi wao na utaalamu mwingine ili kuweza kufanikisha kile anachohitaji mwenye kutaka nyumba.

Katika kunogesha mada yetu hii, nadhani ni vyema pia tukafahamishana na kujikumbusha baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kujenga nyumba yako kwa upya kabisa, na hasa ikiwa ndio mara yako ya kwanza kufanya ujenzi:


1.    Kuwa na dondoo kadhaa kuhusu gharama za ujenzi
Kabla ya kuanza ujenzi, fanya tathmini binafsi ili uweze kujua kama unaweza kumudu gaharama ya nyumba unayotaka kwa ukubwa gani kwa muda kiasi gani. Mambo mengine ni malighafi utakazotumia na zitapatikana wapi nan i wapi utajenga. Mambo yote haya ukiyatathmini kwa usahihi y1akupa muelekeo wa gharama na jinsi utakavyofanikisha ujenzi wako.

2.    Fahamu aina ya mafundi na wataalamu utakaowahitaji kukujengea
Ni muhimu pia kuwajua mafundi wazuri na unafuu wao wa gharama sambamba na wataalamu washauri na wachora ramani watakaokusaidia hasa kwa miradi mikubwa. Endapo utataka kuuza kazi zote kwa mtu mmoja ni muhimu pia kuwafahmu uwezo wake, gharama, ubora wa kazi afanyazo na uaminifu wake kwenye kazi na usimamizi wa fedha.

3.    Fahamu kuhusu taratibu za kisheria zinazosimamia maswala ya ujenzi katika eneo la Mji unaoishi
Kila mamlaka ya Mji inataratibu zake za upangaji mandhari ya mji wake kwa makazi na matumizi ya umma, viwanda n.k. Ni muhimu kufahamu mamalaka ya eneo husika imepanga matumizi gani kwenye eneo unalotaka kujenga. Idara ya ardhi itathibitisha umiliki wa eneo na uhalali wa matumizi tarajiwa na idara ya ujenzi watakagua michoro kama inakindhi viwango vya ubora na miundombinu ya maji taka na kutoa Kibali cha Ujenzi. Kwa tatizo la kuwa na maeneo mengi yasiyopimwa, Mabaraza ya Ardhi ya Kata husaidia kutoa uthibitisho wa matumizi ya eneo husika kama halijapimwa. Fuata masharti ya ujenzi kuepuka usumbufu usio na sababu.

4.    Fikiria mahitaji halisi na muundo wa nyumba unayoitaka
Kama ni nyumba ya familia au biashara, ni wewe ndiye unayejua mahitaji halisi kwa maana ya idadi ya vyumba, matumizi yake na pengine muonekano unaoutamani. Mbunifu majengo anaweza kukuongoza kupata mchoro mzuri kwa viwango vya nafasi kitaalamu ili kusitokee nyumba ikajenga halafu ikaonekana chumba Fulani ni kikubwa sana au kimepungua. Kwa hiyo katika hatua hii unafanya kama vile ndio uko ndani ya nyumba na unaigiza akilini kama ndio unaona maisha halisi ndani ya nyumba, unaona swichi za umeme na taa zilipo na kukuhudumia vizuri.

5.    Fikiria mandhari ya nje ya nyumba
Watu wengi hasa wanaokopi ramani tu na kujenga wanakosa umaridadi wa mandhari ya nje. Ni vyema sana ukajenga kufuatana na muundo wa kiwanja chako. Kwa hiyo, utaona umuhimu wa kupata mtaalamu akakutengenezea ramani itakayoendana na eneo lako. Kuna mambo ya kuzingatia kama sehemu ya kuegesha gari, kuanikia nguo na shughuli za uwani, mahali pa kupumzikia na watoto kucheza, na namna ya kuingia nyumbani kwako bila kusahau sehemu sahihi ya kuweka mifumo ya maji taka kwa urahisi wa gari la maji taka kufika hasa kama hakuna mfumo wa majai taka wa umma kuweza kuunganisha.
Mandhari ya nje inahusisha ukijani wa miti na maua. Ni muhimu pia kuwazia mambo kama hayo pia.

