• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Showing posts with label featured. Show all posts
Showing posts with label featured. Show all posts

Thursday, February 22, 2018

Unahifadhi vipi saruji yako?


Simenti au saruji inahitajika kuhifadhiwa mahali palipo pakavu, pasiporuhusu unyevunyevu kupita kadiri iwezekanavyo. Na inashauriwa kama zimewekwa ndani ya nyumba basi mifuko yake ipangwe juu ya kichanja cha mbao na isigusane na ukuta kukwepa ubaridi wa sakafu na ukuta. Kukia na madirisha ya wastani itapendeza zaidi!

Si vyema sana kupanga mstari mmoja zaidi ya mifuko 10 mmoja juu ya mwingine. Zipange katika mtindo kwamba iliyotangulia kuhifadhiwa ndio itakayotumika kwanza kwa sababu ni rahisi sana saruji kuanza kuganda ikipata unyevunyevu. Kumbuka moja ya kipimo cha kujua ubora wa simenti ni ulaini vidoleni na kukosekana mabonge bonge yaliyoganda. 


WAKANDARASI WASIO WAZALENDO WASIPEWE KAZI NDANI YA JIJI LA DAR - NAIBU WAZIRI AWESO


Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea miundo mbinu ya maji safi na maji taka iliyopo katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi amemshukuru Naibu Waziri Aweso kwa msikamano ambao amekuwa akiufanya na wilaya yake ya kuwapa kipaumbele cha kuwatembelea mara kwa mara hali inayoamsha maendeleo zaidi.
Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji wa DAWASCO, Injinia Aron Joseph amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa vile kwasasa wamejipanga zaidi kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa walio pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiwa na mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi wakati alipofanya ziara ya kukagua miundo mbinu ya  maji kwa jiji la Dar es Salaam ambapo amejionea maendeleo mbali mbali ya ujenzi. Pichani akiwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya alipoanzia ziara hiyo.
Akikagua mradi wa Maji Taka (DEWAT) - Mlalakuwa.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akikagua mradi wa maji eneo la Makongo.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akipewa maelezo machache na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi wakati Waziri Awezo alipofanya ziara ya mradi wa maji eneo la Makongo juu ambapo ujenzi bado unaendelea.
Viongozi wa DAWASA, DAWASA pamoja na uomgozi wa serikali ya kijiji wakimsikiliza Naibu Waziri Aweso.
Wakitoka kukagua mradi wa ujenzi wa makongo juu.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi akisalimiana na Meneja wa DAWASCO-Kimara, Peter Fumbuka. Ambapo aliweza kumshukuru na kumpongeza kwa utendaji kazi wake na kumuomba achape kazi kwa bidii.
Muonekani wa ujenzi tanki la maji Makongo juu.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongea na mmoja ya wafanyakazi wa ujenzi wa mradi huo. Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG- DAR. Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amewataka wakandarasi walio wazembe wasipewe kazi kwa  vile wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo kwa kuwakosesha wananchi kupata maji kwa wakati. Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara katika wilaya ya Kinondoni ili kujionea ujenzi mbali mbali ya miundo mbinu inayoendeshwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) na Shirika la majisafi na majitaka jijini Dar es salaam (DAWASCO). Naibu Waziri Aweso amesema kuwa wakati umefika kwa wale wakandarasi wazembe kuacha kuchezea kazi wanazopewa, wafanye kazi kwa bidii ili huduma za maji zitolewe kwa wakati. "Nawaomba sana wale wakandarasi wazembe waache kuwepewa kazi maana wanachafua wilaya ya Kinondoni na Tanzania kwa ujumla maana nimetembelea miradi mbali mbali nimejionea uzembe unaofanywa na wakandarasi, ukiangalia mkandarasi kapewa hela asilimia 70 ila kazi aliyofanya ya asilimia 40 hii haikubaliki kabisa. Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi amemshukuru Naibu Waziri Aweso kwa msikamano ambao amekuwa akiufanya na wilaya yake ya kuwapa kipaumbele cha kuwatembelea mara kwa mara hali inayoamsha maendeleo zaidi. "Mimi sina mengi nitatekeleza maelekezo yote ambayo ameyatoa na nitakuwa msitari wa mbele kutoa maamuzi ya kina kwa wale makandarasi wazembe, sitamuonea aibu mtu,' amesema Naibu Waziri Aweso. Nae Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji wa DAWASCO, Injinia Aron Joseph amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa vile kwasasa wamejipanga zaidi kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa walio pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. "Tunamalizia ujenzi wa matanki makubwa ambayo tutaweza kuwasambazia wananchi wengi zaidi maji hasa walioko pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam," amesema Injinia Aron.

Friday, December 22, 2017

Huyu Ndiye Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi !? Soma hapa kufahamu kazi zao.

Mabweni ya wasichana kwenye Shule ya Sekondari Mubaba Wilayani Biharamulo yaliyojengwa kwa kutumia matofali ya kufungamana ikiwa ni sehemu ya usambazaji wa teknolojia hiyo. PICHA NA NHBRA
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa nyumba bora. Kwa miongo mingi Serikali zote kabla na baada ya uhuru zilitambua matatizo ya nyumba, umuhimu na uharaka wa kuyatatua.

Juhudi mbalimbali zimefanywa kushughulikia tatizo hilo. Ilifikiriwa kwamba ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili ni kuunda taasisi zitakazokuwa na wajibu wa kutoa mafunzo katika sekta ya nyumba ili kuboresha na kuongeza msingi wa ubora wa nyumba kutokana na tatizo kuendelea kuwapo. Serikali iliamua kuunda upya kituo cha Utafiti wa Ujenzi (BRU), kuwa Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA), yenye mamlaka ya kuendesha shughuli kibiashara.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi umejikita katika kufanya utafiti katika maeneo yafuatayo:- Mbinu za ujenzi, Vifaa vya ujenzi, Gharama za ujenzi na usanifu majengo na Uchumi na kijamii.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi ni Wakala ya Serikali iliyoanzishwa tarehe 1 septemba 2001. Wakala hii iko chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ofisi zake ziko Mwenge barabara ya Sam Nujoma Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, umbali wa mita 400 kutoka barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

KAZI ZA NHBRA
Kufanya utafiti kuhusu nyenzo za ujenzi na teknolojia ya ujenzi katika ngazi ya matumizi
Kushirikiana na Mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, Asasi zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Kijamii, Wabia wa maendeleo na watu binafsi katika kuunda na kutoa mafunzo kwa /vikosi vya ujenzi wa nyumba na uzalishaj vyenzo katika ngazi ya wananchi.
Kuhamasisha kujenga uwezo (k.v kiufundi, kifedha na kiuongozi) wa watendaji wanaohusika na maswala ya nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kuhakikisha kuwa mipango, sheria, kanuni za ujenzi, viwango na udhibiti vinalingana na uwezo, mahitaji, matakwa na matarajio ya sekta mbalimbali za wananchi
Kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya vifaa vya ujenzi vya hapa nchini na vya gharama nafuu
Kuonyesha kwa vitendo matumizi ya vifaa vya ujenzi vya nchini
Kushauri serikali na wananchi mambo yanayohusu maswala ya maendeleo ya makazi

KWA MENGI ZAIDI KUHUSU WAKALA HUYU TEMBELEA TOVUTI YA NHBRA HAPA

Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu? Soma Hapa.

Mfano wa jengo la ghorofa moja katika hatua za ubunifu. Ukiwa na mahitaji ya kufanya ubunifu wa jengo lako, wasiliana nasi tutakusaidia. 
Mara nyingi tunajenga nyumba zetu za kuishi au kwa shughuli za kiofisi/biashara kwa kutumia malighafi ya tofali. Vipande vya mawe, tofali nk huungwa moja moja juu ya jingine kwa mpishano maalumu kwa kutumia mota ya simenti na mchanga na hatimaye kupata kitu kinachoitwa ukuta wa nyumba. Aghalabu malighafi na aina ya tofali ikawa tofauti kutegemeana na sababu mbalimbali.

Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jingo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi au tuseme kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

Ukuta tunaouzungumzia hapa ni ule unaoitwa kitaalamu kama ‘masonry wall’ au ukuta wa tope ambao ni matokeo ya utaalamu wa ufundi uashi. Fundi huyu hutumia mota iliyotokana na mchanganyiko wa simenti (au chokaa, udongo nk), mchanga na maji kwa uwiano maalumu kutengeneza kiunganishi (bonding materials). Mchanganyiko huu ukiwa na utepetepe kiasi huunganisha kipande kimoja kimoja cha ama tofali, jiwe, marble, granite, vigae n.k. Tofali linaweza kuwa ama la kuchoma (brick) au yatokanayo na simenti na mchanga pekee au pamoja na kokoto (blocks). 

Yapo majengo yaliyojengwa kwa kuta za zege, mbao au malighafi nyingine. Hatutaweza kutazamia hayo. Tutajikita zaidi kuangazia masonry walls kama nilivyotambulisha awali.

