• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Showing posts with label Ramani. Show all posts
Showing posts with label Ramani. Show all posts

Friday, December 22, 2017

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KATIKA UJENZI WETU? - PART V: FAHAMU HASARA ZINAZOKUKABILI

KARIBU KATIKA SEMEHU YA MWISHO YA MAKALA YETU INAYOHOJI “TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?”. 

Sehemu iliyopita tuliweza kuwafahamu baadhi ya wataalamu muhimu katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, halikadhalika miradi mingine kama ujenzi wa barabara, madaraja na mabwawa ya maji.


Katika kuhitimisha makala yetu hii, leo tutahitimisha kwa kauangalia baadhi ya faida tunazozikosa kwa kutowashirikisha wataalamu katika kufanya miradi yetu ya ujenzi, hasa kwa nyumba zetu za makazi.

Kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, nchi yetu pia imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa nyumba na makazi bora ya watu kuishi. Watu wengi wamejikuta wakijenga kiholela kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na mamlaka za miji kutowajibika ipasavyo kusaidia jamii kuwa na makazi bora na yanayokidhi mahitaji ya sasa na baadae.


Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi. Wataalamu wanaposhirikishwa Serikali yetu inakuwa na uhakika kuwa mipango, sheria, kanuni za ujenzi, na viwango vya ujenzi vinazingatiwa ili kuiwesesha kupanga mipango ya kuhudumia jamii yote kwa mahitaji kama miundombinu ya umeme, kukabili majanga ya moto, maji safi na maji taka.

Kama tulivyofahamu awali, Ujenzi ni teknolojia ya kujenga nyumba, viwanda, barabara, daraja au hata miji. Ni kazi inayohusisha wataalamu wengi na ngazi mbalimbali ya kupanga na kutekeleza. Majengo madogo yanajengwa na watu binfasi kufuatana na maarifa yao bila kuhitaji mpangilio mkubwa kwa kutumia mafundi wenye ujuzi kiasi kutoka vyuo vya ufundi au waliojifunza kupitia maarifa ya watu waliowatangulia. Mamlaka ya Mji husika hulazimika kushirikishwa ili kuruhusu mpangilio unaoruhusiwa kisheria.
Miradi mikubwa ya ujenzi huhitaji mpangilio maalumu na ni lazima kwa mwenye jengo kutafuta kwanza ushauri wa wataalamu, ambao watasimamia kazi yake kuanzia mwanzo wa ubunifu mpaka kukamilika kwa ujenzi.

Mhadisi na msanifu majengo watachora michoro ya jengo. Wataalamu wakadiriaji gharama watakadiria mahitaji ya vifaa na gharama za jengo, usimamizi na malipo mengine ya vibali. Watatafutwa wakandarasi ambao watakaa na kupanga mahitaji ya muda, pesa, wafanyakazi na mashine zitakazotumika.
Kisha ujenzi utasimamiwa na mhandisi na msanifu wa jengo pamoja na wataalamu wengine ambao wamesajiliwa na kupewa vibali vya kufanya kazi hiyo na mamlaka husika. Mamlaka ya mji husika nayo itahusika na watu wake wa ardhi na mipango miji. 

Yote yakizingatiwa na kutekelezwa kwa usahihi na uaminifu hitimisho ni kupata jengo zuri na lenye thamani kulingana na gharama zilizotumika, ambayo ni faida kwa mmiliki wa jengo. 

Kwahiyo, ukiachana na utambulisho huo mpana kuhusu majengo makubwa tufikirie sasa kwa udogo wa majenzi yetu ya makazi ya kuishi kwa kuzingatia sharia na taratibu za miji mbalimbali. Ingawa kwa sehemu kubwa nchi yetu ina shida ya maeneo kutopimwa na kutambulika matumizi halali ya ardhi, lakini bado kuna changamoto ya watu wengi kupuuza taratibu zilizopo kwa sababu za kawaida sana.

