• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Showing posts with label Slider. Show all posts
Showing posts with label Slider. Show all posts

Friday, December 22, 2017

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU WAUJENZI? - PART IV: WAJUE WATAALAMU KWENYE SEKTA YA UJENZI

KARIBU TENA KWENYE MAKALA YETU YA 'TUNAKOSA NINI TUSIPOWATUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?' SEHEMU YA NNE

Tuwajue wataalamu wetu wa ujenzi.

Ndugu msomaji wangu, nikushirikishe sasa kuweza kuwafahamu wataalamu mbalimbali walio na taaluma anuai kuhusiana na masuala ya ujenzi wa majumba. Ni jambo jema kufahamu kuwa wataalamu wote hawa wamesomeshwa na vyuo vyetu vya hapa nchini. Hii ni kusema kwamba utaalamu wa ujenzi ni wetu wenyewe ingawa kwa upande wa bidhaa za ujenzi bado tunategemea sehemu ya utaalamu na ubunifu wa nje ya nchi.

Sote tu mashahidi wa namna taifa la China na raia wake walivyosambaa barani Afrika na Tanzania ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa zao za ujenzi.

NSSF Mafao Haouse, Arusha (Designed by MD Consultancy Ltd)

Wataalamu wengi wa ujenzi nchini wanapata mafunzo yao kwenye taasisi za elumu ya juu kama ATC (Arusha Technical College), MIST (Mbeya Institute of Science and Technology), DIT (Dar es Salaam Institute of Science and Technology), ARU (Ardhi University), CoET n.k; vituo vya mafunzo vya VETA na baadhi ya shule za ufundi kama “Moshi Tech” n.k. 


Shughuli nzima ya ujenzi nchini inasimamiwa na Serikali kupitia Wizara husika na mamlaka zake; na pia Bodi mbalimbali kama Bodi ya maiinjinia-ERB, Bodi ya wakandarasi-CRB, Bodi ya Wakadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo-AQRB bila kuwasahau Baraza la Ujenzi la Taifa-NCC na kwa miundombinu wanaongezeka wakala wa barabara nchini – TANROADS na TARURA.

Ni kina nani na yapi majukumu ya wataalamu (proffesionals) kwenye “kiwanda” cha ujenzi nchini?

Hili ni swali zuri na muhimu ambalo litatuongoza kuwafahamu na kuyafahamu majukumu yao katika ustawi wa sekta ya ujenzi nchini. Baadhi hatuwaoni kwenye ujenzi wa majumba yetu ya kuishi lakini wanafanya kazi katika maeneo mengine makubwa zaidi. 


Tuanze na timu ya wataalamu wanaotambulika kitaaluma kama Geotechnic Engineers (GE). Mpangilio wa masimulizi hautafuata ubora ama umuhimu wa kila taaluma. GE, hawa ni wataalamu wanaohusika na kuchambua sifa za udongo kama sehemu ya taaluma ya uinjia wa majenzi ya barabara, madaraja, mifereji, mabwawa na majengo makubwa, ambapo taaluma hiyo inajulikana kama Civil Engineering.

Mhandisi udongo/Geotechnic Engineer 

Huyu anafanya kupembua sifa za udongo za kimuonekano, kikemikali ambazo zinaweza kuathiri mradi wa ujenzi na namna jingo linavyoweza kukabiliana na matetemeko ya ardhi na majanga mengine na hatimaye kupata muafaka wa aina ya msingi (foundation) wa jengo, daraja n.k unavyopaswa kuwa.

Land Surveyor/mpima ardhi. 
Hili ni kundi linguine la wataalamu wa maswala ya kupima ardhi na mara nyingi wanakuwa sehemu ya utendaji wa kiSerikali. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na Halmashauri za Miji na Majiji ndipo mahali hasa unaweza kuwakuta wataalamu hawa kama maafisa ardhi. Hata hivyo zipo kampuni binafsi pia zinazotoa huduma za upimaji ardhi na wataalamu hawa wanapatikana huko pia.

Kazi yao kubwa katika sekta ya ujenzi kama wataalamu wa kwanza kabisa kufanya kazi eneo la ujenzi kabla ya wengine ni kutambua mipaka ya eneo la ujenzi, kutambua ukubwa wa eneo, kuweka na kukagua beacons, bila kusahau kutambua kiasi cha mbonyeo au mwinuko wa ardhi inayotarajiwa kujengwa. Kazi za taalumu hii zimekuwa zikitolewa zaidi kwa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam.

Mbunifu majengo/Architect

Huyu ndie mtaalamu aliyefuzu mafunzo na kusajiliwa kubuni michoro ya jengo kwa kubadilisha mawazo (concepts) ya mradi fulani na kuyaweka kwenye michoro na muonekano wa uhalisia wa jingo litakavyokuwa likishajengwa. Hufanya kutafsiri mahitaji ya anayetaka kujenga na kuyaweka kwenye uhalisia kwa namna ya kumuwezesha mjenzi kufanya ujenzi.  Hutengeneza taswira ya muonekano wa jengo na mpangilio wa mambo mengine. 

Kabla ya kuanza ujenzi, mbunifu huyu anatakiwa kuchora mchoro wa jingo husika na ndipo ujenzi uanze. Ni rahisi kukosa mwelekeo wa ujenzi kama utaanza kazi ua ujenzi ukiwa huna mchoro unaokuongoza. 

Taaluma ya ubunifu majengo ama Architecture kama taaluma nyingine nayo ina mgawanyo wa utaalamu kwa maana ya ubunifu wa ndani ‘interior design’, mpangilio wan je ya jingo na vitu nama bustani na sehemu za maegesho ‘landscaping’ na ubunifu wenyewe wa jango zima na umaridadi wake wan je na mgawanyo wa vyumba na maeneo huru ndani. 

Bado ni vyuo vikuu vichache ambavyo vinatoa mafunzo ya taaluma hii hapa nchini ambapi pia kuna mafunzo ya wasaidizi kwa ngazi za chini ambao nao hufanya kazi za uchoraji pamoja, kitaalamu hutambulika kama draughtsmen.


Wahandisi/(Civil and Structural Engineers)
Baada ya Mbunifu majengo kumaliza kazi ya kuandaa michoro yake mhadisi ndiye mtaalamu wa pili kuweka utaalamu wake. Mara nyingi kumekuwapo na mchanganyo wa uhandisi na ukandarasi. Kuweka hili sawa kupitia makala hii, ifahamike kuwa mhandisi ni mtaalamu mbunifu wa uimara wa jingo na mkandarasi ni mjenzi wa jingo akifanyika kazi vilivyobuniwa na wahandisi na wabunifu majengo. Mkandarasi anaweza kuwa aidha mtu binafsi au kampuni iliyosajiliwa kufanya kazi ya ujenzi kwa kiwango fulani.

Sasa huyu anayejulikana kama Structural Engineer ndiye Mhandisi hasa na huwajibika kwa uhandisi wa ubora na uimara wa jengo kwa kufanya mahesabu ya uimara (strength), uzito, nguvu na namna vitakavyokabiliana bila kuleta madhara kwenye jengo linalotarajiwa kujengwa.

Ni jukumu la mhandisi huyu kuandaa michoro ya uimara wa jengo kwa maana ya namna nondo na zege na hata vyuma vingine vitakavyokuwa na ukubwa wake kwa maeneo kama nguzo (column), msingi (foundation) bimu (beams), kuta, ngazi za ghorofa na slabu (slabs) kwa upande wa majumba. Halikadhalika huandaa michoro kwa ajili ya madaraja, nguzo kubwa, mabwawa n.k. 

Wakati wa ujenzi anakagua pia ubora wa bidhaa (materials) zinazotumika na namna nondo na zege zinavyotengenezwa kama vinafikia ubora unaotakiwa kama alivyobuni kimahesabu.

Inapotokea jengo limeanguka kwasababu zisizotokana na nguvu za asili kama mtetemeko ya ardhi na milipuko ya bomu kwa mfano, mhandisi ndiye hupewa majukumu ya kuchunguza sababu za kihandisi zilizopelekea hitilafu iliyosabababisha jengo kuanguka kama iivyotokea maeneo ya Kisutu Jijini Dar es Salaam miaka michache iliyopita. 

Mkadiriaji Majenzi/Quantity Surveyor(QS)
Mkadiriaji majenzi kwa baadhi ya nchi hutambulika kama Cost Engineer. Ni sawa na kusema ndiye mhasibu kwenye sekta ya ujenzi. 

Majukumu makubwa ya mkadiriaji majenzi ni kufanya makadirio ya gharama za mradi wa ujenzi. Makadirio hufanyika wakati wa kubuni wazo la mradi, wakati wa ujenzi na wakati wa kuandaa mkataba wa ujenzi kwa ajili ya kupatana na mkandarasi. Makadirio haya hufanyika kimahesabu kwa majengo mapya au yanayokarabatiwa ama kuboreshwa. 

Mkadiriaji majenzi hufanya kazi katika sekta zote mpaka kwenye uchimbaji madini, miundombinu, na majengo ya nyumba za kuishi na majengo makubwa ya viwanda na taasisi za umma au jumuia. Ili kuweza kukamilisha kazi yake hulazimika kutafuta kiasi (quantity) cha visaidizi kama nguvu kazi, zana za kazi, bidhaa za ujenzi n.k. 

Katika miradi mkubwa ya ujenzi QS ndiye huwajibika kufanya yafuatayo
a. Kufanya makadirio ya bajeti ya mradi
b. Kuchanganua madhara yanayoweza kujitokeza kwa kubadilisha dizaini ya jengo na bajeti yako
c. Kuandaa BOQ (kitabu cha makadirio ya gharama na kiwango cha kazi) ambayo husaidia wakati wa kumtafuta mkandarasi wa kutekeleza ujenzi
d. Kuandaa kamabrasha ya tenda za ujenzi na kusimamia zoezi zima
e. Kuhakiki kazi ya ujenzi iliyofanyika na kuipa thamani yake kwa ajili ya kuruhusu malipo kufanyika kwa mkandarasi kwa kiwango cha kazi alichofanya.
f. Kusimamia mabadiliko yate ya kimuundo na kiujenzi na hata gharama wakati ujenzi unaendelea tofauti na kilichobuniwa awali.
g. Kuandaa hesabu za malipo ya mwisho kwa makandarasi ilikwa mmradi umekamilika kwa namna taratibu na sharia za ujenzi zinavyoelekeza na majukumu mengine. 

