HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA: UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI VYA UJENZI
Kibali cha ujenzi ni kibali kinachotokewa na mamlaka za Miji ama Majiji chini ya sheria ndogo za Udhibiti wa ujenzi Mjini. Kibali hiki kinatolewa ili kumruhusu Mwananchi afanye ujenzi au ukarabati wa jengo mahali fulani katika eneo la mji husika.
Katika makala ya leo, nakupitisha kwenye tataribu za kufuata ili kupata kibali cha ujenzi kwa kuangalia tataribu na kanuni za utoaji vibali hivyo kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Kabla ya hapo, kwanza tuangalie kwa pamoja umuhimu wa kupata kibali cha ujenzi.
1. Kutimiza matakwa ya sheria ndogo za Jiji
2. Kuwezesha kujenga majengo na nyumba kwa kuzingatia maelekezo ya mipango miji
3. Kudhibiti ujenzi holela na miji isiyopangika
Kanuni za Utoaji wa Vibali vya Ujenzi na Hatua za Kufuata
Hatua hizi zinaanza baada ya kuwa umeshakamilisha michoro ya jengo lako
1. Kuwasilisha michoro iliyokamilika na kujaza fomu maalumu inayotolewa na Halmashauri, fomu ambayo inajumuisha maoni ya wataalamu wafuatao
a. Mkaguzi wa Majengo wa Jiji (Building Inspector)
b. Afisa Ardhi wa Jiji (City Land Officer)
c. Mpima Ardhi wa Jiji (City Land Surveyor)
d. Afisa Mipango Miji wa Jiji (City Town Planning Officer)
e. Afisa Afya wa Jiji (City Health and Sanitation Officer)
2. Ukishawasilisha michoro iliyokamilika pamoja na kujaza fomu niliyotaja hapo juu, fomu itaambatanishwa na michoro husika (architectural na structural drawings) na kupita kwa wataalamu wote niliotaja kwa ajili ya uhakiki.
Wataalamu hao watapitia maombi yako na michoro na kujiridhisha yafuatayo.
a. Mkaguzi wa Majengo wa Jiji ataangalia kama michoro inakidhi haja ya kiufundi na masuala mengine ya kitaalamu
b. Afisa Ardhi wa Jiji ataangalia kuona kama umiliki wa eneo unalotaka kufanya ujenzi ni halali na umiliki wake ni sahihi
b. Mpima Ardhi wa Jiji atajiridhisha na mipaka halali ya eneo unalotaka kuendeleza
c. Afisa Mipango Miji atajiridhisha kama ujenzi unaoombewa kibali ni sahihi kwa mujibu wa michoro ya mipango miji kuendana na matumizi ya ardhi ya eneo husika
d. Afisa Afya wa Jiji atajiridhisha kuona kama usafi kwa ujumla na mfumo wa maji taka umezingatiwa
3. Kama nyaraka za umiliki zimekidhi vigezo, zitawasilishwa kwenye Kamati ndogo ya Mipango Miji na utoaji vibali
4. Endapo muombaji utakuwa umekamilisha hatua zote muhimu kwa wakati, kibali cha ujenzi kitapatikana ndani ya majuma mawili hadi manne.
Kumbuka, michoro unayotakiwa kuwasilisha ni ile ambayo imethibitishwa na wataalamu wabunifu wa michoro ya ujenzi ikiwa na mihuri halali, sambamba na kuwa na hati sahihi za umiliki wa eneo. Ukikamilisha haya zoezi linakuwa rahisi sana.
Makala ijayo tutaangalia ni madhara na hatari gani inaweza kukukumba endapo utajenga au kukarabati jengo lako ndani ya Jiji la Arusha bila kibali toka Halmashauri ya Jiji.
No comments:
Post a Comment