Kujenga nyumba kunahitaji umakini mkubwa sana na wakati mwingine mwenye kujenga anahitajika kuwepo eneo la ujenzi mara kwa mara na ikibidi kushiriki katika hatua zote za kuanza wazo la ujenzi mpaka kukamilika kwa nyumba yake. Ukaribu huu unakusaidia kupata nyumba na makazi ya ndoto yako.

Kwa kuangalia msingi kwamba atakayeitumia ni wewe na familia yako, ni wazi kuwa unahitaji kuhakikisha unapata makazi yaliyo bora na yatakayodumu kwa muda mrefu. Pengine, yawezekana ukawa huna kabisa ufahamu wowote kuhusu namna ya kufanya ujenzi wako na kuwa vile unavyotamani. Pengo hilo linazibwa na wataalamu wa ujenzi kama ukiamua kuwashirikisha. Hawa watakusaidia kufanya ndoto yako kuwa kweli na kukuongoza kupata bidhaa za gharama nafuu na bora. 


Mtaani kuna mafundi wengi wazuri na wazoefu lakini wana dosari ya kujenga kwa mazoea pekee na kukariri kazi nyingine zilizopita na ndio maana ni rahisi kukuta mitindo ya nyumba iliyojengwa na fundi mmoja ikifanana kwa mambo mengi. Hali itakuwa tofauti kama mafundi hawa watashirikisha ujuzi wao na utaalamu mwingine ili kuweza kufanikisha kile anachohitaji mwenye kutaka nyumba.

Katika kunogesha mada yetu hii, nadhani ni vyema pia tukafahamishana na kujikumbusha baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kujenga nyumba yako kwa upya kabisa, na hasa ikiwa ndio mara yako ya kwanza kufanya ujenzi:


1.    Kuwa na dondoo kadhaa kuhusu gharama za ujenzi
Kabla ya kuanza ujenzi, fanya tathmini binafsi ili uweze kujua kama unaweza kumudu gaharama ya nyumba unayotaka kwa ukubwa gani kwa muda kiasi gani. Mambo mengine ni malighafi utakazotumia na zitapatikana wapi nan i wapi utajenga. Mambo yote haya ukiyatathmini kwa usahihi y1akupa muelekeo wa gharama na jinsi utakavyofanikisha ujenzi wako.

2.    Fahamu aina ya mafundi na wataalamu utakaowahitaji kukujengea
Ni muhimu pia kuwajua mafundi wazuri na unafuu wao wa gharama sambamba na wataalamu washauri na wachora ramani watakaokusaidia hasa kwa miradi mikubwa. Endapo utataka kuuza kazi zote kwa mtu mmoja ni muhimu pia kuwafahmu uwezo wake, gharama, ubora wa kazi afanyazo na uaminifu wake kwenye kazi na usimamizi wa fedha.

3.    Fahamu kuhusu taratibu za kisheria zinazosimamia maswala ya ujenzi katika eneo la Mji unaoishi
Kila mamlaka ya Mji inataratibu zake za upangaji mandhari ya mji wake kwa makazi na matumizi ya umma, viwanda n.k. Ni muhimu kufahamu mamalaka ya eneo husika imepanga matumizi gani kwenye eneo unalotaka kujenga. Idara ya ardhi itathibitisha umiliki wa eneo na uhalali wa matumizi tarajiwa na idara ya ujenzi watakagua michoro kama inakindhi viwango vya ubora na miundombinu ya maji taka na kutoa Kibali cha Ujenzi. Kwa tatizo la kuwa na maeneo mengi yasiyopimwa, Mabaraza ya Ardhi ya Kata husaidia kutoa uthibitisho wa matumizi ya eneo husika kama halijapimwa. Fuata masharti ya ujenzi kuepuka usumbufu usio na sababu.