Mjenzi/Builder
Mjenzi au builder husoma na kuielewa michoro yote na maelekezo mengine na kuangalia inaoana vipi. Anachanganua uwezekano wa jengo kujengeka na namna litakavyotunzika kama lilivyobuniwa. Ni sawa na kusema huyu ni mhakiki ingawa kwa hapa kwetu ni nadra kuwakuta wataalamu hawa kwa majukumu haya kama mtaalamu wa pembeni. Mara nyingi wanakuwa kama sehemu ya wakandarasi.

Mhandisi wa Huduma za Jengo/(Building Service Engineer)
Kwa kawaida jengo halikamiliki kwa kuwa na ubunifu wa jengo lenyewe tu na uimara wake. Kwasababu kila jengo ni maalumu kwa matumizi Fulani huwa kunakuwa na huduma muhimu za kuwawezesha watumiaji wa jengo hilo kuweza kulitumia. Huduma tunazozizungumzia hapa ni kama mfumo wa maji safi na machafu, mfumo wa umeme, mfumo wa mawasiliano ya kitekinohama nausalama.

Huduma nyingine ni mfumo wa kukabiliana na hitilafu ya moto, mfumo wa usafirishaji kwenda na kutoka ghorofani (vertical transportation) na mfumo wa kuweka hali ya ujoto au baridi na kutoa hewa chafu nje ya jengo (mechanical ventilation)

Huduma zote hizi hubuniwa na kusimamiwa na mtaalamu anayetambulika kama Mhandisi wa Huduma za Jengo (Services Engineer) akifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wataalamu wengine ambao nimeshawaelezea hapo awali. 



Mafundi au Artisans
Hawa ndio watu wanaofanya kazi kwa vitendo eneo la ujenzi wakiwa na ujuzi wa namna tofauti tofauti. Mafundi mchundo (Technicians) wanaingia kundi hili pia wakiwa na utaalamu (skills) kwa maeneo tofauti tofauti ya ujenzi kama ufundi seremala, ufundi chuma, ufundi tope (masonry) n.k. 

Wataalamu Washauri (The Consultants)
Kila mradi uliofuata taratibu za ujenzi kwa mujibu wa sharia zetu unalazimika kuwa na timu ya washauri wataalamu kwa msingi kwamba mmiliki (Client) anayetaka kufanya maradi wa ujenzi anaweza kuwa sio mtaalamu wa maswala ya ujenzi na hata akama atakuwa na utaalamu hataweza kuwa na uelewa wa kila kitu. Hivyo inamlazimu kuwa na timu ya watu watakaomshauri na kumsaidia kufanikisha mradi wake ili aweze kupata thamani halisi ya alichowekeza na kilichojengwa kama vinawiana. 

Wataalamu Washauri ni mjumuiko wa wataalamu wote niliowaeleza hapo mwanzo, wataalamu kama Mbunifu Majengo, Mkadiriaji majenzi, Wahandisi wa jengo na Huduma, na wataalamu wengine. 

Hawa washauri wanatakiwa kushirikishwa kuanzia mwanzo kabisa wazo la mradi linapoanza kwsasababu kimajukumu washauri hawa ndio huchukua nafasi ya mmiliki au tajiri wa mradi na kumuwakilisha katika maswala ya kitaalamu. 

Mkandarasi/Building Contractor
Mkandarasi kwa lugha rahisi anahesabika kuwa ni mkusanyiko wa timu ya wajuzi wa masuala ya ujanzi pamoja ambao wao majukumu makubwa ni kubadilisha michoro na kuifanya kuwa uhalisia wa kilichobuniwa. Mkandarasi huwajibika kukusanya vifaa na bidhaa za ujenzi na kutumia utaalamu wa watu wake kufanikisha ujenzi husika mpaka kukamilika kwake na kuwa tayari kwa matumizi yaliyokusudiwa. Kawaida katika miradi mingi kunakuwa na Mkandarasi mkuu na wakandarasi wadogo ambao kwa magawanyo wa majukumu wao hufanya shughuli nyingine ambazo wengine hawawezi. Ndio haswa wanaohusika na ufanikishaji wa huduma za jengo kama nilivyozifafanua awali.

Mkandarasi ninayemzungumzia hapa kisheria ni yule ambaye amepata leseni ya kufanya kazi kutoka Bodi ya Makandarasi nchini (Contractors Registration Board).

Mpaka kufikia hapa ni matumaini yangu kuwa kwa kiasi Fulani nimeweza kudadavua maswala machache muhimu ambayo kimsingi yanatoa jibu la tunakosa nini tusipotumia wataalamu kwenye ujenzi wa nyumba zetu. Kama umebahatika kupeleleza nyumba zilizojengwa kwa kushirikisha wataalamu hata kwa hatua mojawapo na zile ambazo zimejengwa bila kuwashirikisha utakubaliana name kuwa zilizoshirikisha wataalamu zinaubora na umaridadi mzuri tofauti na zile ambazo hazikuhusisha wataalamu hata kwa ushauri tu. 

Tukutane tena katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala hii ambapo tutaweza kufahamu sasa nini tunachokikosa. 


Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU? - PART III: SOMA HAPA UNACHOTAKIWA KUFANYA UKITAKA KUJENGA NYUMBA KISASA



ILIPOISHIA SEHEMU YA TATU


Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya maaandalizi muhimu yatakayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. 

Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.

