WAZIRI MBARAWA AITAKA BODI YA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI (AQRB KUJITANUA ZAIDI
Judith Ferdinand, BMG
Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiliaji Majenzi, nchini, imehimizwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi jirani katika kutoa mafunzo kwa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuendane na teknolojia ya kisasa.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, katika mafunzo endelevu ya 27 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi yanayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Rocky City Mall Jijini Mwanza.
Profesa Mbarawa amesema,kwa kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi, itasaidia na kuwawezesha wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi, kubadilishana uzoefu pamoja na kuendana na soko la ushindani.
Pia amewaomba wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi,wanapopata fursa katika miradi ya ujenzi watumie elimu walionayo, kwa ajili ya maslahi ya taifa sambamba na uadilifu.
“mchina na mturiki hawawezi kujua historia ya Tanzania lakini ninyi mnaijua nchi yenu, hivyo zitumieni fursa zinapojitokeza katika kubuni michoro ambayo itadumu zaidi ya miaka mia, kulingana na historia ya nchi,katika miradi ya ujenzi,” amesema Profesa Mbarawa.
Hata hivyo ameiomba, bodi hiyo kuhakikisha inasimamia na kufuata sheria namba 4 ya mwaka 2010 katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi hasa kwa wakaguzi wa majengo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza kwenye Mkutano wa mashauriano baina ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiliaji Majenzi unaofanyika kwa siku mbili kuanzia jana, katika Ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.
Kaimu Msajili wa Bodi, Albert Munuo, akizungumza kwenye mkutano huo.
Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Albert Munuo, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wataalamu na wadau wa sekta ya ujenzi kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kukabiliana na changamoto za utandawazi, ili kuchangia kukuza uchumi wa nchi, ambapo mpaka sasa yamewanufaisha wataalamu 5,556.
Mwenyekiti wa Bodi Dkt.Ambwene Mwakyusa, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Bodi, Mbunifu Majengo, Dkt.Ambwene Mwakyusa, amesema, sekta hiyo inathamini jamii inayoitumikia hivyo wametoa vifaa vya maabara za sayansi, vyenye thamani ya milioni 3, ili kuhamasisha vijana wanaosoma masomo ya sayansi, kuja kusomea ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
Mwenyekiti wa Bodi Dr Ambwene Mwakyusa (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella (kulia) vifaa vya maabara.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amesema vifaa hivyo atavipeleka katika shule moja ya wasichana ya sayansi, sambamba ameishukuru bodi hiyo kupitia wataalamu wa ujenzi kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vitakua chachu kwa wanafunzi kusoma masuala ya ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.
Wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment