Header Ads

Header Ads

WASANIFU MIRADI YA UJENZI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Eng. Jackson Masaka pamoja na viongozi wengine wa wilaya hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
_______
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameyataka makampuni yanayopewa kazi na Serikali ya kusanifu ujenzi wa barabara kufanya kazi hiyo kwa umakini kwa kutambua na kubainisha changamoto zitakazosababisha ucheleweshaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo hapa nchini.

Mhe. Kwandikwa ametoa maelekezo hayo wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti  na barabara za maingilio kwa kiwango cha changarawe mkoani Singida na kusisitiza kuwa wasanifu barabara wakifanya kazi kwa weledi kutasaidia Serikali kuweza kuepukana na usumbufu, ongezeko la gharama na ucheleweshwaji wa miradi hiyo.
“Changamoto za barabara ni zile zile katika maeneo mengi hivyo wasanifu waongeze weledi ili kusaidia mkandarasi kufanya kazi zake kwa wakati na haraka na hivyo kusaidia Serikali kutopoteza fedha kwa miradi mingi inayochukua muda mrefu”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Amezitaja changamoto ambazo zimesababisha ucheleweshwaji wa ujenzi wa daraja la sibiti na barabara za maingilio ikiwa ni ukutaji wa mawe mengi katika barabara hiyo na ongezeko wa makalvati ambapo hapo kwenye usanifu wa awali havikuwepo.
Aidha amemtaka mkandarasi China Henan International Corporation anayejenga daraja hilo kuongeza vifaa eneo la kazi ili kuongeza kasi ya ujenzi na kumaliza kwa muda uliopangwa.
Mhe. Kwandikwa amewatoa hofu wananchi wa mikoa ya Simiyu na Singida wanaounganishwa na daraja hilo kuwa mradi huo utakamilika mapema mwanzon mwakani.
“Mradi huu ni ukombozi katika kukuza uchumi wa mikoa hii, hivyo Serikali inajitahidi kila linalowezekana kuhakikisha unakamilika kwa wakati”, amesema Mhe. Kwandikwa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo, amemhakikishia Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa wataendelea kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili mradi ukamilike kwa wakati viwango vilivyokubaliwa katika mkataba.
“Maendeleo ya mradi mpaka sasa unaendelea vizuri na kazi zilizobaki ni uwekaji wa vyuma juu ya nguzo za daraja ambapo utakamilika hivi karibun”, amesema Eng. Kapongo.
Ujenzi wa daraja la sibiti lenye urefu wa mita 82 na upana wa mita 10.5 linalounganisha wilaya Mkalama na Meatu utahusisha na ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita 25 unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 18.1 ambazo zote zinagharamiwa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100

No comments: