TUNAKOSA NINI TUSIPOTUMIA WATAALAMU WAUJENZI? - PART IV: WAJUE WATAALAMU KWENYE SEKTA YA UJENZI
KARIBU TENA KWENYE MAKALA YETU YA 'TUNAKOSA NINI TUSIPOWATUMIA WATAALAMU KWENYE UJENZI WETU?' SEHEMU YA NNE
Tuwajue wataalamu wetu wa ujenzi.
Ndugu msomaji wangu, nikushirikishe sasa kuweza
kuwafahamu wataalamu mbalimbali walio na taaluma anuai kuhusiana na masuala ya
ujenzi wa majumba. Ni jambo jema kufahamu kuwa wataalamu wote hawa wamesomeshwa
na vyuo vyetu vya hapa nchini. Hii ni kusema kwamba utaalamu wa ujenzi ni wetu
wenyewe ingawa kwa upande wa bidhaa za ujenzi bado tunategemea sehemu ya utaalamu na ubunifu wa nje
ya nchi.
Sote tu mashahidi wa namna taifa la China na raia wake walivyosambaa
barani Afrika na Tanzania ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa zao za ujenzi.
Wataalamu
wengi wa ujenzi nchini wanapata mafunzo yao kwenye taasisi za elumu ya juu kama
ATC (Arusha Technical College), MIST (Mbeya Institute of Science and
Technology), DIT (Dar es Salaam Institute of Science and Technology), ARU
(Ardhi University), CoET n.k; vituo vya mafunzo vya VETA na baadhi ya shule za
ufundi kama “Moshi Tech” n.k.
Shughuli nzima ya ujenzi nchini inasimamiwa na Serikali kupitia Wizara husika na mamlaka zake; na pia Bodi mbalimbali kama Bodi ya maiinjinia-ERB, Bodi ya wakandarasi-CRB, Bodi ya Wakadiriaji Majenzi na Wabunifu Majengo-AQRB bila kuwasahau Baraza la Ujenzi la Taifa-NCC na kwa miundombinu wanaongezeka wakala wa barabara nchini – TANROADS na TARURA.
Ni kina
nani na yapi majukumu ya wataalamu (proffesionals)
kwenye “kiwanda” cha ujenzi nchini?
Hili ni swali zuri na muhimu ambalo
litatuongoza kuwafahamu na kuyafahamu majukumu yao katika ustawi wa sekta ya
ujenzi nchini. Baadhi hatuwaoni kwenye ujenzi wa majumba yetu ya kuishi lakini
wanafanya kazi katika maeneo mengine makubwa zaidi.
Tuanze na timu
ya wataalamu wanaotambulika kitaaluma kama Geotechnic
Engineers (GE). Mpangilio wa masimulizi hautafuata ubora ama umuhimu wa
kila taaluma. GE, hawa ni wataalamu wanaohusika na kuchambua sifa za udongo
kama sehemu ya taaluma ya uinjia wa majenzi ya barabara, madaraja, mifereji,
mabwawa na majengo makubwa, ambapo taaluma hiyo inajulikana kama Civil Engineering.
Mhandisi udongo/Geotechnic Engineer
Huyu anafanya kupembua sifa za udongo za kimuonekano, kikemikali ambazo zinaweza kuathiri mradi wa ujenzi na namna jingo linavyoweza kukabiliana na matetemeko ya ardhi na majanga mengine na hatimaye kupata muafaka wa aina ya msingi (foundation) wa jengo, daraja n.k unavyopaswa kuwa.
Land Surveyor/mpima ardhi.
Hili ni kundi linguine la wataalamu wa
maswala ya kupima ardhi na mara nyingi wanakuwa sehemu ya utendaji wa
kiSerikali. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na Halmashauri za Miji na Majiji
ndipo mahali hasa unaweza kuwakuta wataalamu hawa kama maafisa ardhi. Hata
hivyo zipo kampuni binafsi pia zinazotoa huduma za upimaji ardhi na wataalamu
hawa wanapatikana huko pia.
Kazi yao
kubwa katika sekta ya ujenzi kama wataalamu wa kwanza kabisa kufanya kazi eneo
la ujenzi kabla ya wengine ni kutambua mipaka ya eneo la ujenzi, kutambua ukubwa
wa eneo, kuweka na kukagua beacons, bila kusahau kutambua kiasi cha mbonyeo au
mwinuko wa ardhi inayotarajiwa kujengwa. Kazi za taalumu hii zimekuwa
zikitolewa zaidi kwa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam.
Mbunifu majengo/Architect
Huyu ndie mtaalamu aliyefuzu mafunzo na kusajiliwa kubuni michoro ya jengo kwa kubadilisha mawazo (concepts) ya mradi fulani na kuyaweka kwenye michoro na muonekano wa uhalisia wa jingo litakavyokuwa likishajengwa. Hufanya kutafsiri mahitaji ya anayetaka kujenga na kuyaweka kwenye uhalisia kwa namna ya kumuwezesha mjenzi kufanya ujenzi. Hutengeneza taswira ya muonekano wa jengo na mpangilio wa mambo mengine.
Kabla ya
kuanza ujenzi, mbunifu huyu anatakiwa kuchora mchoro wa jingo husika na ndipo
ujenzi uanze. Ni rahisi kukosa mwelekeo wa ujenzi kama utaanza kazi ua ujenzi
ukiwa huna mchoro unaokuongoza.
Taaluma ya
ubunifu majengo ama Architecture kama taaluma nyingine nayo ina mgawanyo wa utaalamu
kwa maana ya ubunifu wa ndani ‘interior design’, mpangilio wan je ya jingo na
vitu nama bustani na sehemu za maegesho ‘landscaping’ na ubunifu wenyewe wa
jango zima na umaridadi wake wan je na mgawanyo wa vyumba na maeneo huru ndani.
Bado ni vyuo vikuu vichache ambavyo vinatoa mafunzo ya taaluma hii hapa nchini
ambapi pia kuna mafunzo ya wasaidizi kwa ngazi za chini ambao nao hufanya kazi
za uchoraji pamoja, kitaalamu hutambulika kama draughtsmen.
Wahandisi/(Civil and Structural Engineers)
Baada ya
Mbunifu majengo kumaliza kazi ya kuandaa michoro yake mhadisi ndiye mtaalamu wa
pili kuweka utaalamu wake. Mara nyingi kumekuwapo na mchanganyo wa uhandisi na
ukandarasi. Kuweka hili sawa kupitia makala hii, ifahamike kuwa mhandisi ni
mtaalamu mbunifu wa uimara wa jingo na mkandarasi ni mjenzi wa jingo akifanyika
kazi vilivyobuniwa na wahandisi na wabunifu majengo. Mkandarasi anaweza kuwa
aidha mtu binafsi au kampuni iliyosajiliwa kufanya kazi ya ujenzi kwa kiwango
fulani.
Sasa huyu
anayejulikana kama Structural Engineer ndiye Mhandisi hasa na huwajibika kwa
uhandisi wa ubora na uimara wa jengo kwa kufanya mahesabu ya uimara (strength), uzito, nguvu na namna
vitakavyokabiliana bila kuleta madhara kwenye jengo linalotarajiwa kujengwa.
Ni jukumu
la mhandisi huyu kuandaa michoro ya uimara wa jengo kwa maana ya namna nondo na
zege na hata vyuma vingine vitakavyokuwa na ukubwa wake kwa maeneo kama nguzo (column), msingi (foundation) bimu (beams),
kuta, ngazi za ghorofa na slabu (slabs)
kwa upande wa majumba. Halikadhalika huandaa michoro kwa ajili ya madaraja,
nguzo kubwa, mabwawa n.k.
Wakati wa
ujenzi anakagua pia ubora wa bidhaa (materials)
zinazotumika na namna nondo na zege zinavyotengenezwa kama vinafikia ubora
unaotakiwa kama alivyobuni kimahesabu.
Inapotokea
jengo limeanguka kwasababu zisizotokana na nguvu za asili kama mtetemeko ya
ardhi na milipuko ya bomu kwa mfano, mhandisi ndiye hupewa majukumu ya
kuchunguza sababu za kihandisi zilizopelekea hitilafu iliyosabababisha jengo
kuanguka kama iivyotokea maeneo ya Kisutu Jijini Dar es Salaam miaka michache
iliyopita.
Mkadiriaji Majenzi/Quantity Surveyor(QS)
Mkadiriaji
majenzi kwa baadhi ya nchi hutambulika kama Cost
Engineer. Ni sawa na kusema ndiye mhasibu kwenye sekta ya ujenzi.
Majukumu
makubwa ya mkadiriaji majenzi ni kufanya makadirio ya gharama za mradi wa
ujenzi. Makadirio hufanyika wakati wa kubuni wazo la mradi, wakati wa ujenzi na
wakati wa kuandaa mkataba wa ujenzi kwa ajili ya kupatana na mkandarasi.
Makadirio haya hufanyika kimahesabu kwa majengo mapya au yanayokarabatiwa ama
kuboreshwa.
Mkadiriaji
majenzi hufanya kazi katika sekta zote mpaka kwenye uchimbaji madini,
miundombinu, na majengo ya nyumba za kuishi na majengo makubwa ya viwanda na
taasisi za umma au jumuia. Ili kuweza kukamilisha kazi yake hulazimika kutafuta
kiasi (quantity) cha visaidizi kama nguvu kazi, zana za kazi, bidhaa za ujenzi
n.k.
Katika
miradi mkubwa ya ujenzi QS ndiye huwajibika kufanya yafuatayo
a. Kufanya
makadirio ya bajeti ya mradi
b. Kuchanganua
madhara yanayoweza kujitokeza kwa kubadilisha dizaini ya jengo na bajeti yako
c. Kuandaa
BOQ (kitabu cha makadirio ya gharama na kiwango cha kazi) ambayo husaidia
wakati wa kumtafuta mkandarasi wa kutekeleza ujenzi
d. Kuandaa
kamabrasha ya tenda za ujenzi na kusimamia zoezi zima
e. Kuhakiki
kazi ya ujenzi iliyofanyika na kuipa thamani yake kwa ajili ya kuruhusu malipo
kufanyika kwa mkandarasi kwa kiwango cha kazi alichofanya.
f. Kusimamia
mabadiliko yate ya kimuundo na kiujenzi na hata gharama wakati ujenzi
unaendelea tofauti na kilichobuniwa awali.
g. Kuandaa
hesabu za malipo ya mwisho kwa makandarasi ilikwa mmradi umekamilika kwa namna
taratibu na sharia za ujenzi zinavyoelekeza na majukumu mengine.
Mjenzi/Builder
Mjenzi au builder husoma na kuielewa michoro yote
na maelekezo mengine na kuangalia inaoana vipi. Anachanganua uwezekano wa jengo
kujengeka na namna litakavyotunzika kama lilivyobuniwa. Ni sawa na kusema huyu
ni mhakiki ingawa kwa hapa kwetu ni nadra kuwakuta wataalamu hawa kwa majukumu
haya kama mtaalamu wa pembeni. Mara nyingi wanakuwa kama sehemu ya wakandarasi.
Mhandisi wa Huduma za Jengo/(Building Service Engineer)
Kwa
kawaida jengo halikamiliki kwa kuwa na ubunifu wa jengo lenyewe tu na uimara
wake. Kwasababu kila jengo ni maalumu kwa matumizi Fulani huwa kunakuwa na
huduma muhimu za kuwawezesha watumiaji wa jengo hilo kuweza kulitumia. Huduma
tunazozizungumzia hapa ni kama mfumo wa maji safi na machafu, mfumo wa umeme,
mfumo wa mawasiliano ya kitekinohama nausalama.
Huduma
nyingine ni mfumo wa kukabiliana na hitilafu ya moto, mfumo wa usafirishaji
kwenda na kutoka ghorofani (vertical
transportation) na mfumo wa kuweka hali ya ujoto au baridi na kutoa hewa
chafu nje ya jengo (mechanical
ventilation)
Huduma
zote hizi hubuniwa na kusimamiwa na mtaalamu anayetambulika kama Mhandisi wa
Huduma za Jengo (Services Engineer)
akifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wataalamu wengine ambao
nimeshawaelezea hapo awali.
Mafundi au Artisans
Hawa ndio
watu wanaofanya kazi kwa vitendo eneo la ujenzi wakiwa na ujuzi wa namna
tofauti tofauti. Mafundi mchundo (Technicians) wanaingia kundi hili pia wakiwa
na utaalamu (skills) kwa maeneo tofauti tofauti ya ujenzi kama ufundi seremala,
ufundi chuma, ufundi tope (masonry) n.k.
Wataalamu Washauri (The Consultants)
Kila mradi
uliofuata taratibu za ujenzi kwa mujibu wa sharia zetu unalazimika kuwa na timu
ya washauri wataalamu kwa msingi kwamba mmiliki (Client) anayetaka kufanya maradi wa ujenzi anaweza kuwa sio
mtaalamu wa maswala ya ujenzi na hata akama atakuwa na utaalamu hataweza kuwa
na uelewa wa kila kitu. Hivyo inamlazimu kuwa na timu ya watu watakaomshauri na
kumsaidia kufanikisha mradi wake ili aweze kupata thamani halisi ya
alichowekeza na kilichojengwa kama vinawiana.
Wataalamu
Washauri ni mjumuiko wa wataalamu wote niliowaeleza hapo mwanzo, wataalamu kama
Mbunifu Majengo, Mkadiriaji majenzi, Wahandisi wa jengo na Huduma, na wataalamu
wengine.
Hawa
washauri wanatakiwa kushirikishwa kuanzia mwanzo kabisa wazo la mradi linapoanza
kwsasababu kimajukumu washauri hawa ndio huchukua nafasi ya mmiliki au tajiri
wa mradi na kumuwakilisha katika maswala ya kitaalamu.
Mkandarasi/Building Contractor
Mkandarasi
kwa lugha rahisi anahesabika kuwa ni mkusanyiko wa timu ya wajuzi wa masuala ya
ujanzi pamoja ambao wao majukumu makubwa ni kubadilisha michoro na kuifanya
kuwa uhalisia wa kilichobuniwa. Mkandarasi huwajibika kukusanya vifaa na bidhaa
za ujenzi na kutumia utaalamu wa watu wake kufanikisha ujenzi husika mpaka
kukamilika kwake na kuwa tayari kwa matumizi yaliyokusudiwa. Kawaida katika
miradi mingi kunakuwa na Mkandarasi mkuu na wakandarasi wadogo ambao kwa
magawanyo wa majukumu wao hufanya shughuli nyingine ambazo wengine hawawezi.
Ndio haswa wanaohusika na ufanikishaji wa huduma za jengo kama nilivyozifafanua
awali.
Mkandarasi
ninayemzungumzia hapa kisheria ni yule ambaye amepata leseni ya kufanya kazi
kutoka Bodi ya Makandarasi nchini (Contractors Registration Board).
Mpaka
kufikia hapa ni matumaini yangu kuwa kwa kiasi Fulani nimeweza kudadavua
maswala machache muhimu ambayo kimsingi yanatoa jibu la tunakosa nini
tusipotumia wataalamu kwenye ujenzi wa nyumba zetu. Kama umebahatika kupeleleza
nyumba zilizojengwa kwa kushirikisha wataalamu hata kwa hatua mojawapo na zile
ambazo zimejengwa bila kuwashirikisha utakubaliana name kuwa zilizoshirikisha
wataalamu zinaubora na umaridadi mzuri tofauti na zile ambazo hazikuhusisha
wataalamu hata kwa ushauri tu.
Tukutane
tena katika sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala hii ambapo tutaweza kufahamu sasa nini tunachokikosa.
Mwandishi/Mchambuzi
Tumainiel W. Seria
BSc. Building Economics (Hons), UCLAS
GQS (Registered with AQRB)
Director: S&L CostCare and Planners
P.O Box 16094 Arusha
+255757718080
seria.tw@gmail.com
No comments:
Post a Comment