Mfano wa ramani ya nyumba


Jambo la kuanza nalo ni kufikiria mahali sahihi utakapo jenga nyumba yako


Mahali unapotamani kujenga makazi yako yanahusika kuamua aina ya nyumba yako hapo baadae. Inaweza kuwa unawazia kujenga nje ya mji au mjini. Eneo unalotamani kujenga nyumba ya kuishi linaweza kuwa ni eneo lililopimwa ama bado halijapiwa. Ardhi yake ni ya mabonde na milima ama tambarare. Utaangalia matumizi mengine ya eneo hilo na miundombinu yake. Pengine ni eneo jirani na viwanda n.k. Hata udongo na hali ya hewa ya eneo husika inanafasi yake, pengine ni ufukweni mwa bahari.

Kumbuka, uamuzi wa eneo la kujenga unaweza kuashiria uharaka wa kukamilisha kujenga nyumba yako kwasababu kwa mfano kama unatazamia kujenga katika eneo la katikati ya mji huwa ni gharama kubwa na hata upatikanaji wake ni wa taabu kidogo. Ikiwa ni eneo la mjini kuna ugumu wake pia kwa mfano kupata kibali cha kujenga.Miji mingine kwa mfano Jiji letu la Arusha halitoi vibali kwa ujenzi wa nyumba ndogo zisizo za ghorofa kwa maeneo ya katikati ya Jiji.


Kwa eneo ambalo limekwishajengwa na kupangwa kuwa eneo la makazi huwa ni rahisi zaidi hata kupata kibali cha ujenzi wa makazi na miundombinu yake huwa maalumu kwa makazi ya watu.


Jambo la pili kujiandaa nalo ni pesa za kugharamia ujenzi husika hata kwa kuanzia tu na wataalamu utakaowatumia bila kusahahu gharama za mamlaka ya mji au mtaa husika na tozo za vibali mbalimbali vya huduma na ruhusa. Ni vizuri kupanga kiasi cha fedha ulichonacho au kujikusanyia kitakufikisha wapi katika ujenzi wako. Itakuwa gharama zaidi kama utaamua kupata eneo na kujenga hapo hao, ingawa kwa baadhi wanaweza.

Hata hivyo, kutokuwa na pesa ya kuanza ujenzi hadi kumaliza hakuwezi kuwa kizuizi cha kutojenga nyumba iliyobora. Kamwe usikate tamaa ama kuamua kujenga tu alimradi umejenga kitu ambacho hakina ubora na hakikidhi mahitaji kitaalamu. Kuna taasisi nyingi za mikopo (loans and mortgages) zinaweza kukusaidia. 

Lakini pia kwa kujikusanyia pesa kidogokidogo na kuzitunza kwa malengo ya ujenzi unaweza kufanya ujenzi wako ulio katika ubora mzuri. Kuna wataalamu washauri wa maswala ya gharama za ujenzi kabla, baada na wakati wa ujenzi wanaweza kusaidia. Kitaalamu wanaitwa  Quantity Surveyors ama Cost Engineers kwa baadhi ya nchi kama Uingereza.

Hatua ya ya tatu, baada ya kuwa umejiandaa kifedha na maandalizi mengine kufanya ujenzi, fikiria sasa kumpata mtaalamu mbunifu wa majengo atakayekusaidia kuandaa mchoro wa nyumba yako. Hatua hii ni muhimu zaidi na ndipo watu wengi wanapokosea na kujikuta wakitumia gharama kubwa baadae kujenga nyumba ambayo haiwapi raha waliyoitamani kwa kuwazia ama kwa kuona mahali fulani ama kwenye mitandao ya internet. Shirikiana na mchoraji akuelekeze namna ambavyo mawazo yako ameyaweka kwenye mchoro kama unavyohitaji na kuhakiki ukubwa wa nyumba na mgawanyo wa vyumba.

roof structure - seriajr
Jengo kwa matumizi ya kuishi likiwa katika hatua za uezekaji
Kuna baadhi ya watu wanaweza kuona muonekano wa nyumba kwa nje wakavutiwa nao na kumuonesha fundi mjenzi na kumtaka awajengee wakiamini kwa muonekano wa nje watapata kuridhika hata na ndani. Bahati mbaya wanakuwa hawafahamu kuwa mgawanyo wa vyumba ndani, saizi yake na mpangilio wa mahusiano ya vyumba na maeneo tofauti ndio huleta mvuto, ubora na raha ya nyumba husika.

Kwa hiyo, kama nilivyoeleza kuwa ukishakuwa umejiandaa unamtafuta mtaalamu mbunifu wa majengo, kitaalamu anaitwa Architect (tutajifunza baadae nafasi yake katika ujenzi pamoja na wasaidizi wake). Unampatia mahitaji yako halisi na namna unavyotamani nyumba yako iwe, nae kwa utaalamu wake atakushauri namna nzuri ya kuyapanga mahitaji yako hayo na kuyaweka kwenye mchoro ambao fundi anaweza kuutumia kujenga nyumba yako.

Mtaalamu huyo atayaunganisha mahitaji yako na kuyapanga kitaalamu ili kuweza kupata jengo ambalo litakuwa na sifa za mahitaji ya nyumba bora. Mifano ya mahihaji muhimu ni madirisha yanayoruhusu hewa kwa kupangilia uhusiano mzuri na milango kupata kitu kinachoitwa kitaalamu kama cross ventilation. Pia mpangilio wa vyumba, sehemu ya chakula, jiko na vyoo bila kusahau baraza na korido.


Utoaji na uingizaji wa maji masafi na machafu una umuhimu wake pia na halikadhalika namna sebule itakavyokaa na kutumiwa na wageni na watu watakaokuwa wanaishi kwenye hiyo nyumba bila kusahau maliwato kwa mgeni. Pia maswala ya usalama wa jengo dhidi ya hatari ya moto na hata mpangilio wa madirisha kuoanish na uelekeo wa upepo.

Ni vizuri pia tukifahamishana kuwa kwa mujibu wa sheria zetu za ujenzi hapa nchini kuhusu nyumba za kuishi (residential houses), endapo mtu anajenga jengo la ghorofa analazimika kumtafuta injinia amsaidie kumuandalia mchoro utakaohusu uimara wa jeingo kwa maana kwamba utakuwa ni mchoro unaoonesha namna nondo zitakavyojipanga, idadi na saizi yake, bila kusahahu ubora wa zege na mambo mengine yahusuyo uimara wa jingo lako.

Sasa kama utakuwa unawazia jengo la namna hiyo ni lazima kisheria kutafuta Structural Engineer akusaidie kuandaa michoro mingine.


Hatua ya nne, baada ya kuwa na mchoro wako utahitaji kujua makisio ya gharama halisi za mradi ama kwa kujenga mpaka kumaliza ama kwa awamu tofauti. Mtaalamu mkadiriaji majenzi niliyemueleza hapo awali kuwa anatambulika kitaaluma kama Quantity Surveyor/Cost Engineer atahitajika kufanya hesabu za makadirio ya gharama ili uweze kujua namna halisi ya kujipanga kutegemeana na mchoro ulivyo na jinsi utakavyokuwa umechagua material gani za kutumia kwa kushauriana na kitaalamu. QS huyu atakusaidia kubajeti vizuri na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima au bidhaa bora na rahisi lakini lengo likibaki kupata nyumba bora. Wakati mwingine hata fundi mzoefu anaweza kukusaidia.

Hatua ya tano. Mpaka hapo utakuwa umeshakamilisha hatua za awali muhimu kabla ya kuanza mradi wako wa ujenzi. Sasa unaweza kuwatafuta wataalamu wajenzi kwa maana ya kampuni au mafundi binafsi wenye uelewa mzuri wa kutafsiri michoro ya ujenzi ili muweze kukubaliana na kuanza kazi ya ujenzi tukichukulia kuwa eneo tayari lipo, limehakikiwa na kuonekana liko tayari kwa ujenzi na udongo wake ukiwa umeshaoanishwa na aina ya msingi wa nyumba utakavyokuwa.

nembo ya AQRB
Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 ya AQRB, Bodi ya Wakadiria Majenzi na Wabunifu wa Majengo inahimiza matumizi ya kampuni za wakandarasi zilizosajiliwa kufanya ujenzi kwa kufuata mchanganuo ufuatao

· Ujenzi wa majengo yoyote ya ghorofa ya ukubwa na thamani yeyote
·  Majenzi yote ya makazi yanayozidi thamani ya sh milioni 50 na ujenzi wake unahitaji uhandisi (structural inputs)
· Ujenzi wa majengo yote ya umma kama shule, hospitali, masoko, makanisa, misikiti, kumbi za starehe n.k


·  Ujenzi wa majengo ya viwanda, maghala n.k

Kwa hiyo utaona ni namna gani sheria inajaribu kumsaidia mjenzi kupata kilicho bora kwa kutumia wataalamu. Ni ukweli kwamba idadi kubwa ya watanzania hawana uwezo wa kujenga kwa kutumia wataalamu na hata kiwango cha nyumba yenye thamani ya milioni 50 wakati wa kuanza ujenzi hawana. Baadhi wanazikwepa kampuni wakijaribu kuokoa gharama za ziada ili zitumike kwenye ujenzi wenyewe.
Sehemu ya kazi za kweka urembo wa nyumba kwa ndani. Kazi ya SeriaMjenzi
Hata hivyo, kutokuwa na uwezo wa kukodi ama kuajiri kampuni kufanya ujenzi wako sio kipingamizi cha kutowashirikisha wataalamu kama nilivyoeleza hapo awali. 

Unaweza kuepuka kutumia kampuni kujenga lakini kama uliwashirikisha wataalamu kuandaa wazo la ujenzi wako kitaalamu unaweza kumtumia fundi yeyote mjuzi akakusaidia kujenga kwa gharama ambazo mara nyingi ni pungufu kidogo ya gharama za makampuni. Mtaani tunao mafundi wengi na wataalamu baadhi wakiwa wamehudhuria mafunzo rasmi chuoni na wengine wakijifunzia tu mtaani na kujikusanyia uzoefu. Wote ni wataalamu. 


Itaendelea Sehemu ya nne, ambapo tutaweza kuwajua wataalamu mbalimbali wanaohusikana ujenzi.

Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com


TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI ? - PART II: DHANA YA MAKAZI BORA


Leo ikiwa ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hii tutaangalia kwa ukaribu zaidi dhana nzima ya nyumba bora ya binadamu ambapo madhumuni na miundo yake hutegemeana sana na hali halisi ya kidunia kwa utofauti wa sehemu moja na nyingine. Hii ni dhana tata kidogo.