6.    Fikiria maisha marefu ya jengo lako
Yawezekana unapanga kujenga nyumba yako eneo fulani ukitaraji litakuwa makazi yako ya kudumu. Lakini, uhalisia ni kuwa maisha nayo hubadilika kadiri majukumu ya kiuchumi yanavyobadilika. Ni nyema ukafikiria kuwa na jengo lisilohitaji ukarabati mkubwa kisi cha kuongeza gharama za maboresho huko baadae endapo itatokeo ukalazimika kufanya biashara. Aina ya malighafi utakayotumia pia ina nafasi kubwa kwenye gharama za ukarabati muda baada ya muda.

7.    Fanya uchaguzi mzuri wa finishing materials na decorations

Ni kawaida kukuta nyumba imebuniwa vizuri lakini finishing touch yake na rangi vinafanya iwe ya muonekano usiopendeza. Tumia muda mwingi kupeleleza huku ukishauriana na wataalamu na kusoma majarida mbalimbali ili uweze kupata chaguo sahihi la rangi na malighafi nyingine za kumba nyumba yako kwa ndani na nje. Kuna rangi maalumu kwa ndani pekee na nyingine kwa nje pekee. Halikadhalika madhari ya majirani zako na ukijani uliokuzunguka navyo vinaathiri aina ya urembo wa nyumba. Muhimu kushirikisha wataalamu wa kazi husika kukusaidia mawazo na ushauri.




Kwa hiyo, usiposhirikisha wataalamu katika ujenzi wako unakosa faida zifuatazo:

1.       Kupata aina ya nyumba inayojitosheleza kuendana na matamanio yako. Katika ubunifu kuna mambo usiyoyajua ambayo wataalamu watakusaidia kuyafahamu, matahali uhusiano wa uelekeo wa upepo na milango/madirisha (cross ventilation) n.k. Ukimshirikisha mbunifu akayaweka mawazo yako katika mchoro, atakusaidia kupata picha halisi ya jinsi nyumba yako itakavyokuwa nah ii itakuongezea hamasa ya kukamilisha ndoto yako.



2.       Kujenga kwa ramani/michoro ya nyumba. Michoro hii itakusaidia kwa masuala mengine kama bima, kupata mkopo, kuuza n.k. Itakusaidia pia kama utahitaji kufanya maboresho ya nyumba yako na kuwa rahisi kwa fundi mwingine kujua eneo Fulani kuna nini katika nyumba.

3. Kushirikisha wataalamu kutakusaidia kujua makadirio ya gharama za ujenzi wako. Makadirio haya hayatawezekana kukupa uhalisia kama hutakuwa na michoro yenye vipimo na mapendekezo ya finishing, milango, madirisha, na aina ya uezekaji wa paa. Michoro hii utaipata kwa mbunifu wa majengo endapo utamshirikisha. Ukishakuwa na michoro ya jengo lako, unaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujua ujenge namna gani kwa awamu hasa kama huna nguvu ya kujenga nyumba nzima kwa wakati mmoja. Bila michoro utajikuta unajenga na kuongeza vyumba kwa mpangilio usioshabihiana.

4.       Kushirikisha wataalamu kutakuepusha kujikuta unaingia kwenye hasara ama ya kubomolewa nyumba au kulipishwa faini zisizo za lazima kwa ama kupuuza au kutojua na kufuata utaratibu fulani.  Wakati mwingine ukipata mtaalamu mwaminifu atakusaidia kutotapeliwa na maofisa wasio waaminifu.

5.       Nafasi ya kushauriana na mtaalamu mchoraji namna ya kuongeza au kupunguza ukubwa wa jengo lako wakati ujenzi ukiendelea kwa msingi kwamba wakati wowote mawazo yanaweza kubadilika na kutamani eneo Fulani likae tofauti na lilivyobuniwa awali.