4.    Fikiria mahitaji halisi na muundo wa nyumba unayoitaka
Kama ni nyumba ya familia au biashara, ni wewe ndiye unayejua mahitaji halisi kwa maana ya idadi ya vyumba, matumizi yake na pengine muonekano unaoutamani. Mbunifu majengo anaweza kukuongoza kupata mchoro mzuri kwa viwango vya nafasi kitaalamu ili kusitokee nyumba ikajenga halafu ikaonekana chumba Fulani ni kikubwa sana au kimepungua. Kwa hiyo katika hatua hii unafanya kama vile ndio uko ndani ya nyumba na unaigiza akilini kama ndio unaona maisha halisi ndani ya nyumba, unaona swichi za umeme na taa zilipo na kukuhudumia vizuri.

5.    Fikiria mandhari ya nje ya nyumba
Watu wengi hasa wanaokopi ramani tu na kujenga wanakosa umaridadi wa mandhari ya nje. Ni vyema sana ukajenga kufuatana na muundo wa kiwanja chako. Kwa hiyo, utaona umuhimu wa kupata mtaalamu akakutengenezea ramani itakayoendana na eneo lako. Kuna mambo ya kuzingatia kama sehemu ya kuegesha gari, kuanikia nguo na shughuli za uwani, mahali pa kupumzikia na watoto kucheza, na namna ya kuingia nyumbani kwako bila kusahau sehemu sahihi ya kuweka mifumo ya maji taka kwa urahisi wa gari la maji taka kufika hasa kama hakuna mfumo wa majai taka wa umma kuweza kuunganisha.
Mandhari ya nje inahusisha ukijani wa miti na maua. Ni muhimu pia kuwazia mambo kama hayo pia.

6.    Fikiria maisha marefu ya jengo lako
Yawezekana unapanga kujenga nyumba yako eneo fulani ukitaraji litakuwa makazi yako ya kudumu. Lakini, uhalisia ni kuwa maisha nayo hubadilika kadiri majukumu ya kiuchumi yanavyobadilika. Ni nyema ukafikiria kuwa na jengo lisilohitaji ukarabati mkubwa kisi cha kuongeza gharama za maboresho huko baadae endapo itatokeo ukalazimika kufanya biashara. Aina ya malighafi utakayotumia pia ina nafasi kubwa kwenye gharama za ukarabati muda baada ya muda.

7.    Fanya uchaguzi mzuri wa finishing materials na decorations

Ni kawaida kukuta nyumba imebuniwa vizuri lakini finishing touch yake na rangi vinafanya iwe ya muonekano usiopendeza. Tumia muda mwingi kupeleleza huku ukishauriana na wataalamu na kusoma majarida mbalimbali ili uweze kupata chaguo sahihi la rangi na malighafi nyingine za kumba nyumba yako kwa ndani na nje. Kuna rangi maalumu kwa ndani pekee na nyingine kwa nje pekee. Halikadhalika madhari ya majirani zako na ukijani uliokuzunguka navyo vinaathiri aina ya urembo wa nyumba. Muhimu kushirikisha wataalamu wa kazi husika kukusaidia mawazo na ushauri.




Kwa hiyo, usiposhirikisha wataalamu katika ujenzi wako unakosa faida zifuatazo:

1.       Kupata aina ya nyumba inayojitosheleza kuendana na matamanio yako. Katika ubunifu kuna mambo usiyoyajua ambayo wataalamu watakusaidia kuyafahamu, matahali uhusiano wa uelekeo wa upepo na milango/madirisha (cross ventilation) n.k. Ukimshirikisha mbunifu akayaweka mawazo yako katika mchoro, atakusaidia kupata picha halisi ya jinsi nyumba yako itakavyokuwa nah ii itakuongezea hamasa ya kukamilisha ndoto yako.



2.       Kujenga kwa ramani/michoro ya nyumba. Michoro hii itakusaidia kwa masuala mengine kama bima, kupata mkopo, kuuza n.k. Itakusaidia pia kama utahitaji kufanya maboresho ya nyumba yako na kuwa rahisi kwa fundi mwingine kujua eneo Fulani kuna nini katika nyumba.

3. Kushirikisha wataalamu kutakusaidia kujua makadirio ya gharama za ujenzi wako. Makadirio haya hayatawezekana kukupa uhalisia kama hutakuwa na michoro yenye vipimo na mapendekezo ya finishing, milango, madirisha, na aina ya uezekaji wa paa. Michoro hii utaipata kwa mbunifu wa majengo endapo utamshirikisha. Ukishakuwa na michoro ya jengo lako, unaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujua ujenge namna gani kwa awamu hasa kama huna nguvu ya kujenga nyumba nzima kwa wakati mmoja. Bila michoro utajikuta unajenga na kuongeza vyumba kwa mpangilio usioshabihiana.

4.       Kushirikisha wataalamu kutakuepusha kujikuta unaingia kwenye hasara ama ya kubomolewa nyumba au kulipishwa faini zisizo za lazima kwa ama kupuuza au kutojua na kufuata utaratibu fulani.  Wakati mwingine ukipata mtaalamu mwaminifu atakusaidia kutotapeliwa na maofisa wasio waaminifu.

5.       Nafasi ya kushauriana na mtaalamu mchoraji namna ya kuongeza au kupunguza ukubwa wa jengo lako wakati ujenzi ukiendelea kwa msingi kwamba wakati wowote mawazo yanaweza kubadilika na kutamani eneo Fulani likae tofauti na lilivyobuniwa awali.

6.       Kama unataka kujenga kwenye eneo ambalo halijapimwa, mtaalamu atakusaidia kupata michoro ya jengo ambayo hata wakati wa ukaguzi wa baadae bado jengo lako litapimwa na kuonekana liko kwenye viwango na kuwa na thamani nzuri.

7.       Kushirikisha wataalamu waaminifu kutakusaidia kuepukana na wachakachuaji wakitumia kigezo cha wewe kutokuwa na ufahamu na mambo ya ujenzi. Kuna baadhi ya wajenzi si waaminifu na wanaweza kukupa hesabu kubwa za vifaa kinyume na uhalisia kwa lengo la kupata faida zaidi.
8.       Kupata kilicho bora na kwa thamani halisi ya fedha zako.

9.       Wataalamu watakusaidia kupata mbadala wa malighafi ya kutumia katika ujenzi wako huku ubora na uzuri wa kazi ukiwa vile vile kama unavyotamani. Hii ni pamoja na ushauri kuhusu malighafi zinazoweza kukuongezea gharama za ukarabati wa nyumba yako mara kwa mara.

10      Wataalamu watakusaidia kujua ukubwa wa chumba kwa matumizi tofauti kuendana na ukuaji wa teknolojia. Mathalani size ya madirisha, milango, vitasa na hata ukubwa wa maeneo kama choo na bafu ili kutosheleza vifaa utakavyonunua kwa ajili ya matumizi yako. Hata namna ya kupanga sebule kisasa kwa uwiano mzuri na sebule, jiko na veranda ni mambo ambayo utayapata kwa ushauriano mzuri na mtaalamu wa ujenzi.

11      Kuepuka hasara ya kujenga nyumba kubwa isiyosadifu mahitaji halisi kwa mhusika kutofahamu namna ya kujenga kulingana na mahitaji ya wakati gani.

Nyumba iliyojengwa kwa kubuniwa vizuri huleta raha kuishi ndani yake maana inakuwa na mpangilio unaotoa uhuru kwa kila memba wa familia kufurahia eneo lake na kuweka usiri wa mambo ya familia na wageni. Unaweza kujiuliza, kuna sababu yeyote ya msingi kwa mtu anayejenga nyumba ya milioni 65 lakini anakwepa kupata michoro kwa gharama ya shilingi laki tano tu au hata pungufu?

Kumbuka, katika ujenzi wa nyumba, kosa likishafanyika awali na nyumba kukamilika ni gharama sana kurekebisha. 


Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Blogger (http//:arusha255.blogspot.com na http//:ujenzidirect.blogspot.com)
Project QS, Proposed PPF Plaza Corridor Area Arusha
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com

Friday, January 20, 2017

MWONGOZO WA KUCHAGUA RAMANI BORA YA NYUMBA

Ramani ya nyumba-Mali ya P.Joseph

Bila shaka kila mmoja wetu anatamani kumiliki nyumba yake,na bila shaka wale ambao wamekwisha jenga wana ndoto za kujenga tena ama kuwashauri ndugu na marafiki kujenga.

Ujenzi katika sehemu kubwa ya Tanzania haufuati taratibu na sheria za ujenzi wa makazi.Zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha hili lakini kwa leo mjadala utajikita katika namna ya kuchagua ramani bora ya nyumba

Ramani ya nyumba ni dira ambayo ni kazi ya usanifu yenye kuleta picha ya uhalisia utakaofikiwa na kutarajiwa na mteja.Kazi hii hufanywa na msanifu majengo amnbaye kwa lugha ya kiingereza huitwa Architect.

Msanifu husikiliza kwa makini matarajio ya mteja na kuiweka picha ya matarajio katika mchoro (picha).Watu wengi hudhani kazi ya Architect ni kuchora tu ramani,na ndio maana wengi hudhani ni jambo rahisi.Ukweli ni kwamba kazi yake ni kusanifu mawazo ya mteja na kuyaweka kuwa halisi.Kwa maana hiyo,hii ni fani ambayo huitaji umakini na elimu ya kutosha ili kuhakikisha anasanifu jengo ambalo litafanya wanaoishi waishi wakiupata msawazo katika joto,hewa,mwanga na wawe na furaha na kupapenda wanapoishi.

Baada bya maelezo hayo sasa tujiulize je,ramani bora inazingatia mambo gani?Ijulikane kwamba nimejaribu kupitia vigezo vitakavyomfanya kila mtu aelewe

Kwa wale ambao wana mpango wa kujenga nyumba bora za kisasa,mambo
yafuatayo ni muhimu kuyazingatia unapochagua ramani bora kwa ajili ya
nyumba yako: 
Mchoro ukionesha uhusiano uliopo kati ya sehemu moja na nyingine katika eneo (site plan).Picha ni mali ya Nyumba BoraTz


1.Izingatie maono ya mteja (client)-client imaginationikiwa na maana,mteja anapaswa kupata kile anachokipenda na alichofikiri kichwani kwake eitha kwa kuona ama kwa kutarajia 

2.Iwe na uhusiano mzuri kati ya eneo na eneo (mfano sebule na dining,dining na
jiko, sebule na vyumba.

3. Izingatie matumizi bora ya ardhi kwani ardhini gharama ( iwe na mgawanyo bora kati ya eneo linalojengwa, eneo amanafasi ya kutembea (circulating space), eneo la kijana (green
zone)-ama eneo linalopandwa miti, maua na vingine vyenye kuleta uhai.Ni lazima iepuke uwepo wa sehemu zisizo na kazi (dead space)

4.Izingatie hewa na mwanga wa kutosha katika kila eneo linalotumika,nanyumba bora huzingatia hewa na mwanga wa asili na sio artificial air.(viyoyozi)

5.Izingatie uwepo wa sitiri (privacy) –ihakikishe kila mtumiajianakuwa na uhuru wa kutosha na kuepuka muingiliano

6. Izingatie kuliendeleza eneo, lisiwe mfu kwa maana ya kuliharibu ama kuondoa vitu
vya msingi ambavyo vinafanya ardhi iwe oevu/endelevu 

7. Iwe inazingatia kufikika na matumizi kwa watu wa umri wote na maumbile yote mfano wazee,walemavu. 

8. Uzingatie uzuri- iwe inavutia (appealing to eyes) na wakati Fulani mvuto wake uwe wa kipekee ama mfano mahali inapojengwapo, iwe kioo cha eneo,utamaduni na mazingira ya eneo.

