TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU? - PART III: SOMA HAPA UNACHOTAKIWA KUFANYA UKITAKA KUJENGA NYUMBA KISASA
ILIPOISHIA SEHEMU YA TATU
Hebu fikiria kwamba ni wewe msomaji wangu umeamua kujiwekea mipango ya kuwa na nyumba yako nzuri, salama na bora. Katika hatua hii ni muhimu sana kujua mambo muhimu yatakayokuwezesha kutimiza ndoto yako ya kuwa na nyumba bora katika makazi bora pia. Kuna orodha ya maaandalizi muhimu yatakayofanikisha ujenzi wa nyumba bora.
Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.
Kwa upana wa makala hii sitazungumzia kwa undani sana mahitaji ya ndani ya nyumba ikiwa tayari kwa matumizi. Nitaangalia zaidi mambo makubwa ya nje ya kufanyia kazi kujiandaa ili kuwa na nyumba ama makazi yaliyobora.
Mfano wa ramani ya nyumba |
Jambo la kuanza nalo ni kufikiria mahali sahihi utakapo jenga nyumba yako.
Mahali unapotamani kujenga makazi yako yanahusika kuamua aina ya nyumba yako hapo baadae. Inaweza kuwa unawazia kujenga nje ya mji au mjini. Eneo unalotamani kujenga nyumba ya kuishi linaweza kuwa ni eneo lililopimwa ama bado halijapiwa. Ardhi yake ni ya mabonde na milima ama tambarare. Utaangalia matumizi mengine ya eneo hilo na miundombinu yake. Pengine ni eneo jirani na viwanda n.k. Hata udongo na hali ya hewa ya eneo husika inanafasi yake, pengine ni ufukweni mwa bahari.
Kumbuka, uamuzi wa eneo la kujenga unaweza kuashiria uharaka wa kukamilisha kujenga nyumba yako kwasababu kwa mfano kama unatazamia kujenga katika eneo la katikati ya mji huwa ni gharama kubwa na hata upatikanaji wake ni wa taabu kidogo. Ikiwa ni eneo la mjini kuna ugumu wake pia kwa mfano kupata kibali cha kujenga.Miji mingine kwa mfano Jiji letu la Arusha halitoi vibali kwa ujenzi wa nyumba ndogo zisizo za ghorofa kwa maeneo ya katikati ya Jiji.
Kwa eneo ambalo limekwishajengwa na kupangwa kuwa eneo la makazi huwa ni rahisi zaidi hata kupata kibali cha ujenzi wa makazi na miundombinu yake huwa maalumu kwa makazi ya watu.
Jambo la pili kujiandaa nalo ni pesa za kugharamia ujenzi husika hata kwa kuanzia tu na wataalamu utakaowatumia bila kusahahu gharama za mamlaka ya mji au mtaa husika na tozo za vibali mbalimbali vya huduma na ruhusa. Ni vizuri kupanga kiasi cha fedha ulichonacho au kujikusanyia kitakufikisha wapi katika ujenzi wako. Itakuwa gharama zaidi kama utaamua kupata eneo na kujenga hapo hao, ingawa kwa baadhi wanaweza.
Lakini pia kwa kujikusanyia pesa kidogokidogo na kuzitunza kwa malengo ya ujenzi unaweza kufanya ujenzi wako ulio katika ubora mzuri. Kuna wataalamu washauri wa maswala ya gharama za ujenzi kabla, baada na wakati wa ujenzi wanaweza kusaidia. Kitaalamu wanaitwa Quantity Surveyors ama Cost Engineers kwa baadhi ya nchi kama Uingereza.
Jengo kwa matumizi ya kuishi likiwa katika hatua za uezekaji
|
Kwa hiyo, kama nilivyoeleza kuwa ukishakuwa umejiandaa unamtafuta mtaalamu mbunifu wa majengo, kitaalamu anaitwa Architect (tutajifunza baadae nafasi yake katika ujenzi pamoja na wasaidizi wake). Unampatia mahitaji yako halisi na namna unavyotamani nyumba yako iwe, nae kwa utaalamu wake atakushauri namna nzuri ya kuyapanga mahitaji yako hayo na kuyaweka kwenye mchoro ambao fundi anaweza kuutumia kujenga nyumba yako.
Mtaalamu huyo atayaunganisha mahitaji yako na kuyapanga kitaalamu ili kuweza kupata jengo ambalo litakuwa na sifa za mahitaji ya nyumba bora. Mifano ya mahihaji muhimu ni madirisha yanayoruhusu hewa kwa kupangilia uhusiano mzuri na milango kupata kitu kinachoitwa kitaalamu kama cross ventilation. Pia mpangilio wa vyumba, sehemu ya chakula, jiko na vyoo bila kusahau baraza na korido.
Utoaji na uingizaji wa maji masafi na machafu una umuhimu wake pia na halikadhalika namna sebule itakavyokaa na kutumiwa na wageni na watu watakaokuwa wanaishi kwenye hiyo nyumba bila kusahau maliwato kwa mgeni. Pia maswala ya usalama wa jengo dhidi ya hatari ya moto na hata mpangilio wa madirisha kuoanish na uelekeo wa upepo.
Ni vizuri pia tukifahamishana kuwa kwa mujibu wa sheria zetu za ujenzi hapa nchini kuhusu nyumba za kuishi (residential houses), endapo mtu anajenga jengo la ghorofa analazimika kumtafuta injinia amsaidie kumuandalia mchoro utakaohusu uimara wa jeingo kwa maana kwamba utakuwa ni mchoro unaoonesha namna nondo zitakavyojipanga, idadi na saizi yake, bila kusahahu ubora wa zege na mambo mengine yahusuyo uimara wa jingo lako.
Sasa kama utakuwa unawazia jengo la namna hiyo ni lazima kisheria kutafuta Structural Engineer akusaidie kuandaa michoro mingine.
Hatua ya nne, baada ya kuwa na mchoro wako utahitaji kujua makisio ya gharama halisi za mradi ama kwa kujenga mpaka kumaliza ama kwa awamu tofauti. Mtaalamu mkadiriaji majenzi niliyemueleza hapo awali kuwa anatambulika kitaaluma kama Quantity Surveyor/Cost Engineer atahitajika kufanya hesabu za makadirio ya gharama ili uweze kujua namna halisi ya kujipanga kutegemeana na mchoro ulivyo na jinsi utakavyokuwa umechagua material gani za kutumia kwa kushauriana na kitaalamu. QS huyu atakusaidia kubajeti vizuri na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima au bidhaa bora na rahisi lakini lengo likibaki kupata nyumba bora. Wakati mwingine hata fundi mzoefu anaweza kukusaidia.
Hatua ya tano. Mpaka hapo utakuwa umeshakamilisha hatua za awali muhimu kabla ya kuanza mradi wako wa ujenzi. Sasa unaweza kuwatafuta wataalamu wajenzi kwa maana ya kampuni au mafundi binafsi wenye uelewa mzuri wa kutafsiri michoro ya ujenzi ili muweze kukubaliana na kuanza kazi ya ujenzi tukichukulia kuwa eneo tayari lipo, limehakikiwa na kuonekana liko tayari kwa ujenzi na udongo wake ukiwa umeshaoanishwa na aina ya msingi wa nyumba utakavyokuwa.
nembo ya AQRB |
Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 ya AQRB, Bodi ya Wakadiria Majenzi na Wabunifu wa Majengo inahimiza matumizi ya kampuni za wakandarasi zilizosajiliwa kufanya ujenzi kwa kufuata mchanganuo ufuatao
· Ujenzi wa majengo yoyote ya ghorofa ya ukubwa na thamani yeyote
· Majenzi yote ya makazi yanayozidi thamani ya sh milioni 50 na ujenzi wake unahitaji uhandisi (structural inputs)
· Ujenzi wa majengo yote ya umma kama shule, hospitali, masoko, makanisa, misikiti, kumbi za starehe n.k
· Ujenzi wa majengo ya viwanda, maghala n.k
Kwa hiyo utaona ni namna gani sheria inajaribu kumsaidia mjenzi kupata kilicho bora kwa kutumia wataalamu. Ni ukweli kwamba idadi kubwa ya watanzania hawana uwezo wa kujenga kwa kutumia wataalamu na hata kiwango cha nyumba yenye thamani ya milioni 50 wakati wa kuanza ujenzi hawana. Baadhi wanazikwepa kampuni wakijaribu kuokoa gharama za ziada ili zitumike kwenye ujenzi wenyewe.
Sehemu ya kazi za kweka urembo wa nyumba kwa ndani. Kazi ya SeriaMjenzi |
Unaweza kuepuka kutumia kampuni kujenga lakini kama uliwashirikisha wataalamu kuandaa wazo la ujenzi wako kitaalamu unaweza kumtumia fundi yeyote mjuzi akakusaidia kujenga kwa gharama ambazo mara nyingi ni pungufu kidogo ya gharama za makampuni. Mtaani tunao mafundi wengi na wataalamu baadhi wakiwa wamehudhuria mafunzo rasmi chuoni na wengine wakijifunzia tu mtaani na kujikusanyia uzoefu. Wote ni wataalamu.
Itaendelea Sehemu ya nne, ambapo tutaweza kuwajua wataalamu mbalimbali wanaohusikana ujenzi.
Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080 seria.tw@gmail.com
No comments:
Post a Comment