6.       Kama unataka kujenga kwenye eneo ambalo halijapimwa, mtaalamu atakusaidia kupata michoro ya jengo ambayo hata wakati wa ukaguzi wa baadae bado jengo lako litapimwa na kuonekana liko kwenye viwango na kuwa na thamani nzuri.

7.       Kushirikisha wataalamu waaminifu kutakusaidia kuepukana na wachakachuaji wakitumia kigezo cha wewe kutokuwa na ufahamu na mambo ya ujenzi. Kuna baadhi ya wajenzi si waaminifu na wanaweza kukupa hesabu kubwa za vifaa kinyume na uhalisia kwa lengo la kupata faida zaidi.
8.       Kupata kilicho bora na kwa thamani halisi ya fedha zako.

9.       Wataalamu watakusaidia kupata mbadala wa malighafi ya kutumia katika ujenzi wako huku ubora na uzuri wa kazi ukiwa vile vile kama unavyotamani. Hii ni pamoja na ushauri kuhusu malighafi zinazoweza kukuongezea gharama za ukarabati wa nyumba yako mara kwa mara.

10      Wataalamu watakusaidia kujua ukubwa wa chumba kwa matumizi tofauti kuendana na ukuaji wa teknolojia. Mathalani size ya madirisha, milango, vitasa na hata ukubwa wa maeneo kama choo na bafu ili kutosheleza vifaa utakavyonunua kwa ajili ya matumizi yako. Hata namna ya kupanga sebule kisasa kwa uwiano mzuri na sebule, jiko na veranda ni mambo ambayo utayapata kwa ushauriano mzuri na mtaalamu wa ujenzi.

11      Kuepuka hasara ya kujenga nyumba kubwa isiyosadifu mahitaji halisi kwa mhusika kutofahamu namna ya kujenga kulingana na mahitaji ya wakati gani.

Nyumba iliyojengwa kwa kubuniwa vizuri huleta raha kuishi ndani yake maana inakuwa na mpangilio unaotoa uhuru kwa kila memba wa familia kufurahia eneo lake na kuweka usiri wa mambo ya familia na wageni. Unaweza kujiuliza, kuna sababu yeyote ya msingi kwa mtu anayejenga nyumba ya milioni 65 lakini anakwepa kupata michoro kwa gharama ya shilingi laki tano tu au hata pungufu?

Kumbuka, katika ujenzi wa nyumba, kosa likishafanyika awali na nyumba kukamilika ni gharama sana kurekebisha. 


Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Blogger (http//:arusha255.blogspot.com na http//:ujenzidirect.blogspot.com)
Project QS, Proposed PPF Plaza Corridor Area Arusha
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com

Thursday, December 21, 2017

Unafahamu nini kuhusu Window-Sill? Soma hapa

Window-sill ni kimkanda cha zege kwa unene wa mpaka kufikia mm 75 kinachoweka chini ya dirisha kwa ajili ya kuongeza urembo (muonekano mzuri wa dirisha na kusaidia kuelekeza maji  ili yasiingiendani au kubaki kwenye dirisha kwa kutiririka yenyewe kufuata ulalo unaokuwepo kama picha zetu zinavyoonesha.

Unaweza kuzijengea hapo hapo dirishani kwa kusuka box lake, kweka nondo au wiremesh; au kununua ambazo zimeshatengenezwa tayari na kuzipachika eneo husika au unaweza pia zitengeneza pembenni wewe mwenyewe na kuzipachika dirishani na kisha kufanyia finishinh inayofaa.

Ili kufanya kazi ya kuondosha maji (to drain water) kwa usahihi bila kuchafua ukuta, huwa kuna kimfereji (throat) kinawekwa kwa chini ili maji yakiwa yanatiririka yasiweze kugeuka na kuukuta ukuta.

Maji tunayoyazungumzia hapa ni yale yanayoweza kufikia dirisha kutokana na aidha mvua ya upepo au wakati wa kusafidha madirisha.   