Dhumuni kubwa la kuwa na nyumba ya kuishi ni kumpatia mwanadamu usiri wa mambo yake binafsi, na kumlinda dhidi ya madhara yatokananyo na hali ya hewa ya kidunia na viumbe wengine hatari kwa binadamu. Malengo mengine ni raha, ufariji na mahali pa kuendeleza uzao na kutunza afya ya mwanadamu. Nyumba ya kuishi inajitofautisha sana na mejengo mengine kama ya biashara, ofisi, masoko, hospitali, viwanda n.k. Tofauti hiyo hutegemeana sana na lengo la matumizi ya jengo husika kama nilivyoeleza hapo juu.



Ili jamii iweze kuwa na makazi bora inalazimu timu ya wataalamu mbalimbali washirikiane kwa ukaribu sana ili kufanikisha hilo. Makazi bora lazima yahusishe nyumba bora na miundombinu inayoizunguka. 

Watu wengi wanaamini kujenga nyumba ya kuishi ni jambo gumu sana katika maisha yetu na hivyo kuishia kujenga alimradi tu ni kijumba cha kujisitiri. Ni kweli ujenzi ni gharama, lakini ukiwa na mipango mizuri na malengo thabiti unaweza kufanikisha kuwa na nyumba yako iliyo bora kwa urahisi kabisa. Kila kinachopangwa kikapangika vizuri huleta matokeo mazuri. 

Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya mambo muhimu yanayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.


Itaendelea Sehemu ya 3.. 
Tembelea ukurasa huu tuelimike pamoja



Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com

Thursday, May 4, 2017

Wakandarasi 3,000 nchini wafutiwa usajili kwa kukiuka sheria.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwa miradi yote yenye thamani isiyozidi bilioni 10 wapewe Wakandarasi wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani kwani wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza uwekezaji ndani ya nchi.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo mjini DODOMA wakati anafungua mkutano wa siku Mbili wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi mwa mwaka 2017.

Makamu wa Rais amesisitiza wakandarasi hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na sheria pamoja na kumaliza kazi wanazopewa ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia ubora wa kazi na gharama zilizokubalika kwenye mikataba na sio vinginenevyo.

Makamu wa Rais amewataka wakandarasi kote nchini kuacha mara moja tabia ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wanayopewa.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa ili wathubuti kujitosa na kumudu zabuni za ujenzi kwani kwa kufanya hivyo kutaleta faida mbalimbali ikiwemo fedha watakazopata watawekeza ndani ya nchi na kutoa ajira za kutosha kwa vijana wa Kitanzania.

“Hatuwezi kuwa na Tanzania ya Viwanda huku tukiwanufaisha Makandarasi wa nje pekee ni lazima Makandarasi wa ndani wanufaike pia.”

Kuhusu madeni ya wakandarasi, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakandarasi kuwa Serikali haijawasahau na bajeti ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ambayo imepitishwa na bunge imezingatia kilio hicho cha wakandarasi.

Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kulipa madeni inayodaiwa na wakandarasi ili kujenga mahusiano mazuri ya wakandarasi hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesisitiza kuwa Wizara hiyo inaendelea kusimamia sheria na maadili kwa wakandarasi ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inayotekelezwa kote inakuwa na ubora unaotakiwa.

Waziri Profesa Mbarawa amekiri kuwa kuna baadhi ya wakandasiri ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo hivyo kujenga miradi jinsi ya kiwango hivyo ni muhimu kwa wakandarasi hao kufanya kazi kwa ubora ili waweze kuaminiwa na Serikali na kupewa kazi.

Amesema kuwa Wizara yake itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakandarasi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyotakiwa.

Naye, Msajili wa Bodi ya Wakandarasi Nchini Rhoben Nkori amesema bodi hiyo imefuta usajili wa wakandarasi 3,000 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Usajili wa Wakandarasi ya mwaka 1997 na kwa sasa bodi hiyo inawakandarasi 9,000 kote nchini.

Msajili huyo pia amesema kuwa katika kuratibu mwenendo wa kazi za makandarasi bodi hiyo ilikagua miradi 3,813 ambapo kati ya miradi hiyo miradi 2714 sawa na asilimia 71.2 haikuwa na kasoro na miradi mingine ilikuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo miradi hiyo kutofanywa na wakandarasi waliosajiliwa na kutozingatia usalama wa wafanyakazi.

Kasoro nyingine ni wakandarasi kufanya kazi zaidi ya viwango vya madaraja yao,miradi kutosajiliwa na miradi kutokuwa na bango.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
IKULU- DODOMA. 4-May-2017

Thursday, March 23, 2017

WAZIRI MBARAWA AITAKA BODI YA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI (AQRB KUJITANUA ZAIDI



Judith Ferdinand, BMG

Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiliaji Majenzi, nchini, imehimizwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi jirani katika kutoa mafunzo kwa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuendane na teknolojia ya kisasa.

Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, katika mafunzo endelevu ya 27 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi yanayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Rocky City Mall Jijini Mwanza.

Profesa Mbarawa amesema,kwa kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi, itasaidia na kuwawezesha wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi, kubadilishana uzoefu pamoja na kuendana na soko la ushindani.

Pia amewaomba wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi,wanapopata fursa katika miradi ya ujenzi watumie elimu walionayo, kwa ajili ya maslahi ya taifa sambamba na uadilifu.

“mchina na mturiki hawawezi kujua historia ya Tanzania lakini ninyi mnaijua nchi yenu, hivyo zitumieni fursa zinapojitokeza katika kubuni michoro ambayo itadumu zaidi ya miaka mia, kulingana na historia ya nchi,katika miradi ya ujenzi,” amesema Profesa Mbarawa.

Hata hivyo ameiomba, bodi hiyo kuhakikisha inasimamia na kufuata sheria namba 4 ya mwaka 2010 katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi hasa kwa wakaguzi wa majengo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza kwenye Mkutano wa mashauriano baina ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiliaji Majenzi unaofanyika kwa siku mbili kuanzia jana, katika Ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.
Kaimu Msajili wa Bodi, Albert Munuo, akizungumza kwenye mkutano huo.

Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Albert Munuo, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wataalamu na wadau wa sekta ya ujenzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kukabiliana na changamoto za utandawazi, ili kuchangia kukuza uchumi wa nchi, ambapo mpaka sasa yamewanufaisha wataalamu 5,556.
Mwenyekiti wa Bodi Dkt.Ambwene Mwakyusa, akizungumza kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti wa Bodi, Mbunifu Majengo, Dkt.Ambwene Mwakyusa, amesema, sekta hiyo inathamini jamii inayoitumikia hivyo wametoa vifaa vya maabara za sayansi, vyenye thamani ya milioni 3, ili kuhamasisha vijana wanaosoma masomo ya sayansi, kuja kusomea ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
Mwenyekiti wa Bodi Dr Ambwene Mwakyusa (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella (kulia) vifaa vya maabara.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amesema vifaa hivyo atavipeleka katika shule moja ya wasichana ya sayansi, sambamba ameishukuru bodi hiyo kupitia wataalamu wa ujenzi kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitakua chachu kwa wanafunzi kusoma masuala ya ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
Wajumbe waliohudhuria mkutano huo.

MKUTANO WA BODI YA USAJILI WA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI WAWAKUTANISHA WADAU JIJINI MWANZA


Mwenyekiti wa Bodi Mbunifu Majengo Dkt. Ambene Mwakyusa, akizungumza na wanahabari nje ya ukumbi wa mkutano wa   mashauriano kati ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi,Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashitaka,  uliofanyika Jijini Mwanza.

Judith Ferdinand, BMG
Maofisa wa Jeshi la Polisi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ambyo ni Mwanza, Kigoma, Kagera,Geita, Mara, Shinyanga, Simiyu pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka  nchini (DPP) Biswalo Mganga, wamenufaika na elimu kuhusu sheria namba 4 ya mwaka 2010, kwenye sekta ya ujenzi.

Elimu hiyo imetolewa leo katika ufunguzi wa mkutano wa   mashauriano kati ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi,Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Mashitaka,  uliofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi Mbunifu Majengo Dkt. Ambene Mwakyusa amesema, malengo ya mkutano huo ni kubadilishana uzoefu,ili kuongeza ufanisi katika kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 bila vikwazo  pamoja na kujitambulisha kwa wadau,shughuli za bodi,kuelimisha umuhimu wa kuwatumia wataalamu katika shughuli za ujenzi.

Dkt. Mwakyusa amesema, wameona watumie utaratibu wa kuelimisha Maofisa wa Jeshi la Polisi na ofisi ya DPP,ili waelewe sheria hiyo na waweze kutoa msaada wa haraka pale unapohitajika.

Pia amesema,Bodi imesajili wataalamu 1442  lakini wamaotenda kazi ni wacheche kutokana na wengine kuwa walimu vyuoni, hivyo wameona jeshi la Polisi ndio wenye uwezo wa kuwasaidia pale ujenzi unapoanza  kama umefuata taratibu za kiserikali kwa kufatilia stika na vibao vinavyobandika kama ilivyo kwa bima na leseni kwa dereva.
Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani akiongea.

Kwa upande wake  Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo Nsato Marijani ambaye ndiye  mgeni rasmi amesema, jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Bodi hiyo, katika usimamizi wa sheria pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa mtu yoyote atakayeenda kinyume na maelezo ya Sheria namba 4 ya mwaka 2010.

Aidha ameiomba, Bodi hiyo kutoa ushirikiano hasa pale ushahidi unapotakiwa kwa muda muafaka,kwani kila fani ina  wataalamu wake.

"Ikumbukwe kila fani inawataalamu wake, hivyo ushirikiano wenu katika kutoa taarifa za kitaalamu utasaidia sana wataalamu wa jeshi la Polisi kuchukua hatua syahiki kwa wakati na wepesi," alisema Marijani.

Naye DPP Mganga amesema, siyo wapelelezi wote wana taaluma ya uhandisi, hivyo kujua chanzo  cha jengo kubomoka mpaka wapate ushirikiano kutoka kwa wahandisi.

Kadhalika amesema,mtu yoyote atakayefanya kosa katika ujenzi na kuwepo kwa ushahidi atafikishwa mahakamani.
Displaying Pix.JPG

Friday, January 20, 2017

MWONGOZO WA KUCHAGUA RAMANI BORA YA NYUMBA

Ramani ya nyumba-Mali ya P.Joseph

Bila shaka kila mmoja wetu anatamani kumiliki nyumba yake,na bila shaka wale ambao wamekwisha jenga wana ndoto za kujenga tena ama kuwashauri ndugu na marafiki kujenga.