9.Izingatie matumizi bora ya maji na nishati,ikihusianisha vema sehemu zinazohitaji matumizi ya maji (wet areas) na zisizohitaji maji |(dry areas), sehemu zenye kuhitaji nishati na kutoa nishati-hot areas na hivyo kurahisisha matumizi bora ya maji na nishati.Na katika zama hizi ambayo dunia inashuhudia uhaba wa maji na nishati katika nchi za Afrika,ni vizuri wasanifu majengo waanze kufikiria majengo ambayo ni rafiki katika matumizi na rafiki wa mazingira

10.Kwa nyumba ambazo ni za wakazi wengi,ni vema ikazingatia kukuza uhusiano na undugu mfano kuwe na kibaraza (verandah ya pamoja), sehemu za mapumziko za pamoja pia,ili kuhakikisha ujamaa na ushirikiano unadumishwa

 Kumbuka nyumba
utakayoijenga ni sehemu ya kudumu ( permanent structures) hivyo ni vizuri ukifahamu mapema mambo haya kabla ya kujenga kuepuka mkanganyiko wa kisaikolojia,maamuzi na uchumi. 
N:B- Nyakati hizi watu wanapenda nyumba ambazo zinaondoa kabisa uhusiano wa kijamii mfano
ukaribu na majirani,ushirikiano-nadhani ni wakati sasa wasanifu majengo Tanzania wafikirie ni jinsi gani kinachoitwa privacy kinavyoathiri ujamaa,enzi za nyerere fikra ilikuwa watu wanaotumia apartment wapike pamoja,wafue sehemu moja,lakini kwa sasa watanzania
wanafiki tofauti na labda kwa sababu hatuna falsafa inayoliunganisha taifa

CHANZO/HATIMILIKI YA STORI: UJENZIBORATZ

Kwa maswali na maoni Wasiliana nasi UJENZIBONGO ama wasiliana na UJENZIBORATZ kupitia anwani pepe nyumbaboratz@gmail.com

UCHAGUZI WA RANGI KATIKA NYUMBA

UCHAGUZI WA RANGI KATIKA NYUMBA

Rangi katika nyumba ina faida kuu mbili,zikiwa ni kuongeza nakshi (kupendezesha) na kazi ya pili ni kulinda kuta.

NYUMBA BORA TZ wamekuandalia picha hizi kuweza kuchanganua masuala ya rangi.







picha zote ni mali ya Joseph P.

Rangi za kuta zinaweza kuwekwa katika makundi mawili ya rangi msingi na rangi sekondari (upili)
Rangi msingi ni rangi ambazo hupigwa ili kuwezesha rangi upili kudumu.Hujulikana kama primer kwa lugha ya kiingereza

Makala hii fupi inalenga kushirikisha wasomaji na wale ambao wangependa kujenga kuhusu uchaguzi wa rangi.

Ni wazi kuwa kila mtu ana uchaguzi wake wa rangi,na mara nyingi kuvutia kwa rangi ni baina ya mtazamaji na maono yake.

Zipo rangi zilizopoa na zinazong'aa sana.Ni sawa na kusema rangi zinazoakisi zaidi mwanga na zile za kutunza mwanga.

CHANZO/HAKI MILIKO: NYUMBABORATZ

Wednesday, December 21, 2016

JE, UNAFAHAMU KUWA UBUNIFU WA JENGO HUAKISI GHARAMA HALISI ?

ujenziBongo.Co.Tz
Kitaalamu. ubunifu wa majengo hufanywa na wataalamu wanaitwa Architects ama kwa kiswahihi wabunifu majengo.

Ubunifu wa jengo ni hali ya kuumba taswira ya kufikirika na kuiweka katika hali  ya mwonekano wa kama kitu halisi, kwamba endapo ujenzi ukifanyika jengo litakuwa namna hiyo.

Ubunifu huwa ni hatua ya awali kabisa kwenye ujenzi kwa mtu ambaye tayari ana kiwanja chake na huwasilishwa kwa njia ya michoro ya kisanifu kama nilivyoeleza hapo juu, kwa kuchukua mawazo na matamanio ya mwenye kutaka kujenga na kuyaweka katika mpangiliowa mahitaji halisi kwa kuzingatia eneola ardhi lilivyo na ukubwa wake bila kusahau mazingira yanayozunguka eneohilo


Baadae utahitaji kujua gharama halisi za nyumba ya ndoto yako kulingana na ubunifu huo kwa bei ya sokoya wakatihuo. Pengine yawezekanaunahitaji kujenga baadae, nayoni sahihi kuwana mchoro na kujiandaa nao.

Hatua hii ningumukidogo na inahitaji uwe mwenye nidhamu sana katika kufikia malengo yako. Yawezekana pia umepata hela za mara moja kutokana na msihemishe zako na ukatamani ufanye uwekezaji wa nyumba. Ili kuepuka kuishia katikati ya safari, ni muhimu ukashirikisha wataalamu wabunifu na wakadiriaji gharama za ujenzi wakakushauri ni jengo gani na la ukubwa gani litatoshea pesa uliyo nayo kwamtindogani.

Kama kichwa cha habari cha somo kinavyoeleza, ubunifu ambao hutoa mwonekano halisi wa nyumba yako hutafsiri gharama halisi ya nyumba yako. Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kusaidia kupunguza gharama kwenye ujenzi na wakati huohuo ukaweza kupata jengo lamuonekano wa nyumba uitakayo. Watu wengi huwa wanajenga tu kwa mazoeana kuiganyumba za majirani, hawajisumbui kufanya ubunifu wa kile ambacho nafasi zao hutamani kuwa nazo. Unaweza kusoma baadhi ya mbinu hapa za kupunguza gharama

Hata hivyo, katika hatua ya ubunifu,zipo namnatofauti zakuweza kushauriana na mbunifu majengo na kuweza ya kupunguza gharama kwa kuondoa baadhi ya mahitaji yasiyo ya lazima, kwa mfano, kupunguza idadi ya kuta za ndani, kutokuwana nafasi nyingi zisizona ulaziman.k

Kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu, unaweza kujenga nyumba bora na ya kisasa, nyumba bora ndogo inayokidhi mahitaji naukaimaliza badala ya kujenga nyumba kubwa kwa mazoea na ukashindwa kuimaliza. Amua! Unaweza! 


Tuesday, November 15, 2016

KUTANA NA MBUNIFU MAJENGO EDWARD KAYOMBO HAPA! ISHI KATIKA NDOTO YAKO

Leo nimekusogeza karibu na mtaalamu wa ubunifu wa majengo ya aina mbalimbali. Anafahamika kama Edward Kayombo na kama utakuwa umefurahia moja ya kazi zake unaweza mcheki kwa nambari 0762 965 587. Ikikosekana unaweza kuwasiliana nasi kwa 0757718080 tukakusaidia kupata ukitakacho! Karibu sana.
Baadhi ya kazi zake za ubunifu ni hizi hapa chini

















Sunday, April 24, 2016

A simple 3 bedrooms residential house 3D model

Muonekano wa mbele

Mounekano wa upande wa ubavuni kulia

Muonekano wa nyuma na baraza ya jikoni/uwani

Upande wa ubavuni kushoto

Mfano wa ubunifu wa jengo la makazi hatua za awali..

Picha hizi zinaonesha mfano wa muonekano wa nje (in 3D view) wa jengo la makazi lililobuniwa kabla ya kujengwa.

Wataalamu wa ubunifu majengo (Architects) hubuni muundo wa jengo mfano kama huu na kisha kusimamia ujenzi wake ili kupata jengo halisi kama lilivyobuniwa.

Katika muonekano wa picha hizi, bado umaridadi wa nje na mazingira na muonekano halisi wa jinsi jengo litakavyokuwa haujakamilika. Lakini mpaka hatua hii tayari unaweza kuwa na michoro (floor plan) na kufanya ujenzi. Hapa bado kuna  hatua zaidi mchoro unapitishwa kwenye program maalumu na kuongeza uhalisia.

Kwa mahitaji binasi ya huduma za ushauri na ubunifu wa jengo lako unalowazia, pamoja na  makadirio ya gharama zake  unaweza kuwasiliana nasi.

Karibu!



SeriaJr