NOGESHA UREMBO WA NYUMBA KWA KUWEKA 'PLANTER' ZA MAUA


Baadhi ya watu hujenga nyumba zao kwa kutilia mkazo urembo wa ndani pekee. Hata wakati wa kununua kiwanja husahau kufikiria na mahitaji ya nyumba kwa nje na kujikuta wananunua maeneo ambayo hayatoshelezi kujenga nyumba na kuacha eneo la wazi kwa maana ya bustani za kupumzikia, maeneo ya kuanikia nguo, kuegesha magari na hata kutengeneza urembo mwingine wa kuzunguka jengo.

Picha hii zinaonesha baadhi ya urembo wa mawe kuzunguka nyumba ukipambwa kwa maua. Hizi tunaita "planter boxes" au hata "flower boxes".  Ni nzuri zaidi kwa nyumba ambayo imejengwa kwa kuwa na msingi mrefu kutokea kwenye udongo. Unaweza kuotesha maua peke yake au kuchanganya na nyasi/ukoka kutegemeana na ubunifu wako. Zaidi kwenye muonekano wa mbele ya nyumba unapoingilia.

Picha zingine zinaonesha uendelezaji wa bustani za maua na ukoka kupamba eneo la makazi. Unaweza kuiga vitu vizuri kama hivi na ukaboresha nyumbani kwako.






Tangastone Surfacing with regular pattern!




Regular pattern Tangastone surfacing to floor, externally! For your driving areas, parking etc.
TUNAO MAFUNDI WAZURI SANA KUKUSAIDIA KAZI YAKO. WASILIANA NASI UPATE KILICHO BORA +255713705462









Monday, December 19, 2016

Je, unaweza kutofautisha tiles za sakafu na za ukutani!? Tegua kitendawili hapa

Pichani ni ukuta wa uzio wa nyumba (fence) ukiwa umenakshiwa kwa marumaru/tiles.
Yawezekana ukaona ukuta unapendeza lakini usifahamu kama vigae/tiles vilivyotumika havikuwa sahihi.
Kwa jinsi vigae vinavyotengenezwa, hutengenezwa maalumu vikiwa na sifa maalumu kwa matumizi ya eneo maalumu. Kwa mfano, tiles za kujengea sakafuni hutengenezwa kwa kuwa na sifa (properties) zinazowezesha kufaa kwa matumizi ya sakafu kwa watumiaji kukanyaga wakitembea, halikdhalika za ukutani na ndio maana ukienda dukani unaulizia ama tiles zaukutani au za sakafu. Za uutani nazo unaweza lazimika kuulizia ama za bafuni, jikoni au maeneo mengine kwa urembo. Na za sakafuni pia hutegemeana na mahali zinapowekwa.

Kaika picha zetu hizi zinaonesha ukuta umependeza sana,lakinikama utachunguza vizuri utagundua kuwa tiles zilizotumika hapa hazikuwa maalumu kwa ukuta wa nje na baadhi ni maalumu kwa sakafu. 
Lengo la posti hiinikujaribu tu kukumbushana kukumbuka kuwa kuna tofauti ya hizi tiles kutegemeana na matumizi. Siokila wakati tutegemee mafundi pekee watuelekeze. Ni imani yangu kuwa dondoo kama hizi zitakusaidia kupata kilicho bora zaidi.

Baadae nitaweka maelezo kamili ya tilesnaainazakena wapi zitumike zipi!



Tuesday, November 15, 2016

KUTANA NA MBUNIFU MAJENGO EDWARD KAYOMBO HAPA! ISHI KATIKA NDOTO YAKO

Leo nimekusogeza karibu na mtaalamu wa ubunifu wa majengo ya aina mbalimbali. Anafahamika kama Edward Kayombo na kama utakuwa umefurahia moja ya kazi zake unaweza mcheki kwa nambari 0762 965 587. Ikikosekana unaweza kuwasiliana nasi kwa 0757718080 tukakusaidia kupata ukitakacho! Karibu sana.
Baadhi ya kazi zake za ubunifu ni hizi hapa chini