• Unataka Kujenga Ukuta Imara wa Nyumba Yako Utakaodumu Muda Mrefu?

    Ukuta wa nyumba ni sehemu muhimu na ya kudumu katika jengo lolote. Huweka uimara wa jengo na kudhibiti joto la nje na la ndani sambamba na kuweka usiri wa vitu vilivyomo ndani ya jingo. Hutoa ulinzi na kuweka usalma dhidi ya matukio ya hatari na wizi kwa vitu ama watu waliomo ndani.

  • Tunakosa nini Tusipotumia Wataalamu katika Ujenzi Wetu?

    Kushirikisha wataalamu kunatoa fursa ya kujua mbinu mpya na bora za ujenzi, kufaahamu vifaa vya ujenzi na sifa zake, kujua namna ya kupata gharama nafuu za ujenzi na usanifu majengo kuendana na ndoto yako binafsi.

  • Unafahamu Nini Ukinunua Simenti Imeandikwa 32.5N au 42.5N?

    Kuna madaraja matatu ya ubora/uimara wa simenti/saruji ambayo ni uimara wa chini 32.5, uimara bora zaidi ya ule wa chini 42.5 na uimara wa juu zaidi 52.5. Saruji ya gredi 52.5 bado haijaanza kuzalishwa kwa soko la Tanzania. Hii ni kusema kwamba tuna gredi ya 32.5 na 42.5 tu.Simenti ya daraja la chini la ubora 32.5 inafaa zaidi kwa matumizi ya plaster na kazi ndogo ndogo, na ile ya daraja la juu zaidi yani 42.5 inafaa zaidi kwa kazi za zege kama nguzo, bimu, slabu, madaraja n.k kutokana na uimara wake kuwa mkubwa zaidi.

Friday, October 21, 2016

TASWIRA: RAIS MAGUFULI ALIVYOWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI HOSTEL ZA WANAFUNZI UDSM


Leo October 21 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni 20 ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mwezi Juni mwaka huu wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho.
Wakati Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi la mradi huo, tayari ujenzi umefikia asilimia 75 ambapo majengo 20 yaliyounganishwa kimuundo yamefikia ghorofa ya nne na ujenzi huo unaofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba, 2016.
Rais Magufuli ameahidi kuwa, kwa kuwa majengo hayo yanauwezo wa kubeba ghorofa sita, Serikali itafanya utaratibu wa kutumia moja ya likizo za wanafunzi kuongeza ghorofa nyingine mbili ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata nafasi.
1
Rais Magufuli akikata utepe kabla ya kuweka jiwe la msingi
1
5
Rais Magufuli na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandara

7
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania TBA Arch. Elius Mwakalinga akitoa ufafanuzi kwa Rais Magufuli kuhusu ujenzi wa Hosteli
7

PICHA ZOTE NA MAELEZO: MILLARDAYO.COM

HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA: UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI VYA UJENZI

Kibali cha ujenzi ni  kibali kinachotokewa na mamlaka za Miji  ama Majiji chini ya sheria ndogo za Udhibiti wa ujenzi Mjini. Kibali hiki kinatolewa ili kumruhusu Mwananchi afanye ujenzi au ukarabati wa jengo mahali fulani  katika eneo la mji  husika.

Katika makala  ya leo, nakupitisha kwenye tataribu za kufuata ili kupata kibali cha ujenzi kwa kuangalia tataribu na kanuni za utoaji vibali hivyo kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Kabla ya hapo, kwanza tuangalie kwa pamoja umuhimu wa kupata kibali cha ujenzi.
1. Kutimiza matakwa ya sheria ndogo za Jiji
2. Kuwezesha kujenga majengo na nyumba kwa kuzingatia maelekezo ya mipango miji
3. Kudhibiti ujenzi holela na miji  isiyopangika

Kanuni za Utoaji wa Vibali vya Ujenzi na Hatua za Kufuata
Hatua hizi zinaanza baada ya kuwa umeshakamilisha michoro ya jengo lako
1. Kuwasilisha michoro iliyokamilika na kujaza fomu maalumu inayotolewa na Halmashauri, fomu ambayo inajumuisha maoni ya wataalamu wafuatao
a. Mkaguzi wa Majengo wa Jiji  (Building Inspector)
b. Afisa Ardhi wa Jiji (City Land Officer)
c. Mpima Ardhi wa Jiji (City Land Surveyor)
d. Afisa Mipango Miji  wa Jiji (City Town Planning Officer)
e. Afisa Afya wa Jiji (City Health and Sanitation Officer)

2. Ukishawasilisha michoro iliyokamilika pamoja na kujaza fomu niliyotaja hapo juu, fomu itaambatanishwa na michoro husika (architectural na structural drawings) na kupita  kwa wataalamu wote  niliotaja kwa ajili  ya uhakiki.

Wataalamu hao watapitia maombi yako na michoro na kujiridhisha yafuatayo.
a. Mkaguzi wa Majengo wa Jiji ataangalia kama michoro inakidhi haja ya kiufundi na masuala mengine ya kitaalamu
b. Afisa Ardhi wa Jiji ataangalia kuona kama umiliki wa eneo unalotaka kufanya ujenzi ni  halali na umiliki wake ni  sahihi
b. Mpima Ardhi wa Jiji atajiridhisha na mipaka halali ya eneo unalotaka kuendeleza
c. Afisa Mipango Miji  atajiridhisha kama ujenzi unaoombewa kibali ni  sahihi kwa mujibu wa michoro ya mipango  miji  kuendana na matumizi ya ardhi  ya eneo husika
d. Afisa Afya wa Jiji atajiridhisha kuona kama usafi kwa ujumla na mfumo wa maji taka umezingatiwa

3. Kama nyaraka za umiliki zimekidhi vigezo, zitawasilishwa kwenye Kamati ndogo ya Mipango Miji  na utoaji vibali 

4. Endapo muombaji utakuwa  umekamilisha hatua zote muhimu kwa wakati, kibali cha ujenzi kitapatikana ndani ya majuma mawili hadi  manne.

Kumbuka, michoro unayotakiwa kuwasilisha ni  ile ambayo imethibitishwa na wataalamu wabunifu wa michoro ya ujenzi ikiwa na mihuri halali, sambamba na kuwa na hati sahihi za umiliki wa eneo. Ukikamilisha haya zoezi linakuwa rahisi sana.

Makala ijayo tutaangalia ni  madhara na hatari gani inaweza kukukumba endapo utajenga au kukarabati jengo lako ndani ya Jiji la Arusha bila kibali toka Halmashauri ya Jiji.