Ujenzi katika sehemu kubwa ya Tanzania haufuati taratibu na sheria za ujenzi wa makazi.Zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha hili lakini kwa leo mjadala utajikita katika namna ya kuchagua ramani bora ya nyumba

Ramani ya nyumba ni dira ambayo ni kazi ya usanifu yenye kuleta picha ya uhalisia utakaofikiwa na kutarajiwa na mteja.Kazi hii hufanywa na msanifu majengo amnbaye kwa lugha ya kiingereza huitwa Architect.

Msanifu husikiliza kwa makini matarajio ya mteja na kuiweka picha ya matarajio katika mchoro (picha).Watu wengi hudhani kazi ya Architect ni kuchora tu ramani,na ndio maana wengi hudhani ni jambo rahisi.Ukweli ni kwamba kazi yake ni kusanifu mawazo ya mteja na kuyaweka kuwa halisi.Kwa maana hiyo,hii ni fani ambayo huitaji umakini na elimu ya kutosha ili kuhakikisha anasanifu jengo ambalo litafanya wanaoishi waishi wakiupata msawazo katika joto,hewa,mwanga na wawe na furaha na kupapenda wanapoishi.

Baada bya maelezo hayo sasa tujiulize je,ramani bora inazingatia mambo gani?Ijulikane kwamba nimejaribu kupitia vigezo vitakavyomfanya kila mtu aelewe

Kwa wale ambao wana mpango wa kujenga nyumba bora za kisasa,mambo
yafuatayo ni muhimu kuyazingatia unapochagua ramani bora kwa ajili ya
nyumba yako: 
Mchoro ukionesha uhusiano uliopo kati ya sehemu moja na nyingine katika eneo (site plan).Picha ni mali ya Nyumba BoraTz


1.Izingatie maono ya mteja (client)-client imaginationikiwa na maana,mteja anapaswa kupata kile anachokipenda na alichofikiri kichwani kwake eitha kwa kuona ama kwa kutarajia 

2.Iwe na uhusiano mzuri kati ya eneo na eneo (mfano sebule na dining,dining na
jiko, sebule na vyumba.

3. Izingatie matumizi bora ya ardhi kwani ardhini gharama ( iwe na mgawanyo bora kati ya eneo linalojengwa, eneo amanafasi ya kutembea (circulating space), eneo la kijana (green
zone)-ama eneo linalopandwa miti, maua na vingine vyenye kuleta uhai.Ni lazima iepuke uwepo wa sehemu zisizo na kazi (dead space)

4.Izingatie hewa na mwanga wa kutosha katika kila eneo linalotumika,nanyumba bora huzingatia hewa na mwanga wa asili na sio artificial air.(viyoyozi)

5.Izingatie uwepo wa sitiri (privacy) –ihakikishe kila mtumiajianakuwa na uhuru wa kutosha na kuepuka muingiliano

6. Izingatie kuliendeleza eneo, lisiwe mfu kwa maana ya kuliharibu ama kuondoa vitu
vya msingi ambavyo vinafanya ardhi iwe oevu/endelevu 

7. Iwe inazingatia kufikika na matumizi kwa watu wa umri wote na maumbile yote mfano wazee,walemavu. 

8. Uzingatie uzuri- iwe inavutia (appealing to eyes) na wakati Fulani mvuto wake uwe wa kipekee ama mfano mahali inapojengwapo, iwe kioo cha eneo,utamaduni na mazingira ya eneo.

9.Izingatie matumizi bora ya maji na nishati,ikihusianisha vema sehemu zinazohitaji matumizi ya maji (wet areas) na zisizohitaji maji |(dry areas), sehemu zenye kuhitaji nishati na kutoa nishati-hot areas na hivyo kurahisisha matumizi bora ya maji na nishati.Na katika zama hizi ambayo dunia inashuhudia uhaba wa maji na nishati katika nchi za Afrika,ni vizuri wasanifu majengo waanze kufikiria majengo ambayo ni rafiki katika matumizi na rafiki wa mazingira

10.Kwa nyumba ambazo ni za wakazi wengi,ni vema ikazingatia kukuza uhusiano na undugu mfano kuwe na kibaraza (verandah ya pamoja), sehemu za mapumziko za pamoja pia,ili kuhakikisha ujamaa na ushirikiano unadumishwa

 Kumbuka nyumba
utakayoijenga ni sehemu ya kudumu ( permanent structures) hivyo ni vizuri ukifahamu mapema mambo haya kabla ya kujenga kuepuka mkanganyiko wa kisaikolojia,maamuzi na uchumi. 
N:B- Nyakati hizi watu wanapenda nyumba ambazo zinaondoa kabisa uhusiano wa kijamii mfano
ukaribu na majirani,ushirikiano-nadhani ni wakati sasa wasanifu majengo Tanzania wafikirie ni jinsi gani kinachoitwa privacy kinavyoathiri ujamaa,enzi za nyerere fikra ilikuwa watu wanaotumia apartment wapike pamoja,wafue sehemu moja,lakini kwa sasa watanzania
wanafiki tofauti na labda kwa sababu hatuna falsafa inayoliunganisha taifa

CHANZO/HATIMILIKI YA STORI: UJENZIBORATZ

Kwa maswali na maoni Wasiliana nasi UJENZIBONGO ama wasiliana na UJENZIBORATZ kupitia anwani pepe nyumbaboratz@gmail.com