Kwa sehemu kubwa ya ujenzi wetu, katika kujenga ukuta wa tope tunatumia simenti kama kemilikali unganishi muhimu zaidi. Simenti nayo ina ubora tofauti kutegemeana na matumizi. Zipo simenti za aina nyingi kwa matumizi tofauti, tutakuja kuzifahamu wakati mwingine.
Jambo la msingi sana kufahamu, ukuta wa nyumba yako utakuwa imara na wa kudumu zaidi kutegemeana na mambo makubwa matatu
1.   Aina ya ukuta unaojenga, mtindo na muundo wake (ukuta wa mawe, tofali,
2.   Ubora wa malighafi uliyotumia kulingana na hali nyingine za mazingira
3.   Ufundi sahihi katika kujenga ukuta
Kulingana na aina ya malighafi inayotumika kujenga ukuta wa tope, inaweza kuwa ni mawe, tofali n.k tunaweza kupata ubora na uimara tofauti ambao utawezesha kuwako kwa aina mbili kuu za ukuta kutokana na nafasi yake kwenye jengo.
1.   Ukuta unaobeba uzito wa jengo (Load Bearing Masonry Walls)
2.   Ukuta usiobeba uzito wa jengo (Non Load Bearing Masonry Walls)
Aina ya kwanza ya Ukuta unaobeba uzito wa jengo, hujengwa kwa kutumia matofali ya kuchoma, mawe, au matofali ya zege/mchanga. Kazi ya ukuta wa aina hii mbali na kugawanya vyumba na kutoa usiri, hufanya kazi kubwa ya kuchukua na kusafirisha uzito wa paa ama jengo jingine la juu kama ni nyumba ya ghoroa na kuupeleka kwenye msingi wa jengo na hatimaye ardhini.
Mfundi ujenzi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa msingi wa nyumba, msingi wa tofali
Kuna unafuu wa gharama kama ukijenga ghorofa kwa kutumia ukuta wa aina hii badala ya nguzo na bimu za zege, hasa kwa jingo la ghorofa moja. Jambo muhimu ni ubora wa malighafi na unene wa ukuta, bila kusahau uwiano wa urefu na unene (slanderness ratio), na huku uimara wa msingi wa jengo katika dhibiti kucheza kwa ardhi kukiwa na umuhimu mkubwa. Kwa hiyo kuta hizi hufanya kazi ya kusafirisha uzito kama mbadala nguzo za zege na nondo. Unafuu unaweza usionekane pia kama eneo unalojenga litalazimu kuwa na msingi wa jamvi nene la zege (raft foundation)
Msingi wa nyumba ukiwa tayari kwa kujenga kuta za kugawanya vyumba. Msingi wa namna hii unauwezo wa kuhimili nguvu zinazoweza kusababisha nyufa. 
Hata hivyo, kuna hatari ya kutokea nyufa kwenye kuta za namna hii kutokana na kukosekana kwa fremu ya nondo na zege ambayo husaidia kukabiliana na nguvu mgandamizo (compression force) na nguvu za utengano (tension forces). Nyufa hizi huwa hatari zaidi kama zitashuka mpaka kuvuka msingi wa jengo.

Mashaka ya jengo kutohimili kutokea kwa nyufa ni hasa wakati wa kukabiliana na matukio kama tetemeko la ardhi, mvua kubwa na upepo mkali, na bila kusahau misukumo ardhini na kuyumba kwa utulivu wa msingi wa jengo (earth pressure & differential foundation settlement). Kufikiria hatari hizi, unalazimika kujihami kwa kushirikisha wataalamu ili kuondokana na mashaka  
Uzito (loads) tunaouzungumzia hapa ni mjumuisho wa uzito wa kuta zenyewe, watu na vilivyomo ndani ya jengo, paa la jengo na nguvu ya upepo (imposed & dead loads). Vipimo vya matofali kwa viwango vyetu ni mm 450x230x150 na mm 450x230x100 ambayo kwa lugha za mafundi huzungumzia inchi 9 (tofali la kulaza), 6, 5 na 4 (tofali la kusimama). Kama utatumia tofali kwa ajili ya ukuta unaobeba uzito, ni wazi kuwa utahitajika kujenga ukuta mnene (tofali za zege za kulaza) ambao utakuwa haupungui mm 225 (inchi 9). Kuta nyingine nyembamba unaweza kuzitumia kwa ajili ya kugawanya vyumba.
Hata hivyo, unene wa ukuta utaongezeka kutegemeana na matumizi ya jengo (occupancy) sambamba na idadi ya ghorofa juu ya “floor” ya chini inayogusana na ardhi.
Kwa ujenzi wa ghorofa, ni sahihi zaidi kujenga kuta za chini kwa mtindo wa mchanganyiko wa tofali pamoja na nguzo chache za zege na nondo zilizoungwa na bimu kuzunguka jengo zima, zikiunganishwa na slabu. Wahandisi wabunifu majengo (Structural/Civil Engineers) wanaweza kukusaidia kupata vipimo sahihi.
Ujenzi wa linta ambayo pia inatumika kuunganisha nyumba nzima kama ring beam. Ni aina ya ujenzi wa kawaida mitaani kwetu na matokeo huwa bora kama mafundi wataalamu watatumika. 
Aina ya pili, Ukuta usiobeba uzito wa jengo ni kuta ambazo kazi yake kubwa ni kugawa vyumba (partition walls) kwa ajili ya usiri na kulinda waliomo ndani dhidi ya hatari za nje. Katika jengo lenye kuta za namna hii kunakuwa na kuta nyingine ama nguzo ambazo ni maalumu kwa ajili ya kusafirisha uzito, mathalani maghorofa mengi tunayoyaona yakijengwa mijini. Kuta hizi hazilazimiki kuwa nene sana na ndio maana unaweza kujenga ukuta wa inchi 4 tu kwa ajili ya kugawanya maeneo ya choo na bafu. 
Mfano wa nyumba ya kuishi iliyokamilika . PICHA ZOTE NI HATI MILIKI YA BLOGU HII

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KATIKA UJENZI WETU? - PART V: FAHAMU HASARA ZINAZOKUKABILI

KARIBU KATIKA SEMEHU YA MWISHO YA MAKALA YETU INAYOHOJI “TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?”. 

Sehemu iliyopita tuliweza kuwafahamu baadhi ya wataalamu muhimu katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, halikadhalika miradi mingine kama ujenzi wa barabara, madaraja na mabwawa ya maji.


Katika kuhitimisha makala yetu hii, leo tutahitimisha kwa kauangalia baadhi ya faida tunazozikosa kwa kutowashirikisha wataalamu katika kufanya miradi yetu ya ujenzi, hasa kwa nyumba zetu za makazi.

Kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, nchi yetu pia imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa nyumba na makazi bora ya watu kuishi. Watu wengi wamejikuta wakijenga kiholela kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na mamlaka za miji kutowajibika ipasavyo kusaidia jamii kuwa na makazi bora na yanayokidhi mahitaji ya sasa na baadae.


Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi. Wataalamu wanaposhirikishwa Serikali yetu inakuwa na uhakika kuwa mipango, sheria, kanuni za ujenzi, na viwango vya ujenzi vinazingatiwa ili kuiwesesha kupanga mipango ya kuhudumia jamii yote kwa mahitaji kama miundombinu ya umeme, kukabili majanga ya moto, maji safi na maji taka.

Kama tulivyofahamu awali, Ujenzi ni teknolojia ya kujenga nyumba, viwanda, barabara, daraja au hata miji. Ni kazi inayohusisha wataalamu wengi na ngazi mbalimbali ya kupanga na kutekeleza. Majengo madogo yanajengwa na watu binfasi kufuatana na maarifa yao bila kuhitaji mpangilio mkubwa kwa kutumia mafundi wenye ujuzi kiasi kutoka vyuo vya ufundi au waliojifunza kupitia maarifa ya watu waliowatangulia. Mamlaka ya Mji husika hulazimika kushirikishwa ili kuruhusu mpangilio unaoruhusiwa kisheria.
Miradi mikubwa ya ujenzi huhitaji mpangilio maalumu na ni lazima kwa mwenye jengo kutafuta kwanza ushauri wa wataalamu, ambao watasimamia kazi yake kuanzia mwanzo wa ubunifu mpaka kukamilika kwa ujenzi.

Mhadisi na msanifu majengo watachora michoro ya jengo. Wataalamu wakadiriaji gharama watakadiria mahitaji ya vifaa na gharama za jengo, usimamizi na malipo mengine ya vibali. Watatafutwa wakandarasi ambao watakaa na kupanga mahitaji ya muda, pesa, wafanyakazi na mashine zitakazotumika.
Kisha ujenzi utasimamiwa na mhandisi na msanifu wa jengo pamoja na wataalamu wengine ambao wamesajiliwa na kupewa vibali vya kufanya kazi hiyo na mamlaka husika. Mamlaka ya mji husika nayo itahusika na watu wake wa ardhi na mipango miji. 

Yote yakizingatiwa na kutekelezwa kwa usahihi na uaminifu hitimisho ni kupata jengo zuri na lenye thamani kulingana na gharama zilizotumika, ambayo ni faida kwa mmiliki wa jengo. 

Kwahiyo, ukiachana na utambulisho huo mpana kuhusu majengo makubwa tufikirie sasa kwa udogo wa majenzi yetu ya makazi ya kuishi kwa kuzingatia sharia na taratibu za miji mbalimbali. Ingawa kwa sehemu kubwa nchi yetu ina shida ya maeneo kutopimwa na kutambulika matumizi halali ya ardhi, lakini bado kuna changamoto ya watu wengi kupuuza taratibu zilizopo kwa sababu za kawaida sana.

Kujenga nyumba kunahitaji umakini mkubwa sana na wakati mwingine mwenye kujenga anahitajika kuwepo eneo la ujenzi mara kwa mara na ikibidi kushiriki katika hatua zote za kuanza wazo la ujenzi mpaka kukamilika kwa nyumba yake. Ukaribu huu unakusaidia kupata nyumba na makazi ya ndoto yako.

Kwa kuangalia msingi kwamba atakayeitumia ni wewe na familia yako, ni wazi kuwa unahitaji kuhakikisha unapata makazi yaliyo bora na yatakayodumu kwa muda mrefu. Pengine, yawezekana ukawa huna kabisa ufahamu wowote kuhusu namna ya kufanya ujenzi wako na kuwa vile unavyotamani. Pengo hilo linazibwa na wataalamu wa ujenzi kama ukiamua kuwashirikisha. Hawa watakusaidia kufanya ndoto yako kuwa kweli na kukuongoza kupata bidhaa za gharama nafuu na bora. 


Mtaani kuna mafundi wengi wazuri na wazoefu lakini wana dosari ya kujenga kwa mazoea pekee na kukariri kazi nyingine zilizopita na ndio maana ni rahisi kukuta mitindo ya nyumba iliyojengwa na fundi mmoja ikifanana kwa mambo mengi. Hali itakuwa tofauti kama mafundi hawa watashirikisha ujuzi wao na utaalamu mwingine ili kuweza kufanikisha kile anachohitaji mwenye kutaka nyumba.

Katika kunogesha mada yetu hii, nadhani ni vyema pia tukafahamishana na kujikumbusha baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kujenga nyumba yako kwa upya kabisa, na hasa ikiwa ndio mara yako ya kwanza kufanya ujenzi:


1.    Kuwa na dondoo kadhaa kuhusu gharama za ujenzi
Kabla ya kuanza ujenzi, fanya tathmini binafsi ili uweze kujua kama unaweza kumudu gaharama ya nyumba unayotaka kwa ukubwa gani kwa muda kiasi gani. Mambo mengine ni malighafi utakazotumia na zitapatikana wapi nan i wapi utajenga. Mambo yote haya ukiyatathmini kwa usahihi y1akupa muelekeo wa gharama na jinsi utakavyofanikisha ujenzi wako.

2.    Fahamu aina ya mafundi na wataalamu utakaowahitaji kukujengea
Ni muhimu pia kuwajua mafundi wazuri na unafuu wao wa gharama sambamba na wataalamu washauri na wachora ramani watakaokusaidia hasa kwa miradi mikubwa. Endapo utataka kuuza kazi zote kwa mtu mmoja ni muhimu pia kuwafahmu uwezo wake, gharama, ubora wa kazi afanyazo na uaminifu wake kwenye kazi na usimamizi wa fedha.

3.    Fahamu kuhusu taratibu za kisheria zinazosimamia maswala ya ujenzi katika eneo la Mji unaoishi
Kila mamlaka ya Mji inataratibu zake za upangaji mandhari ya mji wake kwa makazi na matumizi ya umma, viwanda n.k. Ni muhimu kufahamu mamalaka ya eneo husika imepanga matumizi gani kwenye eneo unalotaka kujenga. Idara ya ardhi itathibitisha umiliki wa eneo na uhalali wa matumizi tarajiwa na idara ya ujenzi watakagua michoro kama inakindhi viwango vya ubora na miundombinu ya maji taka na kutoa Kibali cha Ujenzi. Kwa tatizo la kuwa na maeneo mengi yasiyopimwa, Mabaraza ya Ardhi ya Kata husaidia kutoa uthibitisho wa matumizi ya eneo husika kama halijapimwa. Fuata masharti ya ujenzi kuepuka usumbufu usio na sababu.

4.    Fikiria mahitaji halisi na muundo wa nyumba unayoitaka
Kama ni nyumba ya familia au biashara, ni wewe ndiye unayejua mahitaji halisi kwa maana ya idadi ya vyumba, matumizi yake na pengine muonekano unaoutamani. Mbunifu majengo anaweza kukuongoza kupata mchoro mzuri kwa viwango vya nafasi kitaalamu ili kusitokee nyumba ikajenga halafu ikaonekana chumba Fulani ni kikubwa sana au kimepungua. Kwa hiyo katika hatua hii unafanya kama vile ndio uko ndani ya nyumba na unaigiza akilini kama ndio unaona maisha halisi ndani ya nyumba, unaona swichi za umeme na taa zilipo na kukuhudumia vizuri.

5.    Fikiria mandhari ya nje ya nyumba
Watu wengi hasa wanaokopi ramani tu na kujenga wanakosa umaridadi wa mandhari ya nje. Ni vyema sana ukajenga kufuatana na muundo wa kiwanja chako. Kwa hiyo, utaona umuhimu wa kupata mtaalamu akakutengenezea ramani itakayoendana na eneo lako. Kuna mambo ya kuzingatia kama sehemu ya kuegesha gari, kuanikia nguo na shughuli za uwani, mahali pa kupumzikia na watoto kucheza, na namna ya kuingia nyumbani kwako bila kusahau sehemu sahihi ya kuweka mifumo ya maji taka kwa urahisi wa gari la maji taka kufika hasa kama hakuna mfumo wa majai taka wa umma kuweza kuunganisha.
Mandhari ya nje inahusisha ukijani wa miti na maua. Ni muhimu pia kuwazia mambo kama hayo pia.

6.    Fikiria maisha marefu ya jengo lako
Yawezekana unapanga kujenga nyumba yako eneo fulani ukitaraji litakuwa makazi yako ya kudumu. Lakini, uhalisia ni kuwa maisha nayo hubadilika kadiri majukumu ya kiuchumi yanavyobadilika. Ni nyema ukafikiria kuwa na jengo lisilohitaji ukarabati mkubwa kisi cha kuongeza gharama za maboresho huko baadae endapo itatokeo ukalazimika kufanya biashara. Aina ya malighafi utakayotumia pia ina nafasi kubwa kwenye gharama za ukarabati muda baada ya muda.

7.    Fanya uchaguzi mzuri wa finishing materials na decorations

Ni kawaida kukuta nyumba imebuniwa vizuri lakini finishing touch yake na rangi vinafanya iwe ya muonekano usiopendeza. Tumia muda mwingi kupeleleza huku ukishauriana na wataalamu na kusoma majarida mbalimbali ili uweze kupata chaguo sahihi la rangi na malighafi nyingine za kumba nyumba yako kwa ndani na nje. Kuna rangi maalumu kwa ndani pekee na nyingine kwa nje pekee. Halikadhalika madhari ya majirani zako na ukijani uliokuzunguka navyo vinaathiri aina ya urembo wa nyumba. Muhimu kushirikisha wataalamu wa kazi husika kukusaidia mawazo na ushauri.




Kwa hiyo, usiposhirikisha wataalamu katika ujenzi wako unakosa faida zifuatazo:

1.       Kupata aina ya nyumba inayojitosheleza kuendana na matamanio yako. Katika ubunifu kuna mambo usiyoyajua ambayo wataalamu watakusaidia kuyafahamu, matahali uhusiano wa uelekeo wa upepo na milango/madirisha (cross ventilation) n.k. Ukimshirikisha mbunifu akayaweka mawazo yako katika mchoro, atakusaidia kupata picha halisi ya jinsi nyumba yako itakavyokuwa nah ii itakuongezea hamasa ya kukamilisha ndoto yako.



2.       Kujenga kwa ramani/michoro ya nyumba. Michoro hii itakusaidia kwa masuala mengine kama bima, kupata mkopo, kuuza n.k. Itakusaidia pia kama utahitaji kufanya maboresho ya nyumba yako na kuwa rahisi kwa fundi mwingine kujua eneo Fulani kuna nini katika nyumba.

3. Kushirikisha wataalamu kutakusaidia kujua makadirio ya gharama za ujenzi wako. Makadirio haya hayatawezekana kukupa uhalisia kama hutakuwa na michoro yenye vipimo na mapendekezo ya finishing, milango, madirisha, na aina ya uezekaji wa paa. Michoro hii utaipata kwa mbunifu wa majengo endapo utamshirikisha. Ukishakuwa na michoro ya jengo lako, unaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujua ujenge namna gani kwa awamu hasa kama huna nguvu ya kujenga nyumba nzima kwa wakati mmoja. Bila michoro utajikuta unajenga na kuongeza vyumba kwa mpangilio usioshabihiana.

4.       Kushirikisha wataalamu kutakuepusha kujikuta unaingia kwenye hasara ama ya kubomolewa nyumba au kulipishwa faini zisizo za lazima kwa ama kupuuza au kutojua na kufuata utaratibu fulani.  Wakati mwingine ukipata mtaalamu mwaminifu atakusaidia kutotapeliwa na maofisa wasio waaminifu.

5.       Nafasi ya kushauriana na mtaalamu mchoraji namna ya kuongeza au kupunguza ukubwa wa jengo lako wakati ujenzi ukiendelea kwa msingi kwamba wakati wowote mawazo yanaweza kubadilika na kutamani eneo Fulani likae tofauti na lilivyobuniwa awali.

6.       Kama unataka kujenga kwenye eneo ambalo halijapimwa, mtaalamu atakusaidia kupata michoro ya jengo ambayo hata wakati wa ukaguzi wa baadae bado jengo lako litapimwa na kuonekana liko kwenye viwango na kuwa na thamani nzuri.

7.       Kushirikisha wataalamu waaminifu kutakusaidia kuepukana na wachakachuaji wakitumia kigezo cha wewe kutokuwa na ufahamu na mambo ya ujenzi. Kuna baadhi ya wajenzi si waaminifu na wanaweza kukupa hesabu kubwa za vifaa kinyume na uhalisia kwa lengo la kupata faida zaidi.
8.       Kupata kilicho bora na kwa thamani halisi ya fedha zako.

9.       Wataalamu watakusaidia kupata mbadala wa malighafi ya kutumia katika ujenzi wako huku ubora na uzuri wa kazi ukiwa vile vile kama unavyotamani. Hii ni pamoja na ushauri kuhusu malighafi zinazoweza kukuongezea gharama za ukarabati wa nyumba yako mara kwa mara.

10      Wataalamu watakusaidia kujua ukubwa wa chumba kwa matumizi tofauti kuendana na ukuaji wa teknolojia. Mathalani size ya madirisha, milango, vitasa na hata ukubwa wa maeneo kama choo na bafu ili kutosheleza vifaa utakavyonunua kwa ajili ya matumizi yako. Hata namna ya kupanga sebule kisasa kwa uwiano mzuri na sebule, jiko na veranda ni mambo ambayo utayapata kwa ushauriano mzuri na mtaalamu wa ujenzi.

11      Kuepuka hasara ya kujenga nyumba kubwa isiyosadifu mahitaji halisi kwa mhusika kutofahamu namna ya kujenga kulingana na mahitaji ya wakati gani.

Nyumba iliyojengwa kwa kubuniwa vizuri huleta raha kuishi ndani yake maana inakuwa na mpangilio unaotoa uhuru kwa kila memba wa familia kufurahia eneo lake na kuweka usiri wa mambo ya familia na wageni. Unaweza kujiuliza, kuna sababu yeyote ya msingi kwa mtu anayejenga nyumba ya milioni 65 lakini anakwepa kupata michoro kwa gharama ya shilingi laki tano tu au hata pungufu?

Kumbuka, katika ujenzi wa nyumba, kosa likishafanyika awali na nyumba kukamilika ni gharama sana kurekebisha. 


Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Blogger (http//:arusha255.blogspot.com na http//:ujenzidirect.blogspot.com)
Project QS, Proposed PPF Plaza Corridor Area Arusha
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI ? - PART II: DHANA YA MAKAZI BORA


Leo ikiwa ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hii tutaangalia kwa ukaribu zaidi dhana nzima ya nyumba bora ya binadamu ambapo madhumuni na miundo yake hutegemeana sana na hali halisi ya kidunia kwa utofauti wa sehemu moja na nyingine. Hii ni dhana tata kidogo.

Dhumuni kubwa la kuwa na nyumba ya kuishi ni kumpatia mwanadamu usiri wa mambo yake binafsi, na kumlinda dhidi ya madhara yatokananyo na hali ya hewa ya kidunia na viumbe wengine hatari kwa binadamu. Malengo mengine ni raha, ufariji na mahali pa kuendeleza uzao na kutunza afya ya mwanadamu. Nyumba ya kuishi inajitofautisha sana na mejengo mengine kama ya biashara, ofisi, masoko, hospitali, viwanda n.k. Tofauti hiyo hutegemeana sana na lengo la matumizi ya jengo husika kama nilivyoeleza hapo juu.



Ili jamii iweze kuwa na makazi bora inalazimu timu ya wataalamu mbalimbali washirikiane kwa ukaribu sana ili kufanikisha hilo. Makazi bora lazima yahusishe nyumba bora na miundombinu inayoizunguka. 

Watu wengi wanaamini kujenga nyumba ya kuishi ni jambo gumu sana katika maisha yetu na hivyo kuishia kujenga alimradi tu ni kijumba cha kujisitiri. Ni kweli ujenzi ni gharama, lakini ukiwa na mipango mizuri na malengo thabiti unaweza kufanikisha kuwa na nyumba yako iliyo bora kwa urahisi kabisa. Kila kinachopangwa kikapangika vizuri huleta matokeo mazuri. 

Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya mambo muhimu yanayofanikisha ujenzi wa nyumba bora. Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.


Itaendelea Sehemu ya 3.. 
Tembelea ukurasa huu tuelimike pamoja



Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com

TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WA NYUMBA ZETU!? - PART I

“Nyumba bora, salama na nafuu ni hitaji muhimu kwa kila familia. Bila kuwa na mahali pazuri pa kuishi, watu hawataweza kuwa sehemu ya jamii inayozalisha, watoto hawataweza kujifunza na familia hazitastawi” anaeleza   Bw Tracy Kaufman, Mtafiti wa makazi nafuu kutoka Marekani (http://www.habitat.org/how/poverty.html)


Historia ya binaamu inaelezea mabadiliko makubwa ya ukuaji katika awamu tofauti tofauti za maisha yake.  Kutoka kutembea kwa kuinama mpaka kutembea wima. Kutoka kwenye ugunduzi wa moto, zana za mawe, magome ya miti kujisitiri maungo mpaka ugunduzi wa viatu, nguo, umeme, kompyuta na njia nyingi za usafiri bila kusahau bidhaa mbalimbali za kurahisisha kazi na kujenga makazi bora yenye kila aina ya madoido. 

Binadamu wa awali kabisa wanaelezwa kuwa na utaalamu wao ambao kutokana na hali halisi ya wakati huo ni wa kiwango duni sana kama utalinganishwa kwa nyakati za sasa. Binadamu wa kale alianza kuishi kwenye mapango na mahema ya miti, akitumia nyasi na ngozi za wanyama. Nyumba hizi hazikuwa na milango wala madirisha. Baadae akajua namna ya kutengeneza nyumba za miti na udongo, na baade wakatengeneza tofali za udongo za  kuchoma kwa joto la jua.

Makazi ya kale kwa maana ya nyumba za kuishi binadamu yalihusisha matumizi ya vitu asili moja kwa moja katika ujenzi wake tofauti na sasa ambapo bidhaa ya asili inasanisiwa kupata bidhaa nyingine katika hali ya kuongeza ubora na umaridadi. Nyumba iliyokuwa maalumu kwa mifugo haikuwa tofauti sana na anayoishi binadamu na wakati mwingine ilikuwa inatengenezwa kuwezesha mifugo kama ng’ombe, kondoo na mbuzi kuishi mahali pamoja na binadamu. Wataalamu wa historia wanatueleza kuwa nyumba nyingi za kale zilijengwa kutegemeana na tamaduni na mila za jamii husika.

Kwa kadiri miaka inavyokwenda binadamu amezidi kuwa mgunduzi wa bidhaa na mbinu mbalimbali zitakazomuwezesha kukabiliana na mazingira yanayomzunguka. Ugunduzi huo unahusisha ujenzi wa nyumba bora na bidhaa zake zinazoikidhi mahitaji muhimu kumuwezesha binadamu kuishi mahali safi salama huku kukiwa na nyongeza ya urembo na umaridadi wa aina tofauti tofauti. 

Nikukaribishe katika mfululizo wa makala hii itakayohusu kuwajua wataalamu mbalimbali katika taaluma ya ujenzi, hususani ujenzi wa nyumba za kuishi binadamu sambamba na umuhimu wa mjenzi kuwashirikisha watalamu hao katika kila hatua ya ujenzi wake kwa minajili ya kupata nyumba iliyobora, nzuri, salama na yenyekukidhi mahitaji. 


Nakumbuka wakati fulani nikiwa mwanafunzi Chuo Kikuu (UCLAS) mwalimu wangu wa somo la Ujenzi alipata kuniambia tukiwa mapumziko ya chakula kuwa kila mtu ni mbumbumbu kwa jambo fulani bila kujali vyeti alivyonavyo; akimaanisha kuwa kama wewe ni mtaalamu katika taaluma fulani uliyosomea ama kujifunza lazima utakuwa mbumbumbu kwenye taaluma nyingine ambazo hujajifunza.


Akadai kuwa kadiri mtu anavyozidi kusoma jambo moja kwa undani zaidi ndivyo anavyozidi kuacha mambo mengine mengi na kubobea kwenye hilo moja pekee. Daktari aliyebobea kwenye upasuaji mkubwa kwa mfano, hawezi kuwa mjuzi kwa kiwango kile kile sawa na mtu mwingine anayeshugulika na maswala ya umeme kama taaluma yake. 

Binadamu wa sasa anajipenda mno na anatamani kufaidi maisha yake kwa kadiri awezavyo. Moja ya matamanio hayo ni makazi bora yatakayompendeza kutegemeana na uwezo wake kifedha na kiutaalamu kugharamia hilo. 

Lakini wapo watu wengi ambao wanatamani kuwa na makazi yanayokonga roho zao bila kujali kama wana uwezo mkubwa kifedha kugharamia umaridadi wanaoutaka ama la na wapo wengine ambao wao hujenga tu kwasababu inawalazimu wajisitiri ndani ya jengo wasidhurike na mashambulizi ya wanyama wakali na ama hali ya hewa ya kidunia. 

Hawa wanaojenga tu alimradi ni jengo la wao kuishi husababishwa kuamua hivyo ama kwa kutokujua wapi na ni nani wamuone kwa ushauri na pia uwezo mdogo kiuchumi. Baadhi pia hujenga kwa mazoea na hata mafundi wanaowatumia sehemu kubwa wanatumia uzoefu pekee.


Nyumba iliyojengwa kwa gharama kubwa sio lazima iwe nyumba bora. Kwa tafsiri rahisi nyumba bora ni ile inayokidhi mahitaji muhimu ya binadamu kuishi ndani na kujisitiri kwa usalama bila kupata madhara. Hii ni pamoja na mazingira yaliyoizunguka nyumba hiyo. 

Tutaona baadae mahitaji hayo muhimu ni yapi. Kwasasa itoshe kufahamu kuwa gharama zilizotumika kujenga makazi yetu ya uswahilini zinatosha kabisa kujenga makazi bora zaidi kwa kuhusisha wataalamu na kuacha kujenga kwa mazoea, sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo kiuchumi na kuogopa kuwashirikisha wataalamu kwa kuhofia gharama.



Itaendelea Sehemu ya pili kuelezea Dhana ya Makazi Bora
Tembelea blogu hii tuelimike pamoja




Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080seria.tw@gmail.com